Uelewa mdogo
juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia umesababisha baadhi ya wanawake kufanyiwa vitendo vya
ukatili ikiwemo kunyanganywa mali na kutelekezwa na watoto katika Kata ya
Tinde halmashauri ya Shinyanga na
kushindwa kuripoti matukio hayo .
Hayo
yamebainika katika utafiti uliofanywa na Klabu ya waandishi wa habari Kata ya
Tinde kupitia mradi wake wa nafasi ya vyombo vya habari katika kumaliza ukatili
kwa wanawake na watoto unaofadhiliwa na
mfuko wa wanawake Tanzania (WFT)ili kubaini changamoto zilizopo na kuchukuwa
hatua ya kumaliza tatizo hilo.
Afisa
maendeleo ya jamii Kata ya Tinde Eva Mlowe amesema wanawake wengi wamekuwa
wakifanyiwa vitendo vya ukatili ndani ya familia zao,lakini wamekuwa waoga na kushindwa kutoa taarifa kutokana na mfumo dume kwa kuogopa kuvunja ndoa zao ama kutengwa kwenye ukoo.
“Ukatili
mkubwa unaofanyika hapa Kata ya Tinde ni wanawake kunyanyaswa na waume
zao,utakuta mwanaume mwingine anaowa mwanamke halafu anampeleka kwenda kuishi
naye ndani ya nyumba anayoishi na mke wake wa ndoa na wakati mwingine anauza mali za familia yakiwemo mazao bila kumshirikisha mke wake na hela anakwenda kunywea pombe”,alisema.
Ukatili
mwingine ni vipigo na baadhi ya wanaume kuuza mazao waliyolima na wake zao na
kwenda kuyahifadhi lakini baada ya muda kupita wamekuwa wakiwadanganya kuwa
wameibiwa,kitendo ambacho kimekuwa kikichochea vitendo vya ukatili ndani ya
familia.
Katika
mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na
watoto,baadhi ya wakazi wa Kata hiyo akiwemo Hashimu Mkalambati amesema hatua
inayopaswa kuchukuliwa kukomesha matukio
hayo ni jamii kuendelea kupatiwa elimu pamoja na madawati ya jinsia yashuke
hadi nganzi ya Kata kusogeza huduma karibu.
Pili
Abdallah mkazi wa Tinde mama wa watoto wawili amesema alifanyiwa ukatili na
mume wake baada ya kufukuzwa na kunyanganywa mali zote walizotafuta pamoja
kisha mwanaume akaowa mwanamke mwingine na kumtelekeza na watoto lakini hakujua
kama huo ni ukatili aliofanyiwa kutokana na kutokuwa na uelewa.
Katika utafiti uliofanywa na timu ya waandishi wa habari Kata ya Tinde umebaini kuna ukatili mkubwa wanaofanyiwa wanawake lakini kutokana na kukosa uelewa wa matukio wanayofanyiwa wamekuwa wakiona na kawaida kufanyiwa vitendo hivyo ambapo elimu bado inahitaji kuendelea kutolewa ili kuwawezesha kupata uelewa zaidi.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya Shinyanga Hoja Mahiba amesema kutokana na kushamili
matukio ya ukatili wa kijinsia,wameamuwa kutumia jeshi la jadi
(Sungusungu)kuwadhibiti watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa wanawake na
watoto.
Amesema pia viongozi wa ngazi za vijiji wamewataka kuweka sheria ndogo ambazo zitatumika kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kama wanavyofanya katika matukio mengine.
Afisa elimu msingi Kata ya Tinde Vumilia Mauna amesema kwa sasa ukatili mashuleni umepungua kutokana na elimu iliyotolewa ikiwa ni pamoja na walimu kuepuka kutoa adhabu kali ambazo zinaweza kuwa chanzo cha ukatili kwa watoto.