MKURUGENZI TAMWA ZANZIBAR ASISITIZA UMUHIMU WA TAKWIMU ZA KIUCHUMI KUSAIDIA USTAWI WA WANAWAKE

Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar Dkt. Mzuri Issa Ally alipokua akizungumza na washiriki wa kongamano la siku moja la kuadhimisha siku ya mwanamke katika ukumbi wa ZURA Maisara mjini Unguja.

Na Muhammed Khamis, Zanzibar
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar Dkt,Mzuri Issa Ally amesema kuwepo kwa takwimu sahihi za kiuchumi kwa wanawake kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ustawi wa wanawake na kuweka mipango mizuri ya maendeleo visiwani Zanzibar.

Aliyasema hayo katika kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani lililofanyika katika ukumbi wa ZURA Maisara mjini Unguja.

Alisema hadi sasa Zanzibar hakuna takwimu sahihi za za kiuchumi ambazo zinaonyesha kipato cha mwanamke hali ambayo inapelekea kutokujua uhalisia wa ongezeko la pato kwa jamii hususani wanawake kwa kuwa takwimu hizo hujumlishwa kwa watu wote na hakuna mgawanyo wa wanaume na wanawake.

‘’Pamoja na mafanikio makubwa ya wanawake katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, bado kuna changamoto zinazowakabili katika kufikia malengo yao,’’ aliongezea.

Katika hatua nyengine Dk. Mzuri alizitaja baadhi ya changamoto nyengine zinazowakabili wanawkae ikiwemo dhana potofu ya jamii kudhani kuwa mwanamke hawezi kushika nafasi za uongozi katika jamii.

Alisema kwa mitazamo hio imepelekea wanawake wengi wenye uwezo kukosa fursa muhimu ambazo zingewafanya waweze kuwainua wanawake wenzao pindi wangepatiwa fursa hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wanaume wa mabadiliko, Mohammed Jabir alisema mifumo katika vyama vya siasa isiyoweka wazi usawa wa wanawake na wanaume kwa kiasi kikubwa inawanyima wanawake fursa za uongozi.

Mohamed alitaja changamoto nyengine kuwa ni mifumo iliyojengeka ndani ya jamii, masuala ya rushwa sambamba na umaskini nao kwa kiasi kikubwa inarejesha nyuma juhudi za wanawake Zanzibar.

Nae Yahya Khatibu Haji ambae ni mtaalamu wa masuala ya maendeleo ya biashara, alisema bado wajasiriamali wa Zanzibar wanashindwa kutumia vyema maendeleo ya sayansi ya teknolojia jambo ambalo kwa sasa linachukua umuhimu wa pekee katika kufikia masoko.

“Kwa kweli ipo haja ya kuangalia namna ya kupata wateja na kufikia masoko kama hujui kutumia mitandao ni wazi kuwa watabaki nyuma kundi ambalo ni wanawake”, alisema.

Aidha aliitaja changamoto ya maradhi ya Corona kwa kiasi kikubwa imewaweka wanawake katika hali mbaya ya kiuchumi hasa kwa kuwa kundi kubwa la wanawake wanajishughulisha na biashara na ujasiriamali.

Akichangia katika kongamano hilo, Faida Mohamed Shaibu, ambae ni mjasiriamali wa bidhaa za kusindika, alisema wajasiriamali wengi wanalia na masoko, ushuru mkubwa, ukosefu wa vifungashio unasababisha changamoto mbalimbali za kufika mbali.

Nae Makamu mkuu wa chuo cha SUZA, Dk Zakia Mohamed, alisema wakati umefika sasa kwa wanawake kujitoa zaidi katika kufikia maendeleo.

Aliwataka wanawake waliopewa nafasi za uongozi kuzitumia vyema ikiwa ni pamoja na kujua shida za watendaji wa chini ili kufikia maendeleo ya taasisi.

“Uongozi ni dhima kubwa katika kufikia maendeleo ya dhati, ili kwenda sambamba na maendeleo hayo hakuna budi kuona kuwa wanatatua changamaoto kwa wanaowaongoza”, alisema.

Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka ambapo ujumbe wa Zanzibar ni ushiriki kamili wa wanawake katika vyombo vya kutoa maamuzi, kutokomeza udhalilishaji, ushiriki wao katika masuala ya kiuchumi ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.
Mtalamu wa kutoka Wizara ya biashara Zanzibar Yahya Khatib Haji alipokua akichangia kuhusu umuhimu wa wanawake katika biashara.
Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar akisisitiza jambo juu ya umuhimu wa wanawake katika uongozi.
Baadhi ya washiriki wa kongamano la siku ya wanawake Duniani walioshiriki.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464