MWANAHABARI AKUTWA AMEUAWA MSITUNI BAADA YA KUPOTEA KWA SIKU 3

Jennifer Itumbi enzi za uhai wake

Mwanahabari Mkongwe Nchini Kenya, Jennifer Itumbi amepatikana akiwa ameuawa baada ya kutoweka kwa siku 3, huku uchunguzi ukionyesha kwamba marehemu alinyongwa kabla ya mwili wake kutupwa msituni. 

Kulingana na Afisa Mkuu wa DCI wa Kilimani, mwili wa Jeniffer Itumbi ulipatikana katika msitu wa Ngong siku tatu baada ya yeye kuripotiwa kwamba ametoweka. 

 Jennifer alionekana mara ya mwisho Ijumaa, Machi 12 katika Ofisi za Tume ya Ardhi ambapo alikuwa akifanya kazi 

Hadi kifo chake, Jennifer ambaye ni mwandishi mkongwe wa habari kutoka Machakos, alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Tume ya Ardhi. 

Itumbi ambaye alikuwa mwanahabari kutoka kaunti ya Machakos aliripotiwa kutoweka Ijumaa, Machi 12, 2021 baada ya kufikishwa kazini na mumewe na aliripotiwa kuacha begi lake na simu ndani ya gari la mumewe kabla ya kuingia ofisini. 

Picha za CCTV zinaonyesha kwamba marehemu aliondoka ofisini dakika chache baadaye na haikubainika alikokuwa akielekea tokea hapo. 

Kulingana na taarifa za Capital FM, maafisa wa polisi walisema kwamba huenda Itumbi aliuawa na mwili wake ukatupwa msituni Ngong kabla ya kupelekwa City Mortuary. 

Tayari maafisa wa DCI wamemhoji mumewe na uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo chake. Mumewe Joseph Komu aliambia maafisa wa DCI kwamba aligundua baadaye kwamba mkewe alikuwa ameacha mkoba wake ndani ya gari. 

"Nilitoka karakana na nikaenda hadi ofisini mwake baada ya kugundua kwamba alikuwa ameacha simu na mkoba wake ndani ya gari, nilipofika ofisini, niliambiwa kwamba hayupo, nilishtuka lakini nilijua alikuwa salama," Komu aliambia DCI.  

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464