Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango
Na Damian Masyenene
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango amesema kuwa atafanya kazi kwa uaminifu na kukidhi matamanio makubwa ya Watanzania, Rais, Wabunge na chama chake (CCM) na kwamba hatokuwa msaliti kwa sababu ya fedha kama ambavyo Yuda Eskarioti alivyofanya kwa Yesu Kristo.
Dk. Mpango ametoa ahadi hiyo leo Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akila kiapo cha utumishi katika nafasi yake mpya ya Makamu wa Rais, huku akieleza kuwa hakutegemea kwamba yeye mtoto wa maskini kutoka Buhigwe angeweza kuteuliwa kuitumikia nafasi hiyo.
"Nitakuwa msaidizi mwaminifu na mzalendo wa nchi yangu, sitakuwa kama Yuda, nitatekeleza kwa bidii na weledi kazi zote utakazonilekeza, nitatekeleza majukumu hayo chini ya uongozi na utumishi wako. nitume nikachape kazi," amesema.
Makamu huyo wa Rais amesisitiza kuwa atashirikiana na viongozi wenzake, ambapo ameishukuru Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupitisha jina lake na wabunge waliompitisha kwa kura zote, na kwamba Bunge limekuwa hazina kubwa kwake kwani amevuna mengi katika kipindi chote alichokuwa ndani ya bunge.
"Nawashukuru wananchi wa Buhigwe Kigoma kwa kuniamini na kunipigia kura. Nawaomba watanzania kuniombea niweze kukidhi matarajio yao na niwe mnyenyekevu, mtii na nitakayesimamia maslahi ya wananchi wanyonge," amesema.
Akieleza namna alivyomuamini Dk. Mpango na kuamua kuteua jina lake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Dk. Mpango ni mcha Mungu, mchumi mahiri, mchapakazi, mzoefu, hodari na hana hili wala lile.
Rais Samia amekishukuru chama chake kwa kumuunga mkono na kulipitisha jina la Mpango, vilevile Bunge kwa kumpigia kura za kishindo na kupitishwa kwa asilimia 100.
"Nilizunguka sana kupata jina, nikaangalia ndani na nje ya Bunge, na mtu niliyemuona anafaa ni ndugu yetu Philip Mpango. Philip nilimkuta ametulia nikaona ndiye anafaa. majina mengine nilikuta yana hili mara lile.
"Atanisaidia kwenye uchumi na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali, nikaona ndiye mtu wa kwenda naye," amesisitiza.