Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Tanzania, Charles Kichere
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kicheere imeendelea kubaini dosari ya matumizi ya fedha yanayofanywa na taasisi na mashirika ya umma pamoja na vyama vya siasa.
CAG amesema kati ya hati 900 alizozikagua, hati 800 sawa na asilimia 87 zinaridhisha huku hati 81 zikiwa na mashaka na mbaya ni 10.
Kichere ameyasema hayo leo Jumapili, Machi 28, 2021 wakati akikabidhi ripoti aliyoifanya kwa taasisi za Serikali Kuu, mamlaka ya serikali za mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na vyama vya siasa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ulioishia Juni 30, 2020.
“Tumeongeza mashirika 10 ambayo tunayakagua na nimeshirikiana na makampuni mengine binafsi kuhakikisha tunakagua ipasavyo pia tumefanya kaguzi za kitaalamu SGR, miundombinu mabasi yaendayo haraka, barabara kuu Morogoro, Kibaha, miradi ya maji wilaya ya Same na Korogwe,” amesema.
Amesema mwenendo wa hati za ukaguzi na tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika ukaguzi mwaka 2019/2020, ametoa jumla ya hati 900 za ukaguzi.
“Hati 243 za serikali kuu 235 zinaridhisha na nyingine sita zina mashaka, mamlaka ya Serikali za mitaa ni 185 na kati ya hizo 124 zinaridhisha na zenye mashaka 53 na zilizokutwa ni mbaya ni nane.
“Mashirika ya umma nimetoa hati 165 na kati yake 162 zinaridhisha na zenye mashaka ni tatu. 290 ni hati za miradi ya maendeleo na kati ya hizo 275 zinaridhisha na zenye mashaka ni 15 na hapa hakuna hati mbaya,” amesema Kichere.
Kichere amesema alikagua hati 17 za vyama vya siasa kati ya hizo nne zinaridhisha na zenye mashaka ni nne, ambapo kati yake, ameshindwa kutoa maoni kutokana na mambo mbalimbali.
“Jumla kuu ya hati zenye mashaka ni 81, sawa na asilimia tisa na hati mbaya ni 10 sawa na asilimia moja na hati 90, nimeshindwa kutoa maoni sawa na asilimia moja,” amesema Kichere.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464