SHULE YA SEKONDARI SALAWE ILIVYOPUNGUZA MIMBA KUPITIA KLABU YA WANAFUNZI, DC NAE ATOA MAAGIZO KWA WALIMU

Wanafunzi wa Pambana Fema Club ya Shule ya Sekondari Salawe wilayani Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa shule hiyo, Faraja Mbilinyi (mwanamke) na mwalimu mlezi wa klabu, Daniel Masri

Na Damian Masyenene, Shinyanga
SHULE ya Sekondari Salawe yenye wanafunzi 746 ikiwa na bweni kwa wasichana 35 ipo katika kijiji chya Azimio kata ya Salawe katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, imetajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya mimba kwa wanafunzi iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Inaelezwa kuwa miaka minne nyuma, shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ilikuwa inapoteza wanafunzi wengi kwa kupata mimba, ambapo inatajwa kuwa kwa mwaka takribani wanafunzi 20 wa kike walikuwa wanaacha masomo kutokana na ujauzito.

Shinyanga Press Club Blog imefanya mahojiano na walimu, wanafunzi, Diwani wa kata na shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kwa jamii katika mradi wa ‘Nafasi ya vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto’ unaotekelezwa na Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania (WFT).

Akielezea hali ilivyokuwa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Salawe, Faraja Mbilinyi alisema kuwa alihamishiwa shuleni hapo mwaka 2019 na kukuta kesi 19 za mimba kwa wanafunzi, lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa hali imepungua na kufikia mimba tatu kwa mwaka jana.

Mwalimu Mbilinyi alieleza kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuanzisha klabu ya wanafunzi ya kuelimisha juu ya tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya afya, inayoitwa ‘Pambana Fema Club’ ambayo sasa ina wanachama 88 wanaotoa elimu ya jinsia, kutokomeza ukatili kwa wanafunzi na watoto na kuelimisha rika kupitia kupitia mikutano na vikundi.

“Hali ilikuwa siyo nzuri sana lakini tunashukuru sasa hali inakwenda vizuri kadri siku zinavyokwenda, nawashukuru walimu, kikundi cha FEMA na waelimishaji rika kutoka maeneo mbalimbali. Lengo letu ni kutokuwa na mimba kabisa,” alisema.

Mwalimu huyo alisistiza kuwa tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na kulega kwa malezi katika familia kwani amefanya ufuatiliaji kwa baadhi ya wanafunzi wanaopata mimba wazazi huwa hawafahamu lolote, ambapo ameshauri kuwa ili kukomesha kabisa na kuhakikisha hali inaendelea kuwa vizuri, ni vyema wazazi wasiwaache watoto na kuwapa uhuru uliopitiliza bila kufanya ufuatiliaji.

Baadhi ya wanafunzi wa kike ambao ni wanachama wa klabu hiyo walieleza kuwa Pambana Fema Club imekuwa msaada kwa wanafunzi wengi, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kwani kupitia elimu wanayoitoa imeweza kubadilisha fikra na kuwakomboa watoto wa kike.

Mmoja wa wanafunzi hao, Paulina Fabian wa kidato cha nne, alisema kuwa klabu yao imekuwa ikitoa ushauri, elimu ya jinsia na hutoa msaada kwa wanafunzi wa kike wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwashauri na kutoa taarifa kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo polisi na taasisi zingine ili kuwanusuru na vijana waharibifu.

Naye Agness Mwininga wa kidato cha tatu alieleza kuwa kupitia shughuli zinazofanywa na klabu hiyo ameweza kupata elimu ya vishawishi mbalimbali wanavyokutana navyo wasichana wengi hususani kutoka kwa wanaume katika kata hiyo wakiwemo waendesha pikipiki na kujiingiza kwenye mahusiano katika umri mdogo.

Kwa upande wake, Mwalimu Mlezi wa klabu hiyo, Daniel Masri alisema kuwa mwaka 2018 ziliripotiwa mimba zaidi ya 20, mimba 8 mwaka 2019 na tatu mwaka jana na kwamba klabu hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupitia majarida wanayoyapata, kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule jirani na shule za msingi na mitaani kupitia mikutano.

“Kulikuwa na tatizo kubwa la mimba, kwahiyo kushirikiana na wadau wa masuala ya kijinsia na afya wakaona itafutwe namna ya kukomesha ukatili huu kwa wanawake na watoto ndipo ikaundwa hii klabu mwaka 2017 na sasa ina wanachama 88 wakiwemo wavulana 40 na wasichana 48,” alisema.

Upande wa Serikali ya kijiji na Kata nao haukuwa nyuma kuhakikisha watoto wa kike wanasalimika na tatizo la mimba za utotoni, ambapo Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu alisema kuwa walilazimika kukaa pamoja viongozi wa serikali za mitaa na kupitisha mikakati ikiwemo kuwakamata wahusika na kuwawajibisha kupitia Sungusungu ikiwemo kuwatenga kwenye kijiji.

Alisisitiza kuwa wazazi wengi wa watoto waliokuwa wanakutwa na tatizo hilo walikuwa hawajitokezi kusaidia mamlaka kuchukua hatua, ambapo hadi sasa ni watu zaidi ya 10 waliokamatwa na kuchukuliwa hatua.

“Hapo nyuma tatizo lilikuwa kubwa, kwahiyo tulikaa tukaelewana viongozi tukapitisha kwamba sungusungu watusaidie kupambana na vita hii, imetusaidia kutujenga na kutubadilisha na pia tukatoa elimu kwa wanafunzi na wananchi, kwahiyo naweza kusema imepungua kutoka asilimia 100 hadi 40,” alibainisha.

Akieleza hali ilivyokuwa katika kata ya Salawe juu ya mimba kwa wanafunzi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko alisema kuwa alikasirishwa na matukio hayo kwani yalikithiri katika shule hiyo na kuleta aibu, lakini sasa anaridhishwa na juhudi inazofanyika kutokomeza mimba kwa wanafunzi.

DC Mboneko aliwataka wananchi kutafuta wanawake wa rika lao na kuwaacha wanafunzi wasome, huku akiagiza mkuu wa shule kuhakikisha kuwa mwaka huu hakuna mwanafunzi wa kike atakayepata mimba shuleni hapo.

“Tafuteni saizi yenu, niachieni watoto wangu wa shule, ogopeni kabisa sketi za wanafunzi msiwasumbue kabisa na wazazi tusaidiane kulea, tuwafuatilie watoto wetu na tusiwaachie uhuru uliopitiliza. Mwaka huu nisisikie kuhusu mimba hapa, wanafunzi waelimishwe na kushauriwa kuepuka mimba,” alisisitiza.
Wanachama wa Pambana FEMA Club wakiwa katika picha ya pamoja na walimu wao
Wanachama wa Pambana Fema klabu wakiwa katika picha ya pamoja na Mwalimu wao mlezi, Daniel Masri (kushoto) na Mwenyekiti wa taasisi ya Women For Change, Getrude Munuo, shuleni hapo.
Wanaklabu hao wakiimba wimbo maalum wa kupinga mimba kwa wanafunzi shuleni hapo





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464