SHUWASA YAZINDUA MRADI WA MAJI UTAKAONUFASHA WANANCHI 15,429, DC MBONEKO ATOA UJUMBE MZITO



Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akifungua maji, mara baada ya kumaliza kuzindua mradi wa maji safi na salama Kata ya Mwawaza mjini Shinyanga.

Na Marco Maduhu - SHINYANGA
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), imezindua mradi wa maji ya Ziwa Viktoria katika Kata ya Mwawaza- Negezi Manispaa ya Shinyanga, ambao utanufaisha wananchi wapatao 15,429 na kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye Kata hiyo ya Mwawaza, ikiwa ni siku ya uzinduzi wa wiki ya maji duniani, ambapo mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza kwenye uzinduzi huo wa mradi huo amesema utekelezaji wake ulianza Februari mwaka jana, na umekamilika Machi mwaka huu na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Amesema mradi huo awali ulikuwa utekelezwe na Mkandarasi kwa gharama ya Sh. bilioni 2.0, lakini ukatekelezwa kwa nguvu za wananchi (force account) kwa Sh. bilion 1,4 na sasa umeshakamilika kwa kutumia gharama nafuu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, amewataka wananchi waitunze miundombinu ya mradi huo wa maji, ili udumu kwa muda mrefu na kuondokana na adha ya maji.

Pia amewataka wasimamizi wa vituo vya kuchotea maji hayo wawepo muda wote, pamoja na kutunza fedha vizuri za mauzo ya maji, ili mradi huo upate kujiendesha na kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi bila ya kikwazo.

Aidha Mwenyekiti wa bodi ya SHUWASA, Mwamvua Jilumbi, amewataka wananchi wawe wanajenga utamaduni wa kulipa ankra zao za maji kwa wakati, ili ipatikane fedha ya kuongeza mtandao wa kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote.

Nao baadhi ya wananchi wa Mwawaza akiwamo Mwatano Salumu, wameshukuru kuzinduliwa mradi huo wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, na kubainisha mbali na kuondoa adha ya kutumia maji ya siyo salama na kuwatua ndoo kichwani, pia umeokoa ndoa zao kutovunjika sababu waume zao walikosa imani nao kutokona na kukawia kurudi nyumbani.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza mara baada ya kumaliza kuzindua mradi wa maji Mwawaza- Negezi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, akitoa taarifa za ujenzi wa mradi huo wa maji.

Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya maji SHUWASA, Mwamvua Jilumbi, akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa maji Mwawaza- Negezi.
 
Katibu wa Itikadi na uenezi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Said Bwanga, akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo wa maji.
 
Diwani wa Mwawaza Juma Nkwabi akizungumza kwenye uzinduzi huo wa mradi wa maji.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akikata Utepe kuzindua mradi wa maji Mwawaza-Negezi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akifungua jiwe la msingi kwenye uzinduzi wa mradi wa maji Mwawaza-Negezi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akifungua maji, mara baada ya kumaliza kuzindua mradi wa maji.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akimtwisha Ndoo Mwanamke Wile Shija mkazi wa Mwawaza, mara baada ya kumaliza kuzindua mradi wa maji.

Wanawake wa Mwawaza wakiendelea kutwishwa ndoo za maji na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Baadhi ya wananchi wa Mwawaza wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa maji.

Baadhi ya wananchi wa Mwawaza wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa maji.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464