Rais Samia Suluhu Hassan.
ZIKIWA zimesalia siku saba kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpata makamu wa rais mpya, gumzo limeibuka kuhusu jina la mtu atakayeteuliwa na kuidhinishwa na Bunge kushika wadhifa huo.Hatua hiyo imekuja baada ya shughuli za maziko ya mwili wa aliyekuwa Rais awamu ya tano, Dk.
John Magufuli kuhitimishwa jana nyumbani kwake Chato mkoani Geita.Kukamilika kwa shughuli hiyo, sasa kunatoa fursa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza takwa la Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 47 (4) kwa kuteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais.
Samia alikuwa Makamu wa Rais kwa Rais Magufuli kwa zaidi ya miaka mitano, kabla ya kuapishwa Machi 19 mwaka huu kuwa Rais.Rais Samia amechukua nafasi hiyo kufuatia kifo cha Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Aidha, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 47(4) inasema, ikitokea kwamba kiti cha Makamu wa Rais kipo wazi, basi mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote ndani ya siku zisizozidi 14 baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura za wabunge walio wengi.
Kutokana na hali hiyo, macho na masikio ya Watanzania sasa yameelekezwa katika katika jina la Makamu wa Rais atakayeteuliwa kushika wadhifa huo.
MAKADA WANAOTAJWA
Ni dhahiri kwa vyovyote vile jina la mtu atakayeteuliwa atatokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama dola.
Hali hii inatafsiriwa kuibua gumzo hasa ikizingatiwa atakayeteuliwa lazima awe na kariba au sifa za urais kama ilivyotokea kwa Mama Samia.Kutokana na hali hiyo, baadhi ya majina yamekuwa yakiibuliwa na wachambuzi mbalimbali wa kisiasa na hata katika mitandao ya kijamii kujaribu kubashiri jina la mteule huyo.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa baadhi ya mawaziri wa sasa na hata waliowahi kuwa mawaziri kwenye Serikali ya Muungano wanatajwa kuwa huenda wakarithi nafasi ya makamu wa Rais.
Kutajwa kwao pia kumeenda sambamba na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kinachokutana mwishoni mwa wiki iliyopita chini ya Makamu mwenyekiti Bara, Philip Mangula na makamu mwenyekiti visiwani, Dk. Ali Mohamed Shein na kutoa maagizo kadhaa ikiwamo kuitisha mkutano wa Halmashauri Kuu na Mkutano mkuu wa chama hicho kuidhinisha jina la Mama Samia kuwa Mwenyekiti.
Mbali na hilo, baadhi ya majina ambayo yanatajwa na wachambuzi wa kisiasa ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk. Emanuel Nchimbi. Nchimbi pia aliwahi kuwa waziri na mbunge katika serikali ya awamu ya nne.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.Wamo pia Waziri wa Mambo ya nje, Prof. Palamagamba Kabudi, Balozi wa Tanzania nchini Denmark, Dk. Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu Kiongozi, Bashiru Ali, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
ORODHA YA MAKAMU WA RAIS WA TANZANIA
Historia ya walioshika ofisi hiyo ya makamu wa rais ni hawa wafuatao:
Abeid Amani Karume 1964 – 1972
Mwinyi Aboud Jumbe 1972 – 1984
Ali Hassan Mwinyi 1984 – 1985
Joseph Sinde Warioba 1985 -1990
John Samuel Malecela 1990 -1994
Cleopa David Msuya 1994 -1995
Omar Ali Juma1995 – 2001
Ali Mohamed Shein2001- 2010
Mohamed Gharib Bilal 2010 -2015
Samia Hassan Suluhu 2015 – 2021
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464