Mwandishi wa habari, Shaban Njia (kushoto) akimuelekeza jambo mmoja wa wakazi wa kata ya Mwakitolyo, Neema Tabu (katikati) juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia wanayokutana nayo
Na Shaban Njia, Shinyanga
WAKAZI wa Kata ya Mwakitolyo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa,wameiomba Serikali kuwapatia elimu ya ukatili wa kijinsia ili kutambua wapi wanatakiwa kwenda kutoa taarifa baada ya kufanyiwa vitendo vya kikatili na waume zao au watu wanaowazunguka.
Hayo waliyabainisha jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii aliyefika katika kata hiyo kufahamu mambo mbalimbali yanayohusu ukatili wa kijinsia chini ya Mradi wa nafasi ya vyombo vya habari katika kumaliza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaotekelezwa na Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania (WFT).
Mmoja wa wakazi hao, Chausiku Manyabili alisema kwamba wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili na waume zao lakini hawatambui kama ni ukatili na kubaki kuendelea kuumia na kwamba wangekuwa na elimu hiyo wangekuwa wanatambua wapi wanatakiwa kupeleka malalamiko yao na kupata msaada.
“Sisi hatufahamu kama kukimbiwa waume zetu nao ni ukatili, tunakimbiwa sana hasa familia inapoongezeka,tunaona kawaida na hatuwezi kulalamika mahala popote pale,laiti tungekuwa na elimu ya kutambua kwa upana dhana ya ukatili wa kijinsia tungejitokeza kutoa malalamiko yetu,” alisema Samweli.
Naye Neema Tabu alisema watoto wadogo hasa wa kike wenye umri wa kwenda shule wanashindwa kwenye shuleni kwa kukosa mahitaji kutoka kwa wazazi wa kiume ambao wanatumia muda mwingi katika shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kuhudumia familia na kupeleka watoto shuleni.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Mwakitolyo, Mussa Gongo alisema kuwa amekuwa akishirikiana na kamati za mtakuwwa katika kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia lakini wananchi wanapojitokea na kukuta hakuna ajenda ya uchimbaji wa madini wanaondoka.
Aidha, amebainisha kuwa kwa siku anapokea kesi zaidi ya sita za wanawake kuachwa na kunyimwa matumizi na waume zao na asilimia kubwa ya kesi hizo zinatoka katika vijiji vya Mwakitolyo na Nyaligogo na haiwezi kupita siku mbili kesi za ukatili wa kijinsia hazijaripotiwa.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwakitolyo, Samson Lutonja aliwataka akinamama kuacha tabia ya kukimbia mikutano ya hadhara wakati wa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa ya vitendo vya kikatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa kwenye jamii ili vipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Mwandishi wa habari, Shaban Njia (kushoto) akimuelekeza namna ya kujaza dodoso, mmoja wa wakazi wa kata ya Mwakitolyo, Neema Tabu (katikati) juu ya masuala ya ukatili wanayokutana nayo