Mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi juu ya
umuhimu wa kuchangia chakula mashuleni ili kuwawezesha watoto wao kupata
chakula cha mchana kutokana na kuishi mbali na shule ,imekuwa ni chanzo cha
wanafunzi kuwa watoro ambapo wastani wa wanafunzi 70 wanakosa masomo kwa siku.
Hayo
yamebainika baada ya timu ya waandishi wa habari kutembelea shule ya sekondari
Didia iliyopo Kijiji cha Bukumbi,wakati wakiwa katika utafiti wa masuala ya
ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na kuzungumza na wanafunzi pamoja na
walimu.
Utafiti huo
wa masuala ya ukatili wa kijinsia unafanywa na Klabu ya waandishi wa habari
Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na mfuko wa wanawake Tanzania (WFT) ili
kuhakikisha matukio yote ya ukatili wa kijinsia yanaibuliwa na kufanyiwa kazi
ili kukomesha vitendo hivyo.
Mkuu wa
shule ya sekondari Didia Mwalimu Faustine Magesa amesema wanafunzi wamekuwa
wakishinda na njaa kuanzia asubuhi hadi saa 9.30 jioni muda wa kutoka
shule,huku baadhi yao wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita kumi hadi kufika
shule.
Amesema
wanafunzi wanaposhinda na njaa wanakumbana na changamoto ya kujiingiza kwenye
vitendo ambayo vimekuwa vikiharibu ndoto zao hasa kwa wasichana kurubuniwa na
kuishia kupewa ujauzito na watu wanaowasaidia fedha.
“Ni kweli changamoto
ni nyingi njiani ambazo wanakumbana nazo ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili
wa kijinsia na wengine kupata ujauzito na kwa mwaka jana 2020 wasichana wanne
walipata mimba,pia wanatoka nyumbani alfajiri ili kuwahi shule wanaweza
kunyanganywa hata baiskeli”alisema Magesa.
Nao baadhi
ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo akiwemo Haji Ramadhan na Irine Mponda
wamesema changamoto ni kubwa kutokana na shule hiyo kujengwa mbali na makazi ya
watu,ambapo njiani wamekuwa wakifiziwa na watu ili wachukuwe baikeli
wanazotumia baadhi ya wanafunzi.
Mwanafunzi
Irine amesema vishawishi ni vingi kwa watoto wa kike ambapo wavulana
wanawasubiri njiani na kuwalazimisha kuwa na uhusiano wa kimapenzi jambo ambalo
wamekuwa wakiripoti kwa walimu walimu wao na kisha kufanya ufuatiliaji ili
kuwabaini.
Afisa elimu
Kata ya Didia Justus Bilago alisema kulikuwa na ndoa za utotoni nyingi lakini
baada ya elimu kutolewa hali imebadilika,ambapo wanafunzi na jamii nzima
imekuwa na ushirikiano mkubwa wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Shinyanga
Hoja Mahiba alisema anaitambua changamoto ya wanafunzi kusoma umbali mrefu na
kwamba suala hilo wanalifanyia kazi na mkakati uliopo ni kujenga mabweni pamoja
na shule nyingine ya sekondari.
Alisema matukio ya ukatili wa kijinsia bado yanaendelea kutokea maneo mbalimbali katika halmashauri hiyo zikiwemo ndoa na mimba za utotoni ambapo baada ya rikizo ya Corona mwaka 2020 wanafunzi 26 waligundulika kuwa na mimba.