Header Ads Widget

WANANCHI SHINYANGA WASHAURIWA KUPIMA FIGO KUEPUKA MADHARA NA GHARAMA KUBWA ZA MATIBABU

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake 

Na Damian Masyenene, Shinyanga
TANZANIA inaungana na mataifa mengine Duniani leo Machi 11, 2021 kuadhimisha Siku ya Figo, huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zikionyesha kuwa, asilimia 10 ya watu duniani wameathiriwa na ugonjwa sugu wa figo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, takwimu zinaonyesha kuwa, Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa sugu wa figo kati ya 4,800 hadi 5,200 ambao wanahitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Kati ya hao wagonjwa 1000 wanapata huduma ya usafishaji wa damu kwa sasa, hadi kufikia Novemba, 2020 jumla ya wagonjwa 316 wamepandikizwa figo katika hospitali mbalimbali. Mathalani, hapa nchini jumla ya wagojwa 78 wamepandikiwa Figo na Madaktari wazawa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (62) na Hospital ya Benjamin Mkapa (16) na waliobaki wamepandikizwa nchini India.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni 'Ishi Salama, na Ugonjwa wa Figo', kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha ushirikishwaji wa mgonjwa wa figo, familia, jamii na marafiki wanaowahudumia waathirika wa ugonjwa sugu wa Figo kuhusu tiba na afya yake ili aweze kuishi salama na ugonjwa wa Figo.

Katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kuchukua tahadhari mapema, Shinyanga Press Club Blog imefanya mahojiano na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John ambaye amewasihi wananchi kufanya vipimo vya mara kwa mara ili kubaini tatizo mapema na kuepuka gharama kubwa za matibabu.

Dk. Luzila ambaye pia ni Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, amesema kuwa endapo wananchi watajenga utamaduni wa kupima afya hususan vipimo vya tatizo la Figo itawasaidia kubaini kama wana tatizo na kuchukua hatua mapema kabla tatizo halijawa kubwa na kujiweka hatarini, hususan kwa watu waliofikisha miaka 40 na kuendelea wanapaswa kufanya vipimo kila mara skwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Katika hatua nyingine, Dk. Luzila ametahadharisha wananchi dhidi ya matumizi holela na makubwa ya dawa hususan za kienyeji bila kiwango maalum na ushauri wa kitaalam kwani hupelekea mwili kuwa na sumu nyingi na kuathiri Figo.

Nawahamasisha watu wa Shinyanga waende kwenye huduma zinazotoa vipimo hivi ikiwemo hospitali yetu ya rufaa kwa sababu gharama za vipimo zinawezekana…..hata hapa wagonjwa wapo na wanakuja, mfano leo (Jana) tumempa rufaa mgonjwa mgonjwa mwene tatizo la figo ambaye yuko ‘stage’ ya tano kwenda Bugando na tatizo lake halikugundulika mapema.

Ukifuatiia matibabu ya hatua hii kwa ‘session’ moja ni kama Sh 900,000 na anatakiwa awe na vipindi viatu kwa wiki, kwahiyo ni gharama sana. Kwahiyo, tufanye vipimo vya mara kwa mara walau mara moja kwa mwaka na mgonjwa wa Kisukari afanye hivyo mara moja kila baada ya miezi mitatu,” alisema.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, viashiria vikuu vya ugonjwa wa Figo ni pamoja na, Shinikizo la juu la damu (Hypertension), Kisukari (Diabetes) na Maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo (recurrent UTI).

Kinga ya ugonjwa sugu wa figo ni kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula lishe bora na kamili, kunywa angalau lita moja na nusu ya maji kwa siku, usafi wa mwili, kutokuvuta sigara au kunywa pombe kupita kiasi pamoja na kudhibiti shinikizo la juu la damu, kisukari na maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John 



Post a Comment

0 Comments