Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika Machi 8, 2021 katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, ambapo aliwataka wanawake kujitambua na kuripoti matukio ya ukatili wanayofanyiwa, kujikwamua kiuchumi na kuacha utegemezi ili kutokomeza vitendo hivyo (Picha: Marco Maduhu)
Salvatory Ntandu Na Damian Masyenene, Shinyanga
KATIKA jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga, asasi za kiraia, taasisi, mashirika yanayojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto zimeombwa kutoa elimu katika uwanda mpana kwa wanaume juu ya athari zitokanazo na ukatili ili kutokomeza matukio hayo kwenye jamii.
Ombi hilo limetolewa jana kwa nyakati tofauti na baadhi ya wanawake katika Kata ya Salawe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani humo, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hii alipofika katika kata hiyo kuibua na kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa nafasi ya vyombo vya habari katika kutokomeza janga hilo kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Tanzania (WFT).
Wanawake hao walieleza kuwa kutokana na baadhi ya vitendo wanavyofanyiwa na wanaume kutokana na mfumo dume, wamejikuta wakibaki na ulemavu wa kudumu na baadhi kupoteza maisha.
Mmoja wa akina mama hao, Tabu Masunga mkazi wa kijiji cha Salawe alisema kuwa bado mwanamke wa kijijini ananyimwa uhuru wa kujieleza pamoja na kumiliki mali, hali ambayo imekuwa ikisababisha wengi wao kutelekezewa familia na waume wao pindi wanapouza mazao msimu wa kilimo.
“Hatuna uhuru hata wa kuazimisha jembe la mkono kwa jirani hadi mwanaume awepo aseme umpatie au la, mkivuna mazao mwanaume anauza yote na hauna haki ya kuuliza wakati mmelima pamoja, hatuna ruhusa ya kumiliki mali ikiwemo ardhi na mifugo,” alisema.
Naye Merry Kisandu mkazi wa Kijiji cha Kakola A katika kata hiyo, alisema kuwa wanaume wanapaswa kupewa elimu juu ya atahari za ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kuondokana na mfumo dume ambao umekuwa kandamizi kwa wanawake hususan maeneo ya vijijini.
“Tunaiomba Sertikali na wadau waongeze jitihada za kutoa elimu kwa wanaume ili wabadilike kifikra na kuachana na tabia za kuwanyanyasa wanawake kwa kuwapiga na kuwaachia majukumu mengi ya kulea familia peke yao na kusababisha watoto kukosa haki zao za msingi,” alisema.
Hata hivyo, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika Machi 8, 2021 katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema kuwa mwanamke ana haki zote ikiwemo kumiliki ardhi na mifugo, huku akiwataka wanaume waoendekeza mfumo dume kuachana na dhana hiyo potofu.
Vilevile, RC Telack aliwataka Wanawake kutoa taarifa za matukio ya ukatili wanayofanyiwa kwenye jamii ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
"Hatutaki kusikia mnalia ndani kwa vipigo, nendeni kwa viongozi wa vijiji, mitaa na hata polisi kwa lengo la kutokomeza matukio haya,” alisema Telack.
Kwa upande mwingine, matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yanatajwa kuongezeka mkoani humo, ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai, 2019 hadi Desemba 2020, jumla ya matukio 10, 354 ya ukatili yameripotiwa.
Kwa Mujibu wa Mpango Mkakati wa mkoa wa Shinyanga wa mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliozinduliwa mwaka jana, umeeleza kuwa baadhi ya kesi za ukatili zinazoripotiwa zimekuwa hazifikishwi mahakamani.
Ambapo, katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2019 jumla ya kesi 470 za ukatili ziliripotiwa katika dawati la jinsia, lakini ni kesi 159 tu zilizofikishwa mahakamani na 314 bado ziko chini ya uchunguzi wa polisi, huku kesi 21 tu zikihukumiwa kati ya hizo 159 zilizofunguliwa na 136 zikiwa bado kwenye uchunguzi.
"Vilevile, mwaka 2018 kati ya kesi 473 za ukatili wa kijinsia na watoto zilizoripotiwa bado kesi 146 bado ziko chini ya upelelezi wa polisi. Kesi nyingi bado zimekwama kutokana na ushirikiano hafifu kutoka kwa waathirika, familia za wahanga na wanajamii pamoja na kutokomea kwa watuhumiwa," ilisema ripoti hiyo.