WATAALAM WA KILIMO PEMBA WASHAURIWA KUONGEZA MBINU UZALISHAJI MAZAO BORA

Washiriki wa mafunzo kwa wataalam wa kilimo kisiwani Pemba kupitia mradi wa VIUNGO wenye lengo la kuwapatia wataalam hao taaluma ya mbinu bora za kuwafundisha wakulima juu ya mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya viungo, Mboga na Matunda

Na Mwandishi Wetu, Pemba
KATIKA kuhakikisha lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao bora ya Viungo, Mboga na Matunda yenye kuzingatia matumizi madogo ya pembejeo za kemikali, wataalam wa kili mo kupitia mradi wa Viungo Pemba wameshauriwa kutumia zaidi mbinu za viwango endelevu vya hiari kwa wakulima ili kufikia malengo hayo.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Biashara na Masoko, Omar Mtarika wakati wa mafunzo kwa wataalam wa kilimo kisiwani Pemba kupitia mradi huo yenye lengo la kuwapatia wataalam hao taaluma ya mbinu bora za kutumia kuwafundisha wakulima juu ya mbinu bora za uzalishaji wa mazao hayo.

Alisema ni jukumu la wataalam wa kilimo kupitia mradi huo kutumia taaluma yao kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya ardhi pamoja na pembejeo za kilimo ili kuzalisha bidhaa bora na salama kwa walaji.

“Lengo la mradi wa huu ni kuhakikisha unawawezesha wakulima kuzalisha mazao bora, kwa wingi na kwa uendelevu, ili wakulima waweze kufikia malengo haya ni lazima waelimishwe kuhusu taaluma hii ya viwango endelevu vya hiari kwa wakulima ili kusudi wazalishe kwa kuzingatia misingi ya kibiashara,” alisema.

Aidha alibainisha kuwa ufikiaji wa malengo ya mradi huo ni lazima wakulima wawe na uwezo wa kulima kilimo endelevu chenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira pamoja na masuala ya kijamii.

Aliongeza kwamba, ufikiaji wa malengo ya mradi yatapatikana kupitia wataalam hao kuwaelimisha zaidi wakulima kuhusu mbinu za kupunguza matumizi ya sumu yasiyo ya lazima katika mazao kwa kuzingatia vigezo vya haki za kibinadaam, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa maji na nishati.

Alisema, “Kufanya hivyo kutasaidia sana malengo ya mradi kukuza masoko endelevu ya biashara za wakulima zinazozalishwa kufanikiwa kwa haraka kutokana na wateja wengi duniani wako tayari kununua bidhaa zilizozalishwa kwa ubora wa hali ya juu bila kuwa na chembechembe za sumu katika uzalishaji wake.”

Meneja wa mradi huo kanda ya Pemba, Sharif Maalim Hamad alisema kutokana na muundo wa mradi kuhitaji upatikanaji wa matokeo chanya kwa wakulima kiuzalishaji na masoko, mafunzo hayo yameandaliwa ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha elimu ya kilimo hicho inawafikia wakulima wengi kwa wakati kupitia wataalam hao katika shehia zao.

“Mafunzo haya tumeyaandaa kwa lengo moja tu kuhakikisha tunawaomgezea taaluma wataalam hawa ili wakatoe elimu ya vigezo bora vya kilimo kwa mjibu wa malengo ya mradi huu kutokana na kwamba wataalam hawa wanatoka katika kila shehia ambazo mradi unatekelezwa,” alisema.

Katika hatua nyingine alibainisha kwamba mafunzo hayo yamejikita zaidi katika utoaji wa taaluma ya kilimo chenye kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, vigezo bora vya kilimo, bustani ya jikoni pamoja na viwango endelevu vya hiari kwa wakulima.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Viungo, Mboga na Matunda unaotekelezwa Zanzibar na taaasisi za People’s Development Forum (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Meneja Mradi wa VIUNGO Kanda ya Pemba Sharif Maalim Hamad akifungua mafunzo ya wataalam wa Kilimo Pemba.
Afisa anayeshughulika na biashara na masoko, Omar Mtarika akitoa mafunzo kwa wataalam wa kilimo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464