WOMEN FOR CHANGE YATOA MSAADA WA VITI NA MEZA SALAWE SEC., DC MBONEKO APONGEZA

Mwenyekiti wa taasisi ya Women For Change, Getrude Munuo (kushoto) akimkabidhi viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Salawe, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kulia) leo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika shule hiyo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Na Damian Masyenene, SHINYANGA 
KATIKA kutoa mchango kwa jamii na kusaidia kutatua changamoto za upungufu wa miundombinu mbalimbali ya kielimu, Taasisi ya Women For Change (WFC) ya Mjini Shinyanga, imetoa msaada wa Viti 20 na Meza 20 katika shule ya Sekondari Salawe iliyopo katika kijiji cha Azimio Kata ya Salawe Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa. 

Msaada huo wenye thamani ya Sh Milioni 1, umekabidhiwa leo shuleni hapo na kikundi hicho mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba pamoja na wawakilishi mbalimbali wa chama (CCM) na Serikali. 

Akipokea Msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amekishukuru kikundi cha Women For Change (WFC) pamoja na wadau wengine waliojitokeza kuchangia elimu ya watoto kwa kushirikiana na Serikali, ambapo ameeleza kuwa mchango huo ni matokeo ya shule hiyo kufanya vizuri kwa kupambana na tatizo la mimba kwa wanafunzi kwani miaka kadhaa nyuma hali juu ya tatizo hilo ilikuwa mbaya. 

DC Mboneko amesema msaada huo unapaswa kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi katika shule hiyo, ambapo amewataka kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo urithi pekee usiopotea, huku akiwaagiza mkuu wa shule hiyo, Mtendaji wa Kata na fundi anayetengeneza vifaa hivyo kuhakikisha kwamba vinakamilika kwa wakati na kukabidhiwa vyote shuleni hapo Machi 22, mwaka huu (Jumatatu). 

"Tumekuja kuwatia moyos ili musome kwa bidii na kufikia ndoto zenu, naushukuru uongozi wa shule kwa namna unavyoendelea kusimamia wanafunzi.....lakini pia wazazi wawafuatilie watoto na watendaji wa Kata na vijiji pamoja na maafisa elimu wasimamie watoto wote wanaopaswa kuja shule wafike, hatutaki utoro," amesema. 

Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa taasisi ya Women For Change (WFC), Getrude Munuo amesema kuwa taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 inaundwa na wanawake 20 wajasiriamali na viongozi imelenga kuinuana kiuchumi, kusaidia watoto na wazee wanaoishi katika mazingira magumu, ambapo msaada walioutoa katika shule ya Sekondari Salawe ni Viti 20 na Meza 20 za kukalia wanafunzi vyenye thamani ya Sh Milioni 1, huku akiahidi kuendelea kutatua changamoto zingine za kielimu katika shule hiyo pale watakapofanikiwa tena. 

Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuendelea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani na kuelekea kwenye sherehe ya Wanawake wa Shinyanga kutoka kada mbalimbali iliyopewa jina la 'Shinyanga Women's Day Out' inayotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu (Jumamosi) katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sherehe ya 'Shinyanga Women's Day Out 2021' inayoandaliwa na taasisi hiyo ya Women For Change, Faustina Kivambe ametumia nafasi hiyo kuwaalika wanawake wote kwenye sherehe hiyo, kwani msaada walioutoa leo ni sehemu ya kuelekea kwenye sherehe hiyo na sehemu ya mapato ya tamasha hilo yanakwenda kuchangia na kutoa misaada katika jamii. 

Amesema sherehe hiyo itahusisha elimu ya afya na mahusiano, ujasiriamali na malezi, ambapo wazungumzaji mbalimbali wakiwemo Mchungaji Daniel Mgogo, Aunt Sadaka, Edna Shoo, Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama, Dk. Mfaume Kibwana na wengine wamealikwa. 

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Salawe, Faraja Mbilinyi amesema kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 746, mbali na changamoto ya upungufu wa baadhi ya miundombinu yakiwemo madawati, bado wanakabiliwa na ukosefu wa huduma ya maji katika jengo la hosteli (wasichana) lenye wanafunzi 35, kukosa mashine ya kuchapisha na kurudufu mitihani hali ambayo husababisha kutokuwa na mitihani ya mara kwa mara, pamoja na upungufu wa meza na viti vya kukalia wanafunzi. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba amesema msaada huo umewaongezea nguvu na utafanya kazi iliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya, huku akiwataka wanafunzi kujibu msaada huo kwa kufaulu vizuri na kuipa matokeo mazuri shule yao. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela amewaomba wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kuvitunza vyema vifaa walivyopewa kwa sababu wanaovileta wanatoa sehemu ya kipato chao kwa uchungu kwa ajili yao.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akisisitiza jambo katika hafla ya kukabidhiwa meza na viti kutoka taasisi ya Women For Change na wadau wengine kwa ajili ya shule ya Sekondari Salawe.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa meza na viti kutoka taasisi ya Women For Change na wadau wengine kwa ajili ya shule ya Sekondari Salawe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba akizungumza na kutoa shukrani kwa taasisi ya Women For Change kwa msaada wa viti 20 na meza 20 walizozitoa kwa shule ya sekondari Salawe
Mwenyekiti wa Taasisi ya Women For Change (WFC), Getrude Munuo (katikati) akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi msaada wa viti na meza.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Salawe, Faraja Mbilinyi akisoma risala mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (hayupo pichani) wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo
Mkuu wa Shule ya Sekondari Salawe, Faraja Mbilinyi (kushoto) akikabidhi risala kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela akizungumza wakati wa hafla hiyo
Diwani wa Kata ya Salawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Joseph Burugu akizungumza katika hafla hiyo
Mwenyekiti wa tamasha la SHINYANGA WOMEN'S DAY OUT linaloandaliwa na taasisi ya Women For Change, Faustina Kivambe aakizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi viti na meza
Mwenyekiti wa Taasisi ya Women For Change, Getrude Munuo (kushoto) akimpa maelezo juu ya msaada walioutoa wa viti na meza katika shule ya sekondari Salawe, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (aliyevaa kiremba chekundu) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Women For Change, Getrude Munuo (kulia kwa Mkuu wa wilaya) na viongozi wa chama (CCM), wanafunzi na wanachama wa taasisi ya Women For Change baada ya kukabidhiwa msaada wa viti na meza katika shule ya sekondari Salawe
Sehemu ya viti 20 na meza 20 zilizokabidhiwa na taasisi ya Women For Change kwa ajili ya wanafunzi katika shule ya Sekondari Salawe
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Salawe pamoja na wadau mbalimbali waliotoa msaada wa viti na meza shuleni hapo ikiwemo Taasisi ya Women For Change
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akiinama ili kuvalishwa skafu na kijana wa skauti katika shule ya sekondari Salawe 
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akivalishwa skafu na mmoja wa vijana wa skauti katika shule ya Sekondari Salawe
Wanachama wa Women For Change wakimkaribisha katika shule ya sekondari Salawe, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko kwa ajili ya kumkabidhi viti na meza
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akikaribishwa katika shule ya sekondari Salawe kwa burudani
Wanachama wa taasisi ya Women For Change wakiserebuka na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba (aliyevaa kofia) pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Salawe
Wanafunzi ambao ni wanachama wa klabu ya 'Pambana Fema Club' inayotoa elimu ya jinsia na kuepuka mimba kwa wanafunzi, wakiimba mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko


Mkurugenzi wa shule ya Little Tressure, Lucy Mwita ambaye pia ni Mwanachama wa taasisi ya Women For Change akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Salawe
Mkurugenzi wa Lulekia Company, Ansila Benedict ambaye ni mwanachama wa Women For Change akizungumza na wanafunzi katika hafla hiyo
Mwenyekiti wa sherehe ya Shinyanga Women's Day Out, Faustina Kivambe akizungumza katika hafla hiyo
Baadhi ya wanachama wa taasisi ya Women For Change wakizungumza na wanafunzi katika hafla hiyo
Wanachama wa Women For Change wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
Wanachama wa Women For Change wakiwa katika shule ya sekondari Salawe kwa ajili ya kukabidhi msaada wa viti na meza



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464