RAIS SAMIA ADOKEZA UTEUZI MWINGIZE BAADA YA PASAKA, AONYA CHOKOCHOKO ZA KAMPENI 2025 ......ATAKA MAPATO YAFIKE TRILIONI 2 KWA MWEZI

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Na Damian Masyenene
KATIKA kuhakikisha kuwa anapata wasaidizi wazuri, weledi, waadilifu, wachapa kazi na watakaosaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amedokeza kuwa kutakuwa na uteuzi mwingine baada ya sikukuu ya Pasaka.

Rais Samia ametoa dokezo hilo leo Aprili 1, 2021 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa kuwaapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri nane na naibu mawaziri nane walioteuliwa jana.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia alianza kwa salamu na kuwatania Makatibu wa Wizara kwa kuwataka wasiwe wanyonge kwani leo haikuwa siku ya kuwafanyia mabadiliko, lakini akasisitiza kuwa siku yao inakuja.

"Makatibu mpo....msiwe wanyonge, siyo leo lakini inakuja," amesema huku akitabasamu.

Hata hivyo, akihitimisha hotuba yake katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kuwa Jumanne baada ya Sikukuu ya Pasaka kuna uwezekano mkubwa wa kukutana tena Ikulu kuapisha viongozi wengine.

"Baada ya sikukuu ya pasaka tutakuja kuapishana hapa na wengine," amesisitiza.

Kauli hizo za Rais Samia zinakuja baada ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango kumuelekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga kushughulikia mivutano baina ya Makatibu wakuu na manaibu wao.

"Mawaziri na manaibu waziri kuvutana natumaini wamesikia na hili tutalifuatilia, chapeni kazi tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kuvutana.

"Mheshimiwa katibu mkuu kiongozi kuna mivutano baina ya makatibu wakuu na manaibu wao, wapo baadhi ya makatibu wakuu ambao manaibu wao wakifanya vizuri inakuwa shida, hasa wanapopaza sauti zao juu ya matumzi ya fedha inakuwa nongwa...waambie tunafuatilia na tutachukua hatua," ameagiza Dk. Mpango.

Vile Vile, Dk. Mpango amemuagiza Waziri wa Ferdha, Mwigulu Nchemba akisaidiana na naibu wake, handisi Hamad Masauni pamoja na timu nzima kutatua masuala ya kifedha ya Muungano, huku akimtaka Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu kukusanya vyema maduhuli na kusimamia matumizi ya fedha kwani mapato kutoka kwenye taasisi na mashirika ya Serikali ni kiduchu.


MAPATO TRILIONI 2
Katika kuongeza mapato ya Serikali, Rais Samia ameitaka Wizara ya fedha kutengeneza mazingira mazuri ya kukusanya kodi na kucha kutumia mabavu bila maarifa hali inayosababisha kuua bishara nyingi nchini, huku akiitaka wizara hiyo kuhakikisha inakusanya mapato yapatayo Sh Trilioni 2 kwa mwezi.

"Mwende mkatanue wigo wa kodi na kutenegeneza walipa kodi wengi zaidi, manake kwa sasa mnaua walipa kodi wengi zaidi, mnatumia nguvu zaidi kuliko akili na maarifa," amesisitiza.

Hata hivyo, Rais Samia amewapongeza viongozi hao kwa kuaminiwa kwa kurudi wote na mabadiliko kidogo katika kuliendesha jahazi ambalo linatakiwa likate mawimbi safari ifike salama.

Pia amempongeza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga kwa kuibua tatizo ndani ya utendaji wa wizara ambazo zimekuwa zikifanya kazi bila kuwa na muunganiko (Coordination), hivyo akamtaka kuhakikisha analimaliza tatizo hilo na serikali inafanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuwatumikia wnaanchi.

"Coordination katika serikali yetu ni ndogo sana, kila waziri anashika lake, huo ugonjwa uliouibua ndiyo wenyewe na wewe ndiye daktari wa kuutibu.

"Serikali hii ni moja, hamna haja ya kugombana wala kuvuatana mara huyu kanichukulia instrument, kaeni muone njia gani mtaweza kufanya kazi kwa pamoja. Sisi ni watumishi wa Watanzania na nitakuwa na kipimo cha mabega, nikiona mtu mabega yamepanda juu najua huyu siyo mtumishi," ameeleza. 

KAMPENI 2025
Rais Samia ameonya pia chochoko za baadhi ya wanasiasa na viongozi ambao wameanza maneno na kufanya kampeni za mapema kuelekea mwaka 2025.

"Nafahamu 2025 ipo karibu, inapofika kipindi cha mwisho cha awamu najua kunakuwa na hili na lile, nawaambieni acheni. hili na lile yatakuja baadae, wenye nia na 2025 acheni.

"Kuna wengine wamekosa hizi nafasi kwa sababu ya rekodi zao tu, rekodi zako zitakufuata, na mimi nitawaangalia," amebainisha.









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464