Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Na Damian Masyenene
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonyesha kukerwa na maneno yanayozushwa na baadhi ya watu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii juu ya sababu za kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli.
Rais Samia amesisitiza kuwa Hayati Magufuli alifariki kwa tatizo la Moyo lililokuwa likimsumbua kwa zaidi ya miaka 10.
Akilihutubia bunge la 12 leo Aprili 22, 2021 bungeni jijini Dodoma, Rais Samia amewataka wale wote wenye mashaka na kifo cha Hayati Magufuli na wana taarifa za msingi basi wafike kwenye vyombo husika watasikilizwa, lakini vinginevyo watasakwa na kuchukuliwa hatua.
Rais Samia amesisitiza kuwa wanaofanya uzushi huo wanafanya uchonganishi kwenye taifa na kutaka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
"Nimekuwa nikiona kwenye mitandao taarifa za uchonganishi, taarifa tuliyopewa na madaktari wetu kwa kifo cha mpendwa wetu ni matatizo ya moyo aliyoishi nayo kwa zaidi ya miaka 10.
"Kama wana taarifa za maana waje tuwasikilize, vyombo vya upelelezi na uchunguzi vipo waje tuwasikilize, tofauti na hapo wanaleta uchonganishi. Waache kuleta uchonganishi ndani ya nchi. Niwaambie kuwa tutawatafuta
"Kama wanajizatiti wanafanya hivyo wanadhani hatutowapata, basi warudi kwa mungu wajiulize wanavyofanya hivyo wangeambiwa wao hivyo wangekubali?," ameonya.
WALIOANZA 'KULEGEA'
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza kuwa baada ya kifo cha Hayati Dk. John Magufuli, baadhi ya watendaji wa Serikali, wawekezaji na nidhamu vimeanza kulegea kutokana na watu kuamini kuwa kuondoka kwa JPM mambo yatakwama.
Rais Samia amesema kuwa baadhi ya watendaji wameanza kulegea na kukosa ufanisi, wizi wa mali za umma umeshamiri, wawekezaji waliokuwa kwenye majadiliano na serikali wameanza kurudi nyuma, hivyo amebainisha kuwa MWENDO NI ULE ULE na mambo yatakwenda sawia kadri ya yalivyoahidiwa.
WENYE MASHAKA NA RAIS
Rais Samia pia amebainisha kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wake kutokana na jinsia yake na namna atakavyoyatimiza yale aliyoyasema.
Ambapo, amewatoa wasiwasi na kueleza kuwa anao uzoefu wa kutosha kwenye shughuli za serikali na chama chake (CCM) kwani Mwenyezi Mungu hakuumba ubongo hafifu kwa mwanamke na ubongo makini kwa mwanaume, wote wamezaliwa sawa.
"Nataka niwahakikishieni kuwa nimekuzwa kwenye jamii makini na nina uzoefu wa kutosha kwenye shughuli za serikali na chama changu cha siasa. Najiamini kuwa ninao uwezo wa kuliongoza taifa langu.
"Haya niliyoyasema hapa siendi kukaa na kuyatekeleza peke yangu, nitashirikiana na watanzania wote katika Nyanja tofauti. Tushirikiane katika kulijenga taifa letu," amesema.