RAIS SAMIA ATANGAZA MIKAKATI YA KULINUSURU ATCL, AELEZA MADENI YA KURITHI YALIVYOLIKWAMISHA

Ndege ya Shirika la ATCL

Na Damian Masyenene
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali itaendelea kulilea kimkakati Shirika la Ndege (ATCL) ili liweze kujiendesha kwa faida, kukua na kuweka mahesabu yake sawa.

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 22, 2021 bungeni jijini Dodoma majira ya saa 10 jioni wakati akilihutubia bunge la 12, ambapo ameweka wazi kuwa mbali na kulisimamia shirika hilo, Serikali pia katika kuboresha usafiri wa anga nchini itaendelea na utanuzi wa viwanja vya mikoa pamoja na ujenzi wa uwanja wa kimataifa Msalato jijini Dodoma.

Kauli hiyo ya Rais inakuja baada ya wiki kadhaa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kubainisha kuwa shirika la ATCL limekuwa likijiendesha kwa hasara kwa kutengeneza hasara ya Shilingi bilioni 60 kwa mwaka.

Akieleza namna usimamiaji na kulilea shirika la ndege la Tanzania (ATCL) utakavyosaidia kukuza uchumi nchini, Rais Samia amesema kuwa Serikali itaona uwezekano wa kutoa unafuu wa madeni na tozo za kodi kwa ATCL.

Pia ameeleza kuwa kwa sasa ATCL linasomeka kama halina thamani kwa sababu ya kurithi madeni, hivyo akaahidi kuwa Serikali itakwenda kulitua mzigo wa madeni.  

"Hatukubali kuona shirika linaendelea kupata hasara baada ya uwezekaji mkubwa tulioufanya, tutaendelea kuliwezesha upande wa rasilimali watu wanaoweza kuliendesha. Tutakwenda kulifanyia uchambuzi wa kina ili tupate watu watakaoweza kuliendesha kwa faida," amebainisha.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464