RIPOTI: TAKUKURU YABAINI MADUDU UCHINJAJI MIFUGO KAHAMA....NYAMA ZINAZOZIKWA HUFUKULIWA NA KUUZWA, MCHINJA NGURUWE WALIOKUFA ANASWA



Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa (Picha na Maktaba)

Na Damian Masyenene, Shinyanga
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imebaini uchinjaji holela wa mifugo katika manispaa ya Kahama na kumshauri Mkurugenzi wa manispaa hiyo kuzifunga machinjio zote zinazoendeshwa kienyeji.

Katika ripoti yake iliyotolewa jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa, taasisi hiyo imebaini kuwa nyama za nguruwe zinachinjwa bila ya kukaguliwa na Maafisa Mifugo, huku nyama zinazozikwa kwa kutozingatia taratibu za uchinjwaji kufukuliwa na kuuzwa.

Akitoa ripoti hiyo, Mussa amesema kuwa TAKUKURU wilaya ya Kahama ilipokea taarifa juu ya uwepo wa tuhuma na malalamiko ya uchinjaji wa nyama katika Manispaa ya Kahama ambao haufuati taratibu na Kanuni za uchinjaji na kupelekea nyama kuingizwa katika maeneo ya kuuzia kitendo ambacho ni hatari kwa afya za watumiaji wa nyama hizo. Aidha taarifa ilieleza kuwa mifugo hasa nguruwe mara nyingine huchinjwa ikiwa tayari imeshakufa ama kutokaguliwa na Maafisa Mifugo.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo, Takukuru Kahama kwa mujibu wa jukumu la uzuiaji rushwa kama lilivyoainishwa katika Kif cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007, ilianzisha uchunguzi na ufuatiliaji na kuweza kubaini nyama iliyohifadhiwa katika jokofu la Ofisi ya Mifugo Manispaa ya Kahama ambayo ilithibitika mnyama huyo kuchinjwa akiwa tayari amekufa na ilikamatwa ikiwa tayari kwa muuzaji wa Kitimoto aliyepo katika eneo la Mbulu Manispaa ya Kahama.

“Aidha uchunguzi uliweza pia kubaini eneo la machinjio ya nyama za nguruwe lilipo Nyakato Kahama ambapo tuliweza kujiridhisha kwa kuona eneo ambalo lilifukiwa na kuzikwa nyama ya nguruwe iliyochinjwa kinyume na taratibu usiku wa tarehe 10.04.2021 ikiwa imefukuliwa na kupelekwa kusikojulikana,” ameeleza.

Mussa ameeleza kuwa, baada ya kufanya mahojiano na watu mbalimbali wakiwemo Maafisa Mifugo wa Kata na mashahidi walioshuhudia uwepo wa matukio hayo, Takukuru ilibaini mambo mbalimbali yanayofanyika kinyume na taratibu na sheria zinazosimamia mifugo, ikiwemo uwepo wa machinjio nyingi za kienyeji katika manispaa hiyo, hivyo kuwa ngumu kwa Maafisa Mifugo kujua na kufanya ukaguzi.

“Aidha tumebaini kuwa uwepo wa tatizo hili pia husababisha Manispaa kupoteza mapato yanayotokana na uchinjwaji wa mifugo hasa nguruwe, Kutozingatiwa kwa taratibu za uchinjaji wa nyama unaoelekeza wanyama kukaguliwa kabla na baada ya kuchinjwa, hivyo kupelekea nyama kuingizwa sokoni zikiwa na kasoro ambayo ni hatari kwa afya za watumiaji wa nyama hizo.

“Imebainika pia kwamba hata Maafisa Mifugo wanapotekeleza majukumu yao ya kuzika nyama zilizobainika kuwa na kasoro za kiafya, nyama hizo zinazozikwa hufukuliwa na kwenda kuuzwa katika vibanda vya kuuzia nyama, hasa katika Maeneo ya pombe za kienyeji, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya watumiaji nyama hizo,” amebainisha.

Baada ya uchunguzi na ufuatiliaji wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama kubaini hayo, kwa kushirikiana na Maafisa Mifugo taasisi hiyo iliweza kumkamata mfanyabiashara ya uchinjaji wa nyama za nguruwe, Majaliwa Kayaya Isanduko mkazi wa Nyakato ambaye alibainika kuchinja na kuuza nyama zisizofuata taratibu za uchinjwaji na pia kuchinja na kuuza wanyama (nguruwe) waliokufa.

Mshitakiwa huyo alitozwa faini kwa makosa mawili na kutakiwa kulipa faini ya Sh. 200,000 kwa kila kosa, Mshitakiwa huyo ambaye alilala ndani siku moja (Aprili 13, 2021) alilipa faini Sh. 400,000 baada ya kuandikiwa hati ya makosa na Mwanasheria wa Manispaa na kupewa namba za malipo (Control namba) na kulipia kiasi hicho Benki na kupewa Stakabadhi ya Manispaa.

Aidha, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama ameshauri Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kufunga machinjio hiyo pamoja na machinjio zote za kienyeji na kuweka utaratibu maalum wa uchinjaji wa nguruwe utakaowezesha kufuatwa kwa taratibu za uchinjaji na pia kudhibiti upotevu wa mapato yanayotokana na uchinjaji holela wa mifugo.

“Pia Takukuru Wilaya ya Kahama imeomba kufanya mkutano na maafisa mifugo wote wa Manispaa ya Kahama na wadau wengine wa mifugo ili kuweza kutoa elimu pamoja na kueleza yaliyojiri katika ufuatiliaji huu,” ameeleza Mussa.
Eneo la machinjio ya kienyeji lililopo Nyakato Manispaa ya Kahama ambapo kumebainika uchinjaji wa nyama za nguruwe ambao haufuati taratibu na kanuni za uchinjaji a hivyo kuhatarisha afya za watumiaji wa nyama hizo (Picha na Takukuru)


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464