Wachezaji wa Simba SC
Na Damian Masyenene
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeziruhusu klabu za Smba SC na Namungo FC za Tanzania kuingiza mashabiki kwenye michezo yao ya wikendi hii katika uwanja wao wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa CAF imeiruhusu timu ya Simba kuingiza washabiki 10,000 katika mechi yao dhidi ya AS Vita kutokana na maombi ya TFF.
Mechi hiyo ya tano ya michuno ya ligi ya mabingwa Afrika (CCL) itapigwa Jumamosi Aprili 3, 2021 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Wekundu wa Msimbazi ambao ni vinara wa kundi A wanahitaji alama moja tu ama ushindi ili wafuzu kwenda hatua ya robo fainali.
Awali, CAF iliizuia Simba kuingiza mashabiki katika mchezo wao wa nne dhidi ya Al Merreikh ya Sudan uliochezwa Machi 16, mwaka huu katika uwanja huo, huku wakiruhusiwa watu 200 pekee wakiwemo waandishi wa habari.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeiruhusu timu ya Namungo FC kuingiza washabiki 10,000 katika mechi yao dhidi ya Nkana FC kutokana na maombi ya TFF.
Namungo ilizuiwa kuingiza mashabiki katika mchezo wao uliopita dhidi ya Pyramid FC ya Misri ambao walipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya matajiri hao wa Misri.
Kikosi cha Namungo FC