WADAU WARIDHIKA NA UANZISHWAJI DAWATI LA JINSIA VYUONI, WASEMA NI MWAROBAINI WA UKATILI

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Mwangwa akifungua kikao cha wadau wa masuala ya jinsia chenye lengo la kupitia rasimu ya mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati ya jinsia kwenye taasisi za elimu ya kati na elimu ya juu mkoani Dar es salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa, Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa dawati la jinsia katika Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya Juu utasaidia kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia zinazowakabili wanafunzi na wakufunzi vyuoni.

Hayo yamebainika mkoani Dar es Salaam wakati wa kikao kati ya Serikali na wadau kupitia Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa dawati la jinsia katika Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya Juu .

Baadhi ya Wadau wa masuala ya jinsia wakizungumza wakati wa kupitia rasimu ya Mwongozo huo ulioandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamesema changamoto kubwa iliyokuwepo ni kukosekana kwa mfumo mmoja wa kushughulikia matatizo ya ukatili wa kijinsia katika taasisi za elimu.

Mmoja wa wadau hao Dkt. Rose Shayo, mkufunzi mstaafu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema mwongozo huo ukikamilika na kuanza kutekelezwa utakuwa ni moja ya silaha muhimu katika kupambana na vitendo vya ukatili vyuoni.

"Serikali imefanya vyema kutushirikisha wadau kuandaa mwongozo huu ambao ni imani yangu utaandaa mazingira mazuri kwa vyuo vyetu vya elimu ya juu na kati kuwa na utaratibu mmoja wa kushughulikia masuala ya kijinsia tofauti na hapo awali, kila Chuo kilikuwa na utaratibu wake" alisema Dkt Rose.

Nao baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Irene Paul na Joachim Peter wemesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa mifumo ya kushughulikia vitendo vya ukatili, bado vitendo hivyo vinaendelea kushamiri ila wanaamini mwongozo utakapokamilika, utawasaidia kuwa na nguvu zaidi ya kupambana na vitendo hiyo.

"Changamoto za ukatili wa kijinsia zipo na zinachangia athari mbalimbali kwa wanafunzi ikiwemo kukatisha masomo yao. Kuanzishwa kwa madawati haya kutasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kuwalinda watoa taarifa za ukatili vyuoni, kwani kwa sasa wanafunzi wengi wamekuwa wakihofia usalama wao hivyo kushindwa kutoa taarifa" alisema Irene.

Amesisitiza kuwa, hatua zilizochukuliwa zitawasaidia kupunguza matatizo kwa wote wanafunzi na wakufunzi kwani watajua njia sahihi na salama za kutoa taarifa mahali husika.

Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Grace Mwangwa amewasisitiza wadau kuzingatia Mwongozo huo pale utakapopitishwa kwani utawasaidia vijana pamoja na wakufunzi wa Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya juu kupambana na vitendo vya Ukatili.

Mwangwa ameongeza kuwa mwongozo huo unalenga kuhakikisha masuala yote ya kijinsia yanaainishwa na kujumuishwa katika mipango kazi na Bajeti ya taasisi hizo ili kuhakikisha changamoto za ukatili wa kijinsia zinatatuliwa.

" Serikali inatarajia kuwa, mwongozo huu utatoa kipaumbele katika masuala ya jinsia ikiwa ni pamoja na kuwa na takwimu mbalimbali zilizoainishwa kijinsia na mipango mahususi ya kuondoa tofauti za kijinsia." alisema Mwangwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Women in Law and Development in Africa (WiLDAF) Anna Kulayo amesema maandalizi ya Mwongozo huo yamefanyika kwa muda mrefu hivyo ni wakati wa kuukamilisha ili ufanyiwe kazi kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya Juu.

Kikao cha kupitia rasimu ya mwongozo wa uanzishaji wa dawati la jinsia katika Elimu ya Kati na juu kimefanyika ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya mwongozo huo unaoandaliwa na Wizara ya Afya, kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Wadau.
Mkurugenzi wa Shirika la Women in Law and Development in Africa (WiLDAF), Anna Kulayo akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao cha wadau wa masuala ya jinsia chenye lengo la kupitia rasimu ya mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati ya jinsia kwenye taasisi za elimu ya kati na elimu ya juu Mkoani Dar es salaam.
Wadau wa masuala ya jinsia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa kikao cha kupitia rasimu ya mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati ya jinsia kwenye taasisi za elimu ya kati na elimu ya juu, kilichofanyika Mkoani Dar es salaam.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali WAMJW

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464