WAZIRI AWESO ATEMBELEA MRADI WA MAJI MWAKITOLYO, WANANCHI 14,601 KUNUFAIKA


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa nne kutoka Kushoto) akiwa kwenye ziara ya kukagua mradi wa Maji Mwakitolyo wilayani Shinyanga, watatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Na Marco Maduhu, Shinyanga
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametembelea ujenzi wa mradi wa maji Mwakitolyo uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, na kutoa siku 10 mradi huo uwe umeshakamilika, na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Aweso amefanya ziara hiyo leo , akiambatana na Naibu Katibu Mkuu wizara ya maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba.

Amesema kati ya miradi ya maji 177 ambayo ni kero hapa nchini, mmoja wapo ni mradi huo wa Mwakitolyo, na kuagiza hadi ifikapo Mei 5 mwaka huu ndani ya siku 10 zijazo, uwe tayari umeshakamilika.

"Mradi huu wa maji Mwakitolyo nina historia nao, ni kati ya miradi ya maji kichefuchefu hapa chini, hivyo naagiza hadi ifikapo Mei 5 uwe tayari umeshakamilika, sitaki kuzinguliwa na Rais, nadhani siku ile Bungeni mlisikia Rais alivyosema, na kiu yake kubwa ni wananchi wapate maji," anasema Aweso.

"Pia ma-Meneja Wakala wa maji vijijini Ruwasa, naagiza mfanye kazi kwa kishirikiana na wakuu wa mikoa ,wilaya, na Madiwani, ili kuhakikisha mnafanya kazi zenu kwa ufanisi na kuhudumia wananchi maji safi na salama," ameongeza.

katika hatua nyingine Aweso amesema, Wakandarasi wasio na uwezo hawana nafasi kupewa kazi za ujenzi wa miradi ya maji kwenye wizara hiyo, pamoja na Wahandisi wa maji ambao ni wazembe watawajibishwa, huku akiahidi kutoa Sh. milioni 100 kwa ajili ya kujenga Tenki lingine la maji lenye lita Laki Tano kwenye mradi huo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha kujenga mradi huo wa maji Mwakitolyo, na kuahidi kuusimamia ili ukamilika kwa siku hizo 10 ambazo zimetolewa na kutoa huduma ya maji safi na salma kwa wananchi.

Aidha ameongeza kuwa, wao kama Serikali mkoani Shinyanga wapo vizuri kwenye usimamizi wa ujenzi wa miradi ya maji, ambapo wiki ya madhimisho ya maji walizundua miradi mingi ya maji ukiwamo wa Ihapa, Salawe, Mwamashele na Mwawaza huku miradi mingine wataendelea kuizindua ukiwamo wa Masengwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Kahama na Shinyanga (KASHWASA) Mhandisi Joshua Mgeyekwa, ambao ndiyo watekelezaji wa mradi huo wa maji Mwakitolyo kwa kishirikiana na (RUWASA), alimhakikishia Waziri Aweso kuwa mradi huo utakamilika ndani ya siku hizo 10, ambapo ujenzi wake ulianza mwaka Jana na utagharimu Sh. bilioni 2.3.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji safi na salama Mwakitolyo wilayani Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwenye ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji Mwakitolyo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mbonekom akielezea mradi huo wa maji namna utakavyosaidia wananchi wa Mwakitolyo.
Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi Kahama na Shinyanga (KASHWASA), Mhandisi Joshua Mgeyekwa wa pili kushoto, akielezea namna watakavyo kamilisha mradi huo wa maji Mwakitolyo.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiendelea kukagua ujenzi wa mradi wa maji Mwakitolyo.
Ukaguzi ukiendelea.
Mtambo ukiendelea na shughuli ya kufukia mabomba ya maji.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso, wa Nne kutoka Kushoto akiwa kwenye ziara ya kukagua mradi wa Maji Mwakitolyo wilayani Shinyanga, watatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464