Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana balehe jijini Dodoma leo tarehe 17/04/2021.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe ili kupata Taifa lenye nguvu kazi endelevu.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akizindua Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe.
Ajenda hiyo ya kitaifa nimejikita katika nguzo sita ambazo ni kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kudhibiti mimba za utotoni, kuboresha lishe kwa vijana, kuzuia ukatili wa kimwili na kisaikolojia, kuhakikisha watoto wa kike na kiume wanakwenda shule na kumaliza masomo yao na kuwawezesha vijana balehe wanapata ujuzi na maarifa ya kuchangamkia fursa za kiuchumi.
Akizungumza kuhusu lishe bora amesema agenda itawasaidia vijana hasa kundi la vijana katika kuimarisha nguvu na akili kwa kundi hili ambalo linatarajiwa kuwa nguzo ya Taifa.
"Suala la lishe liwe ni ajenda kwenye shule zetu, kila shule iwe na bustani ya mboga mboga, hii itasaidia vijana kufahamu umuhimu wa lishe salama na kuweza kujitegemea na kuelimisha jamii" alisema Majaliwa.
Aidha, amezitaka Wizara zinazosimamia Ajenda hiyo kusimamia kikamilifu utekelezaji wake ili kuhakikisha lengo linafikiwa kwa ufanisi mkubwa na kuwasaidia vijana.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema masuala ya lishe bado hayapewi kipaumbele kwani asilimia kubwa ya wanawake wenye umri wa kuzalisha wanakabiliwa na tatizo la lishe duni.
Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana balehe inatekelezwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, kazi, Ajira na watu wenye ulemavu na Wizara ya Elimu.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa ajenda hii itatekelezwa katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara na baadaye kuendelezwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Lengo mahsusi la ajenda hii ni kuwawezesha kundi la vijana kati ya miaka 10 na 19 kuimarisha Afya zao ili kuwa wazalishaji bora na nguvukazi ya Taifa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo ya shughuli zinazofanywa na Taasisi ya "Msichana Initiative" kabla hajazindua Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana balehe jijini Dodoma leo tarehe 17/04/2021.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana balehe jijini Dodoma leo tarehe 17/04/2021.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiangalia KItabu cha Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa vijana balehe jijini Dodoma leo tarehe 17/04/2021.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana balehe jijini Dodoma leo tarehe 17/04/2021.
Washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Ajenda ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo yaa Vijana balehe wakifuatilia matukio mbalimbali leo tarehe 17/04/2021.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW