Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Bi Zainab Telack akisisitiza jambo wakati wa Hafla fupi ya kuwapongeza na kutambua mchango wa viongozi wanawake waliofanya vizuri akiwemo Mkuu huyo wa Mkoa na Kamanda wa Jeshi la Polisi ACP Debora Magiligimba waliohinda tuzo hivi Karibuni
Na Josephine Charles-SHINYANGA.
Katika kutambua nafasi za viongozi wanawake Mkoani Shinyanga ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, asasi za kiraia pamoja na Mashirika yanayotekeleza Miradi mbalimbali ya mapambano hayo, zimeamua kuwapongeza Mkuu wa Mkoa huo Bi Zainab Telack na kamanda wa Jeshi la Polisi baada ya kuchukua Tuzo kwa nyakati tofauti hivi karibuni huku wakizitumia tuzo hizo kutafakari kwa pamoja jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga.
Mratibu wa Mfuko wa wanawake Tanzania Mkoa wa Shinyanga Bi Glory Mbia akizungumza kwa niaba ya asasi, amesema lengo la hafla hiyo ni kuwapongeza Viongozi wakuu Mkoani hapa waliopokea Tuzo za heshima ikiwa ni kutambua mchango wao katika masuala mbalimbali sanjali na nafasi za viongozi wanawake katika mkoa wa Shinyanga kwa ngazi zote hasa katika kupinga vitendo vya Ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Bi Glory amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Zainab Telack amekuwa mfano na chachu kwa viongozi wengine wanawake baada ya kutwaa tuzo wakati wa kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili ambapo UNFPA kwa kushirikiana na Wadau wake iliandaa tuzo kwa machampioni 16 wa kupinga ukatili.
Aidha Bi Glory amebainisha kuwa tuzo ya pili ni ile iliyokwenda kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP.Debora Magiligimba baada ya kushinda tuzo katika kategori ya Mwanamke kinara katika Taasisi za umma kanda ya ziwa na kuibuka Mshindi ambapo ni mwanamke ambaye anaongoza taasisi kubwa yenye kuhakikisha ulinzi na usalama wa watanzania unaimarika.
Awali akifungua hafla hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mlezi wa Asasi za Kiraia Mkoani hapa Bw. Thedson Ngwale amesema Shinyanga ina kila sababu ya kujivunia viongozi wanawake kwa sababu hali imekuwa tofauti na miaka ya nyuma, kutokana na kukithiri kwa matukio mengi ya unyanyasaji na ukatili,lakini uwepo wa viongozi hao umesaidia kwa kiwango kikubwa hali ambayo inatia matuamaini.
hata hivyo Ngwale amezipongeza asasi za kiraia zote zilizoamua kuungana pamoja kuandaa hafla hiyo ya kutambua na kuwapongeza Viongozi wanawake Shinyanga kwani inaleta hamasa zaidi kufanya kazi na hasa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutaraji kuona mabadiliko makubwa zaidi miaka mitano mbele endapo Viongozi hawa wataendelea kuwepo.
Mussa Ngangala ni Mkurugenzi wa Shirika la TVMC Mkoani Shinyanga ameiomba Serikali ya mkoa huu kutenga dawati maalumu kwa ajili ya kusikiliza na kupokea kero za wadau pamoja na asasi za kiraia pale wanapokutana na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mussa ameongeza kwa kusema kuwa wadau wote wa Masuala ya Ukatili wanaipongeza ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wanaoutoa hususani muda wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya kuhakikisha ukatili unatokomezwa.
Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Miradi Kutoka PACESHI John Shija ameomba Maboresho yafanyike katika uendeshaji wa Kesi za ukatili wa Kijinsia kwa Jeshi la Polisi na Mahakama ili kudhibiti ushahidi usipotee na kupelekea kesi kufutwa, kwani kufanya hivyo jamii itapata hofu na kuacha kutenda vitendo vya ukatili wa kijinsia endapo wataona na kusikia hukumu inatolewa dhidi ya watenda makosa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Investing in Children and their Societies (ICS) Bw. Kudely Sokoine amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack kuwakutanisha na wadau wanaoshughulikia masuala ya Afya pamoja na Wadau wanaoshughulikia masuala ya Ukatili wa Kijinsia kwa kuwa yana Uhuasiano wa karibu katika kupunguza ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwa na lugha moja wakati wa utekelezaji wake.
Jonathan Manyama Mkurugenzi wa Asasi ya thubutu Africa Initiatives amesema asasi za kiraia kuna wakati wananyong’onyezwa na baadhi ya ofisi za Serikali pale wanaombwa fedha kwa ajili ya kuchangia shughuli za kiserikali na kushindwa kuchangia kulingana na hali iliyopo hushindwa kutambulika,hivyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kama Mama kuwa akiona watoto wake hawana pesa muda huo awaelewe asiwatenge.
Sabrina Majikata yeye ni Meneja Miradi kutoka ICS amesema hivi karibuni Mkoa umezindua Mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini kigumu walichonacho katika asasi hizo ni kutafuta fedha ya kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili lakini changamoto wanayaokumbana nayo ni upatikanaji wa Takwimu sahihi.
Sabrina ameomba kupatikana muafaka wa Takwimu Sahihi na zinaznoendana na wakati zinapohitajika ili kuondoa ile hali ya kila Taasisi kuwa na Takwimu zake Mfano Polisi kuwa na Takwimu zake,Ofisi ya Ustawi wa Jamii kuwa na Takwimu zake.
ACP Debora Magiligimba akiuzngumza katika hafla hiyo amezipongeza asasi za kiraia mkoani Shinyanga kwa kazi nzuri wanayofanya huku akibainisha kuwa ataendelea kushirikiana nao katika mapambano ya ukatili dhidi ya Wanawake na watoto ili jamii ya mkoa wa Shinyanga iweze kuishi kwa amani.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Zainab Telack amezishukuru asasi hizo kwa Pongezi nyingi baada ya kuandaa hafla ya kuwapongeza wanawake Viongozi Mkoa wa Shinyanga kwa kazi wanazofanya ambapo amehaidi kuedelea kushirikiana na kutatua kero zote zinazowakumba wanachi .
amesema Tuzo aliyoipokea siyo yake tu bali niya Shinyanga nzima kwa kuwa hawezi kufanya kazi peke yake bila wadau wa maendeleo.
Kuhusu Changamoto na maombi yaliyosemwa na wadau wote wa Asasi za Kiraia amesema anaenda kuyafanyia kazi maombi yote yaliyotolewa na wadau hao wa kupinga ukatili wa kijinsia.
aidha,Viongozi wengine wanawake waliotambuliwa katika hafla hiyo ,Mkuu wa Magereza Mkoa wa Shinyanga Elizabeth Mbezi,Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko,Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kanda ya Shinyanga Mhe. Mary Mrio,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba,Hakimu wa Wilaya Mhe. Ushindi Swalo na Wabunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga.