BAJETI WIZARA YA AFYA SH. TRILIONI 1, WAZIRI DK. GWAJIMA ATAJA VIPAUMBELE


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeliomba Bunge kuidhinishia Sh1.07 trilioni katika mwaka wa fedha 2021/22.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 11, 2021 na waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2021/22.

Ametaja baadhi ya maeneo yaliyotengewa fedha ni ununuzi na usambazaji wa chanjo Sh63.2bilioni na ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi Sh263.8 bilioni.

Mengine ni Sh45.8 bilioni ni kwa ajili ya miradi misonge ambayo ni ukimwi, malaria na kifua kikuu na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma katika hospitali ya Taifa, hospitali maalum, hospitali za rufaa za kanda na hospitali za rufaa za mikoa, Sh105.9 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa miundombinu katika hospitali hizo.

Maeneo nyingine ni kuendelea kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali ya Taifa, hospitali maalum na hospitali za rufaa za kanda, Sh6.8 bilioni kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba.

Dk Gwajima ametaja eneo jingine ni uboreshaji miundombinu ya vyuo vya afya na kugharamia mafunzo na maendeleo ya wataalam katika sekta ya afya, Sh11.1 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kugharamia mitihani, chakula na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vya afya.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464