Na Damian Masyenene
TIMU ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CCL).
Katika mtanange huo uliopigwa leo Mei 22, 2021 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dare es Salaam, Mabao ya Simba SC yalipachikwa nyavuni na Nahodha John Bocco aliyefunga mawili katika dakika ya 24 na 56 pamoja na Clatous Chama aliyefunga mnamo dakika ya 83.
Hata hivyo, ushindi huo hauipeleki kokote Simba SC kwani katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Kaizer Chiefs waliibuka na ushindi wa mabao 4-0. hivyo matokeo ya mwisho yanasomeka 3-4 na kuifanya Simba SC kushindwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Katika mchezo huo Simba SC walihitaji ushindi wa mabao 5-0 ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele, ama 4-0 na kusubiria mapigo ya penalti.
Sasa Simba SC inarejea kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kutetea ubingwa wake pamoja na ile ya Shirikisho (FA) ambapo Jumatano Mei 26 watashuka dimbani kuwakaribisha Dodoma Jiji FC katika hatua ya robo fainali ya michuano ya FA kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Picha zote na Simba SC Tanzania