SHINYANGA DC YAANZISHA MCHAKATO UTUNGAJI SHERIA NDOGO NGAZI YA VIJIJI MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale akizungumza kwa niba ya Katibu tawala wa mkoa huo, Albert Msovela katika kikao cha kuhitimisha utekelezaji wa mradi wa afua za Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, leo katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
KATIKA kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani hapa yanafanikiwa na kutokomeza kabisa vitendo hivyo, halmashauri hiyo imeanza mchakato wa kutunga sheria ndogo ngazi ya vijiji na kata kusaidia kukomesha ukatili huo.

Hayo yameelezwa leo Mei 18, 2021 na Mratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Aisha Omari ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri hiyo, wakati wa wa kikao cha kuhitimisha mradi wa utekelezaji wa afua za (MTAKUWWA) kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, mradi ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT)- Trust.

Akiwasilisha namna ambavyo halmashauri hiyo ilivyotekeleza mradi wa kujenga uwezo kuhusu afua za mpango huo, Aisha amesema kuwa tayari zoezi la kutunga sheria hizo limekwishaanza katika vijiji vyote 126 na kata 26 za halmashauri hiyo na sasa sheria hizo ziko idara ya sheria ya halmashauri kwa ajili ya hatua za mwisho za kufanyiwa tathmini kabla ya kujadiliwa na baraza la madiwani.

Amesema katika mradi huo uliogharimu Sh Milioni 25 na kuchukua miezi miwili (Januari-Machi) ulilenga kutekeleza afua hizo kwa kuunda kamati za MTAKUWWA na kuzijengea uwezo kamati hizo katika kata 13.

Kaimu Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kitengo cha Sheria, Frank Singo akitoa maelezo namna wanavyofanikisha mchakato wa uundaji sheria za vijiji kukomesha ukatili, amesema kwa sasa wanamakamilisha utungaji huo ili kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi ambayo itazipeleka kwenye baraza la madiwani ili kujadiliwa na kupitishwa.

Hata hivyo, baadhi ya wadau na mashirika mbalimbali yanatekeleza mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika halmashauri hiyo, wakichangia mjadala huo wameipongeza halmashauri hiyo na kushauri iwepo nafasi ya wadau kutoa maoni kwenye sheria hizo na kupendewkeza mambo ya msingi yatakayosaidia kufanikisha vita hiyo.

Ambapo, Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) Mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia amesema kuwa ni vyema wadau hao wangepewa nafasi ya kutoa maoni kwenye utungaji wa sheria hizo ngazi ya awali kuliko kusubiri kwenye hatua ya mwisho, ambapo Kaimu Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Frank Singo alipokea ushauri huo na kuahidi kuufikisha ofisi ya mkurugenzi kwa majadiliano zaidi.

Katika hatua nyingine, Wadau hao wameishauri halmashauri hiyo kukaa kwa pamoja na idara zake ili kuandaa takwimu za pamoja juu ya vitendo mbalimbali vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, takwimu ambazo zitawawezesha wadau kujipima kwa hatua na mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo.

”Halmashauri muandae kikao cha kitaalam kitakachowahusisha wadau wa mashirika na serikali kuchakata data za Julai 2020 hadi Juni 2021 zinazohusihana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na Watoto kitakachosaidia kuwa na kauli moja na kusaidia utekelezaji,” ameshauri Glory Mbia.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la TVMC, Mussa Ngangala ameshauri kuwa ni vyema kukawa na kituo cha pamoja cha mawasiliano cha utoaji takwimu za matukio hayo, kwani kwa sasa hakuna jitihada za makusudi za upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazowasaidia wadau mbalimbali katika utekelezaji wa mradi wa afua za MTAKUWWA katika halmashauri hiyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amebainisha kuwa katika takwimu mbalimbali zinazotolewa za vitendo vya ukatili kwa wanawake na wa Watoto, zinazowahusu Watoto wanaoolewa ama kupewa mimba ambao siyo wanafunzi zimekuwa hazijumuishwi wala kushughulikiwa.

“Inavyoonekana ni kwamba maeneo ya vijijini Watoto walio chini ya miaka 18 wanaopata mimba hawaripotiwi kokote kwa sababu tu siyo wanafunzi, hili ni tatizo lingine linaloonekana kuhalalishwa. lazima kuwe na mawasiliano ya pamoja kwa sababu upande wa afya wanazo rekodi za Watoto chini ya miaka 18 walioanza kliniki kutokana na ujauzito lakini huku kwenye takwimu za ukatili haziji,” amesema.

Akijibu hoja hizo, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Shinyanga, Deus Mhoja amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kuahidi kushughulikia mapendekezo ya wadau hao, ambapo amesema kutokana na changamoto hiyo wameazimia kuwa na vikao vya kila robo mwaka kujadili utekelezaji na mwisho wa robo inayoisha Juni mwaka huu watafanya uchakataji wa takwimu kiweledi.

“Suala la takwimu limekuwa likitusumbua, ziko hovyo hazijakaa katika mtiririko unaoeleweka, tunaahidi kubadilika ili kuwa na takwimu halisi, tumeamua kulivalia njuga ili likae vizuri na tuwe na wasaa mzuri wa kufanya utekelezaji wa afua za MTAKUWWA kwa uhakika,” amebainisha.

Akitoa maelekezo kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga kwa watendaji mbalimbali wa serikali, Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa huo, Tedson Ngwale amesema kuwa kuna baadhi ya watendaji hao wanakwamisha maagizo mbalimbali ya viongozi wa mkoa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, huku akielekeza kamati za MTAKUWWA kuongezewa uelewa na kufanyiwa ufuatiliaji na kukumbushana kila siku kwani bado kuna uelewa mdogo wa majukumu yao.

“Kwa sisi watendaji na yale ambayo tunayoyasikia kule yanatosha, nitatamani nione matokeo kwenye hizo kata 13 mradi unakotelekezwa na isitokee mtendaji akatuangusha katika hii safari. Maeneo yaliyoainishwa kama vichocheo vya ukatili mfano machungani, minadani, yafanyiwe kazi, Pia, tatizo la mwamko mdogo wa wananchi kwenda kutoa taarifa, tufuatilie tujue kuna nini, jeshi la polisi pia litusaidie na watendaji wetu ngazi ya vijiji na kata,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Ngwale ametahadharisha matumizi ya jeshi la Sungusungu katika vita hiyo na kushauri kuwa endapo watatumika basi wapewe elimu kwanza juu ya malengo ya mradi wawe na ufahamu na kupewa malengo na ukomo wake ili kutathminiwa kwa sababu wamekuwa wakishiriki kwa namna fulani kusaidia washukiwa kutoroka.

“Baadhi ya watendaji na idara ya elimu wanashiriki kwa kuwaondoa shuleni/kuwafuta wanafunzi watoro shuleni na kuwafanya wazazi watumie mwanya huo kuwaozesha. Na watendaji wa kata na vijiji wanaoridhika na sababu za kuambiwa eti utoro bila kufanya ufuatiliaji waache, kila mmoja ajitafakari kwenye nafasi aliyopo na tubane mianya yote ambayo inatoa nafasi kwa Watoto kufanyiwa ukatili kwa kuozeshwa na kupewa mimba,” ameeleza.

Katika kikao hicho, taasisi zilizokuwa zinatekeleza miradi ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye halmashauri hiyo chini ya Women Fund Tanzania (WFT) ambazo ni Young Women Leadership (YWL), Thubutu Africa Iniative (TAI), Rafiki- SDO na Klabu ya Waandishi wa Habari Shinyanga (SPC) ziliwasilisha ripoti zao.

Akihitmisha kwa kutoa neno la shukurani juu ya mradi huo, Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia amesema kuwa halmashauri hiyo ni pekee katika mkoa huo ambayo imechaguliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo hivyo amewaomba wadau wote kushirikiana kuhakikisha kwamba wanautekeleza kwa mafanikio.

“Kinachofanyika hapa hakifanyiki maeneo mengi nchini, tunategemea watu wengi watakuja kujifunza hapa,” amesema.

PICHA MBALIMBALI KATIKA KIKAO HICHO
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale akitoa maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa serikali katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unakuwa wa mafanikio na wanaacha kuwa sehemu ya visababishi vya kuukwamisha. Ngwale ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Edward Maduhu (kulia) akifungua kikao hicho
Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Mhoja akitolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali katika kikao hicho na kuongoza mijadala
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akichangia mawazo kwenye mawasilisho ya utekelezaji wa mradi katika kikao hicho
Mratibu wa MTAKUWWA Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo, Aisha Omary akiwasilisha namna ambavyo halmashauri hiyo imetekeleza afua za MTAKUWWA
Mratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC), Estomine Henry akiwasilisha utekelezaji wa mradi wa 'Nafasi ya vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto'
Mratibu wa Miradi wa Shirika la RAFIKI -SDO, Charles Ally akiwasilisha namna shirika hilo lilivyotekeleza mradi wa 'TUWALEE' ambao ulilenga kuongeza uelewa juu ya stadi za malezi bora kwa wazazi na walezi na kuwasaidia watoto kushiriki katika kazi mbalimbali
Mwakilishi wa Shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI) akiwasilisha namna ambavyo shirika hilo limetekeleza mradi wa 'SHULE SALAMA KWA WOTE' katika kata ya Pandagichiza
Afisa Miradi wa Shirika la Young Women Leadership (YWL), Veronica Masawe akiwasilisha jinsi ambavyo shirika lake limetekeleza mradi wa kupiga vita mila na desturi zinazochochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia akisisitiza mambo mbalimbali katika kutekeleza afua za MTAKUWWA
Afisa Miradi wa Shirika la Young Women Leadership (YWL), Veronica Masawe akitoa neno la shukrani kwa niaba ya taasisi zilizoshiriki kutekeleza mradi huo
Wadau wakifuatilia kikao
Kikao kikiendelea
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Shingila, Stephen Peter akichangia hoja
Kikao kikiendelea
Afisa Maendeleo ya jamii kata ya Mwalukwa, Elypendo John akichangia hoja kwenye mawasilisho katika kikao hicho
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI), Rehema Katabi akichangia mawazo kwenye kikao hicho
Kaimu Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kitengo cha Sheria, Frank Singo akitoa maelezo namna wanavyofanikisha mchakato wa uundaji sheria za vijiji kukomesha ukatili
Afisa Maendeleo ya jamii kata ya Nyamalogo, Goodluck Cleopa akichangia mjadala
Wawakilishi dawati la jinsia wakishiriki kwenye kikao hicho
Mwanafunzi wa shule ya msingi Iganza, Elias John akishiriki kikao hicho
Mwakilishi kutoka BAKWATA, Hemedi Rashidi akitoa maoni
Afisa Mtendaji Kata ya Mwalukwa, Kadushi Deogratias akishauri utumiaji wa sungusungu katika mapambano ya ukatili na idara ya elimu kutenga muda wa masomo ya ukatili
Kaimu Afisa Lishe Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Edwin Ibrahim akishauri ufuatiliaji ufanyike kwa watoto walio chini ya miaka 18 ambao wanaoolewa na kupewa mimba wasio katika mfumo wa masomo
Mratibu wa WFT, Glory Mbia akishauri ushirikishaji wa wadau katika utungaji wa sheria ndogo ngazi ya vijiji zinazolenga kutokomeza ukatili
Mkurugenzi wa Shirika la TVMC, Mussa Ngangala akishauri mambo mbalimbali katika kikao hicho
Picha ya pamoja na wadau na mashirika 
Picha ya pamoja ya wadau walioshiriki kikao hicho



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464