MATUMAINI YA WAFANYAKAZI KUHUSU MISHAHARA YAGONGA MWAMBA, RAIS SAMIA AELEZA SABABU, AWAPA MATUMAINI MWAKANI

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza leo kwenye sherehe za Mei Mosi Kitaifa jijini Mwanza

Na Damian Masyenene
JUHUDI za takribani miaka 8 za wafanyakazi kuhakikisha kuwa viwango vya mishahara na madaraja katika sekta ya umma vinapandishwa mwaka huu, zimegonga mwamba baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kuwa ameshindwa kutimiza hitaji hilo la wafanyakazi kutokana na uchumi kudorora kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Mei 1, 2021 kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi Kitaifa katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza yaliyobeba kaulimbiu ya 'Maslahi Bora, Mishahara Juu, Kazi iendelee'.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) iliyotolewa mapema na Kaimu Katibu Mkuu wake, Said Wamba ilieleza kuwa wafanyakazi wa sekta ya umma hawajapandishiwa mishahara kwa miaka sita sasa, huku wale wa sekta binafsi wakifikisha miaka nane bila kupandishiwa mishahara.

Rais Samia amesema kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa huo, uchumi wa Tanzania umepungua, huku akiwa ana muda mfupi kwenye uongozi hivyo anajipanga na kuwapa matumaini kuwa mwaka ujao tarehe kama ya leo watarajie mambo mazuri kwani mambo mengi yatakuwa yamerudi kwenye msitari.

Ameongeza kwa kueleza kuwa sababu zingine ni jumla ya watumishi 85,000 -91,000 wanakwenda kupanda vyeo hivvyo kuigharimu Serikali Sh Milioni 449, kulipa malimbikizo ya mishahra yanayofikia Sh. Bilioni 60, mabadiliko ya muundo wa uongozi yatakayogharimu Sh. Bilioni 120 mabadiliko muundo wa viongozi pamoja na ajira mpya za watumishi 40,000 sekta ya afya na elimu itakayogharimu Sh Bilioni 239.

"Changamoto zote mlizozitaja ni za kweli na za msingi, katika kipindi changu cha uongozi nitahakikisha nashirikiana nanyi katika kuzishughulikia changamoto hizi na kuzipunguza ama kuzimaliza kabisa.

"Ndugu zangu mimi ni mama na mama ni mlezi…..wafanyakazi wenzangu, mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, mimi binafsi natamani kuona mishahara ya watumishi inaongezwa, lakini kutokana na sababu mbalimbali nimeshindwa kukidhi hitaji lenu. 

"Uwezo wetu kiuchumi umepungua. Imekuwa ni vigumu kwangu kwa sababu ndiyo nimeingia na sijakaa vizuri nimeshindwa kupandisha mishahara mwaka huu. Lakini serikali tumejipanga kuboresha maslahi yenu na tunakusudia kupunguza viwango vya kodi za mishahara kwa watumishi na kupunguza mfumuko wa bei ili kupunguza ukali wa maisha kwa watumishi, lakini mwakani siku kama ya leo nitakuja na mpango mzuri," ameahidi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametangaza kuwa Serikali imepunguza asilimia moja ya makato ya PAYE kwenye mishahara na marupurupu mengine na sasa wafanyakazi watakatwa asilimia 8 badala ya 9.

Pia ametangaza kuwa kuanzia mwezi huu (Mei) serikali itaanza kulipa mafao ya wastaafu na itafanya hivyo kila mwezi ili kupunguza mlundikano uliopo, huku akieleza kuwa suala la kucheleweshwa kwa mafao ya wastaafu linamsikitisha kuona watu hao wanazungushwa, hivyo akaielekeza mifuko ya jamii kuwalipa wastaafu hao.

"Kuhusu madeni na madai ya watumishi, serikali inajitahidi kulipa na kuhakiki madeni hayo, napenda kuwahikikishia kuwa serikali italipa madeni yote inayodaiwa na watumishi. Napenda kuonya watendaji wanaozalisha madeni na watumishi wanaotengeneza madeni hewa.

"Suala la bima ya afya – kwenye hili serikali imeona mantiki, ikiwemo mtoto wa miaka 18 bado ni mtegemezi kwa mzazi, tumeona tuongeze umri wa utegemezi kutoka miaka 18 hadi 21. Vilevile, serikali imefuta 6% iliyokuwa ikitozwa zaidi kwenye mkopo wa elimu ya juu, na kuamua kuendelea na asilimia 15 inayokatwa kawaida kwenye mishahara kwa watumishi wa umma," amesema.

Vilevile, kuhusu sakata la watumishi wa darasa la saba waliostaafishwa ajira hususan waliogundulika kuwa hawakufanya udanganyifu wala kughushi vyeti, amewaagiza waajiri wote waliokuwa na wafanyakazi wa namna hii, wahakikishe kila mwenye haki alipwe haki yake, huku akiitaka wizara inayoshughulikia utumishi bora kusimamia hilo.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464