Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais-Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, katikati ni Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo, kupunguza umasikini na kukuza uchumi.
Mhe. Majaliwa ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
“Matokeo ya sensa yataiwezesha Serikali kupata takwimu za msingi zinazotumika kuakisi hali halisi iliyopo na kupanga mipango ya maendeleo kwa kutunga sera pamoja na kupanga mipango, program na kufuatilia utekelezaji wake”, alisema Mhe. Majaliwa.
Alisema ni muhimu wananchi watoe ushirikiano kwa wakusanya takwimu ili kuliwezesha zoezi hilo kuenda vizuri na kuleta matokeo tarajiwa kwa maendeleo ya nchi.
Aidha, aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuanza kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.