Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mei 31, 2021 mjini Shinyanga
Na Damian Masyenene, SHINYANGA
MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Idd Masasi (43) mwenye makazi katika mtaa wa Ndembezi manispaa ya Shinyanga na Kigamboni jijini Dar es Salaam, ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa majibizano ya risasi na askari hao wakimtuhumu kuhusika na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akisimulia tukio hilo wakati akitoa taarifa mbele ya vyombo vya habari mjini Shinyanga leo Mei 31, 2021, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba ameeleza kuwa jana Mei 30, 2021 jeshi hilo lilipata taarifa za siri za uwepo wa jambazi (Idd Masasi) ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa matukio yaliyotokea hivi karibuni Kigamboni, Dar es Salaam yenye namba KGD/IR/1050/2021 na KGD/IR/411/2021, ambapo taarifa hizo za siri zilieleza kuwa jambazi huyo alikimbilia mkoani Shinyanga baada ya kutenda matukio hayo jijini Dar es Salaam.
Taarifa hizo za siri pia zilibainisha kuwa hivi karibuni mtuhumiwa anapenda kutembelea maeneo ya soko la Nguzo Nane lililopo kata ya Kambarage mjini Shinyanga kwa ajili ya kusoma maeneo ya kutenda uharifu ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina wafanyabiashara mbalimbali.
Pia kumbukumbu zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo alishawahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2011 na kutumikia adhabu hiyo katika gereza la Butimba, Mwanza na baadae alitoka kwa rufaa.
“Baada ya kupata taarifa jeshi letu tukishirikiana na kikosi kazi cha askari kutoka jijini Dar es Salaam liliweka mtego maeneo ya soko la Nguzo Nane na ilipofika saa tano asubuhi jambazi huyo alifika maeneo hayo. Hata hivyo, kikosi chetu kilikuwa tayari kimeshamuona na alipogundua kuwa anafuatiliwa na askari alianza kukimbia ndipo askari walipompa ilani ya kusimama kwa kufyatua risasi hewani.
“Lakini hakusimama, hivyo askari waliamua kumfyatulia risasi mbili bila kuleta madhara kwa watu wengine waliokuwepo eneo hilo, risasi hizo zilimjeruhi jambazi huyo mguu wa kushoto na sehemu ya mgongoni na hivyo kuweza kumkamata,” amebainisha ACP Magiligimba.
Baada ya majeraha hayo, mtuhumiwa huyo wa ujambazi alikimbizwa hospitali ya rfaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu ya majeraha aliyoyapata na alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uharifu na waharifu ili mkoa huo uendelee kuwa salama, huku akiwaonya waharifu wanaopanga kutenda uharifu na kukimbilia mkoani humo baada ya kufanya vitendo vya uharifu.
“Nitoe onyo kwa waharifu wote kuwa mkoa wetu siyo sehemu rafiki ya kutenda uharifu au kukimbilia waharifu kujificha baada ya kufanya uharifu mikoa mingine kwani jeshi la polisi limejipanga vizuri kukabiliana nao, aidha mharifu yeyote atakayethubutu kufanya uharifu atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, waharifu wote wafahamu kwamba sehemu ambayo wapo na sisi jeshi la polisi tupo,” amesisitiza Kamanda huyo.
Akikabidhiwa ofisi Mei 26, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati alisema kuwa moja ya vipaumbele vyake vikubwa ni kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa salama na wenye amani na utulivu ili wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi bila hofu ili kuuletea mkoa huo maendeleo endelevu.