RC SENGATI, WAANDISHI WA HABARI WATETA, WAAHIDI KUUNGANISHA NGUVU KWA MASLAHI MAPANA YA MKOA HUO

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akiteta na waandishi wa habari katika kikao cha kufahamiana kilichowakutanisha leo

Na Shinyanga Press Club Blog
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati amekutana na kufanya mazungumzo na waandishi wa habari mkoani humo kwa lengo la kufahamiana, kubadilishana mawazo na kupata maoni ya namna gani watafanya kazi kwa ushirikiano ili kuutangaza mkoa huo na fursa zake kwa nia ya kuvutia wawekezaji na utalii.

Dk. Sengati amekutana na wanahabari hao leo Mei 27, 2021 ofisi kwake siku moja baada ya kukabidhiwa ofisi baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo akitokea mkoani Tabora na kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ambaye amehamishiwa Lindi.

RC Sengati ameahidi kufanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano mkubwa ili kuinua mkoa huo, huku akieleza kuwa siku zote anapenda kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo vya habari na kamwe haipendezi kuona mkoa huo unafanya mambo mengi mazuri lakini hayatangazwi wala kufahamika kwa umma wa Watanzania.

“Mkoa wetu unayo mambo mazuri mengi, natamani sana tufanye kazi kuyatangaza hayo mazuri ili kusudi Watanzania wayafahamu na wajue nini kinaendelea katika mkoa wetu. Siyo vizuri kuwa na mkoa ambao umesinzia kwenye vyombo vya habari taarifa zake nzuri hazisikiki,” amesema Dk. Sengati.

Mwandishi wa ITV/Radio One mkoani hapa, Frank Mshana ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), amempongeza Dk. Sengati kwa kuteuliwa, huku akimshukuru kwa kuthamini na kutambua mchango wa waandishi wa habari, ambapo amemuomba asiwaache nyuma kwenye matukio muhimu ya kimaendeleo ya mkoa huo.

Naye Mwakilishi wa Clouds Media, Kasisi Kosta amemuomba mkuu huyo wa mkoa kutengeneza mahusiano mazuri na waandishi wa habari na kuweka ushirikiano thabiti kwenye mambo muhimu yanayogusa maslahi ya umma, huku Mwandishi wa magazeti ya Habari Leo na Daily News, Kareny Masasy akimuomba aondoe changamoto ya baadhi ya watendaji wa serikali katika mkoa huo kuwagawa waandishi wa habari kwa kufanya kazi na vyombo fulani pekee wanavyoviita ni ‘Vikubwa’ huku wakibagua vingine kuwa ni ‘vidogo’.

Mwandishi wa Magazeti ya Nipashe na The Guardian, Marco Maduhu amemuomba Dk. Sengati kutataua changamoto iliyopo ya waandishi kuachwa na kutoshirikishwa kwenye baaadhi ya matukio makubwa ya kihabari na ya kimaendeleo katika mkoa huo, huku kukiwa na ubaguzi katika ushirikishwaji wa vyombo vya habari, ambapo baadhi ya watendaji wamekuwa wakifanya kazi na runinga pekee.

Dk. Sengati ameahidi kukutana tena na waandishi hao katika kikao kikubwa kitakachowajumuisha waandishi wote wa habari mkoani humo kwa ajili ya kuendelea kufahamiana na kuweka mikakati zaidi.
Dk. Sengati (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo

Picha na Marco Maduhu
 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464