SAVE THE CHILDREN LAWAPIGA MSASA WAKUU WA IDARA, MADIWANI, ASASI ZA KIRAIA SHINYANGA JUU YA UONGOZI BORA NA KUEPUKA MIGOGORO

Mratibu wa mradi wa mijadala jumuishi katika maswala ya uchumi na utawala wa fedha kutoka shirika la Save The Children, Alex Enock (aliyesimama) akiwashuhudia washiriki wa mafunzo hayo wakijadiliana na kuweka maazimio mbalimbali baada ya mafunzo.

Na Shinyanga Press Club Blog
Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga limetoa mafunzo ya uongozi na utawala bora kwa wakuu wa idara, madiwani, viongozi wa asasi za kiraia pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani humo.

Mafunzo hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa Empire na kukutanisha viongozi hao yakilenga kuwajengea uwezo wa kuongoza kwa kufata misingi bora ya uongozi hali itakayosaidia kupunguza malalamiko na migongano ya kimaslahi baina yao na wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa mradi wa mijadala jumuishi katika maswala ya uchumi na utawala wa fedha kutoka shirika la Save The Children, Alex Enock amesema kuwa wanawajengea uwezo viongozi hao ili waweze kufanya kazi kwa weledi wakizingatia maslahi ya wananchi wakati wa utendaji kazi wao.

Enock ameongeza kwa kueleza kuwa iwapo washiriki waliopatiwa mafunzo hayo watayafanyia kazi vizuri itasidia kupunguza malalamiko ya wananchi na kuchochea maendeleo kwenye maeneo yao

“Naombeni sana washiriki mzingatie mafunzo hayo maana tutafanya ufatiliaji ili kubaini kama kuna mabadiliko yoyote yaliyopatikana kutokana na mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kuangalia mienendo yenu katika utendaji kazi,” amesema Enock.

Nao wawezeshaji kutoka Tamisemi idara ya serikali za mitaa, Meshaki Mgovano, Jonasi Kipwani kutoka chuo cha serikali za mitaa Homboro Dodoma pamoja Eliud Mkiramweni ambaye ni mchumi kutoka wizara ya fedha na mipango kwa pamoja wamewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia miiko ya uongozi ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo wao wenyewe kupoteza imani kwa wananchi wanaowaongoza na kupelekea kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki walio patiwa mafunzo hayo wameahidi kubadilika nakufanya kazi kwa weledi maana awali wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na uzoefu hali ambayo imekuwa ikikwamisha maendeleo na kuchochea migogoro na malalamiko ya wananchi kwenye maeneo yao.
Mratibu wa mradi wa mijadala jumuishi katika maswala ya uchumi na utawala wa fedha kutoka shirika la Save The Children, Alex Enock akitoa mafunzo kwa washiriki
Mwezeshaji kutoka Tamisemi idara ya serikali za mitaa, Meshaki Mgovano akiwasilisha mada katika mafunzo hayo
Jonasi Kipwani kutoka chuo cha serikali za mitaa Homboro Dodoma akitoa mafunzo ya uongozi bora kwa washiriki
Mchumi kutoka wizara ya fedha na mipango, Eliud Mkiramweni akizungumza kwenye mafunzo hayo
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464