SERIKALI YATANGAZA AJIRA MPYA ZA UALIMU NA SEKTA YA AFYA

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu, leo Mei 09, 2021 ametangaza nafasi za ajira za ualimu wa shule za msingingi na sekondari sambamba na sekta ya afya, ambapo waombaji wanapaswa kuanza kutuma maombi yao leo mpaka Mei 23, 2021.

Waziri Ummy amesema kutangazwa kwa ajira hizo, kunakuja kufuatia serikali kutoa kibali cha nafasi za ajira 6949 za ualimu na 2726 za kada mbalimbali katika sekta ya afya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliofariki dunia, walioacha kazi, waliofukuzwa pamoja na waliostaafu.

Akivitaja vigezo vya waombaji, Waziri Ummy amesema kwa upande wa ualimu wa shule za msingi, ualimu wa Daraja la 3A, mwombaji anapaswa kuwa na astashahada ya ualimu wa elimu ya awali, elimu ya msingi au elimu ya michezo huku ualimu wa Daraja la 3B, waombaji wakitakiwa kuwa stashahada ya elimu ya awali, elimu ya msingi au elimu maalum ambaapo waombaji watakaopewa kipaumbele ni wale waliosomea masomo ya English, History na Geography.

Kwa upande wa ualimu wa sekondari, Waziri Ummy amesema watakaopewa kipaumbele ni wale waliosomea masomo ya Physics, Mathematics, Chemistry na Biology huku akizitaja sifa za mwombaji wa Daraja la 3C kuwa ni Stashahada ya Ualimu katika masomo yaliyotajwa hapo juu, Stashahada ya elimu maalum katika masomo tajwa, mhitimu wa shahada ya uzamili katika elimu (post graduate degree in education).

Jinsi ya kutuma maombi hayo, mwombaji anatakiwa kutuma kwa njia ya mtandao kwa kuingia katika tovuti ya http://www.ajira.tamisemi.go.tz huku akiwasisitiza waombaji kuwa makini na matapeli wanaowataka kutuma kwanza fedha iliwapate nafasi hizo na kueleza kwamba ajira zote zitatolewa kwa haki kwa waombaji wenye sifa na vigezo.

Kwa maelezo zaidi na jinsi ya kutuma maombi, bofya link hii http://www.ajira.tamisemi.go.tz Mwisho wa kutuma maombi ni Mei 23, 2021.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464