Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile akizungumza na wafamasia, wataalam wa huduma za maabara na wataalam wa mifugo mkoani Shinyanga wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kilichoanza leo Mei 11, 2021 kwenye ukumbi wa Mkuu wa mkoa huo
Na Damian Masyenene, Shinyanga
WAFAMASIA, Waratibu huduma za maabara na mifugo mkoani Shinyanga wametakiwa kufuatilia na kudhibiti ubora wa dawa za mifugo, maduka bubu na yaliyosajiliwa, uingizwaji kinyemela wa dawa na vifaa tiba kutoka nchi jirani na kulinda mali za serikali kwa kudhibiti wizi wa dawa kwa kuweka mfumo wa mawasiliano na watendaji ngazi za chini ili kupata taarifa za dawa ambazo hazina ubora, hazijasajiliwa ama zimeondolewa sokoni.
Wito huo umetolewa leo Mei 11, 2021 mjini hapa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RMO), Dk. Yudas Ndungile wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kilichoanza leo kilichoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kinachowakutanisha wafamasia, waratibu huduma za maabara na wataalam wa huduma za mifugo kutoka halmashauri za mkoa huo.
Dk. Ndungile lengo la kikao kazi hicho ni kudhibiti usambaaji wa dawa zisizo na ubora ili kutohatarisha maisha ya wananchi, kazi ambayo inatakiwa kutekelezwa kwa kujikita kwenye miiko na maadili ya utumishi wa umma.
“Nawasihi tuwe makini kusikiliza na kufuatilia mijadala na mada zitakazowasilishwa ili kuondoka na uelewa na ujuzi utakaotuwezesha kufanya udhibiti na ufuatiliaji. Tumezungukwa na nchi jirani ambazo hazina mfumo thabiti wa ufuatiliaji kwahiyo kuna uwezekano wa kuingia dawa ambazo hazijasajiliwa ama hazina ubora.
“Tunayo kazi kama wadhibiti kuhakikisha tunafuatilia kwa karibu mienendo hususan maduka bubu na hata yale yaliyosajiliwa na tulinde mali za serikali. Jukumu hili hatuwezi kulifanya peke yetu tushirikiane na mifumo iliyopo ya kiuongozi katika mamlaka zetu za serikali, tushirikiane nao tupate taarifa za watu wanaotembea kuuza dawa za serikali mitaani na uanzishwaji wa maduka bubu, maabara bubu na maduka bubu ya mifugo,” amesisitiza.
Dk. Ndungile ameongeza kwa kuwataka wakaguzi hao kutosubiria tu shughuli za kwenda kukagua bali waweke mfumo wa kuwasiliana na watendaji katika ngazi za chini ili kupata taarifa za dawa ambazo hazina ubora, hazijasajiliwa ama zimeondolewa sokoni na watu hawana taarifa
“Tunao wajibu wa kushirikiana na wamiliki wa maduka ya dawa baridi, waagizaji ili kupeana taarifa ya dawa ambazo hazipaswi kuwepo sokoni, dawa gani ambazo hazijasajiliwa na zile zilizotoka nje ya nchi na haziruhusiwi kuuzwa nchini ili kujua namna ya kufanya udhibiti,” ameeleza.
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk. Edgar Mahundi amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutoa elimu namna ya kuimarisha shughuli za udhibiti wa dawa kwani kumekuwepo na vitendo vya uuzaji wa dawa kwa kificho, uingizaji vifaa tiba na dawa kinyume na utaratibu kutokanana nchi yetu kupakana na mataifa jirani, jambo ambalo linaweza kuleta madhara kwa afya ya watanzania na uchumi wa taifa.
Dk. Mahundi amesema kuwa kutokana na uwepo wa vitendo hivyo, wagonjwa wamekuwa wakipata madhara kutokana na vifaa tiba, dawa na vitendanishi visivyokidhi ubora, hivyo wakaguzi wanahitaji kuboresha ufanisi katika suala la kudhibiti wa biashara hiyo.
Amesema kupitia kikao hicho, wadau wataweza kuboresha ufanisi katika manunuzi, matumizi na utunzaji wa vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwani matumizi ya dawa hizo yanahitaji usimamizi sahihi, huku akiwahimiza wakaguzi kuzingatia maadili.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Mtani Njegere akiwasilisha mada ya mifumo ya ukaguzi, amesema kuwa malengo ya ukaguzi ni kujiridhisha kuwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyotengenezwa nchini ama nje ya nchi vinakidhi masharti ikiwemo ubora, ambapo ukaguzi huo unahusisha vibali, majengo, wafanyakazi, bidhaa na nyaraka.
Amewaasa wafamasia wa halmashauri nchini kuchukua hatua pale inapopaswa kuliko kukaa kimya wakidhani shughuli hiyo inawahusu TMDA peke yao, ambapo akitolea mfano wa jambo hilo ameeleza kuwa kwenye usafiri wa mabasi ya umma kumekuwa na wauzaji wa dawa ambao hutumia lugha ya uongo kunadi biashara hiyo lakini wafamasia wanafumbia macho suala hilo na kutochukua hatua.
“Kwenye ukaguzi unakuta wengine kwa mfano akisafiri wanawaachia watu ambao hawana elimu ya jambo hilo mfano wafanyakazi wa ndani na Watoto, tena kwenye maduka ya dawa za mifugo ndiyo balaa kabisa unakutana mtoto ndiye anauza ukimuuliza anakwambia kwamba alikuwa anatazamia kwa baba yake alivyokuwa anafanya ndipo nay eye akajua,” ameeleza.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho ambao ni wakaguzi kutoka halmashauri za mkoa huo akiwemo Afisa Mifugo Manispaa ya Shinyanga, Veron Mwaluko, Mfamasia Dawson Felician na Benson Kitunda kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wameomba mamlaka kuweka mfumo thabiti wa kudhibiti uuzaji holela wa dawa na famasi na maduka ya dawa yasiyokidhi vikego ambayo yanauza dawa zisizotakiwa kuuzwa na maduka hayo, huku wakipendekeza adhabu kali kwa baadhi ya waagizaji wanaoendelea kuingiza nchini dawa zilizopigwa marufuku ama kuondolewa sokoni.
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk. Edgar Mahundi akizungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha wakaguzi wa dawa na vifaa tiba kutoka halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile ambaye alikuwa mgeni rasmi wa kikao hicho akizungumza na washiriki
Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA, Mtani Njegere akiwasilisha mada ya mifumo ya ukaguzi kwa washiriki wa kikao hicho
Mshiriki wa mafunzo hayo, Veron Mwaluko ambaye ni Afisa Mifugo mkoa wa Shinyanga akichangia hoja kwenye mada zilizowasilishwa katika kikao hicho
Mfamasia Benson Kitunda kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akichangia mawazo kwenye kikao hicho
Mfamasia Dawson Felician akitoa maoni juu ya kudhibiti uuzwaji holela wa dawa maeneo ya vijijini
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk. Edgar Mahundi akiwasilisha mada ya sifa, wajibu, majukumu na maadili ya wakaguzi
Washiriki wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali katika kikao hicho
Washiriki wakifuatilia kwa umakini uwasilishaji wa mada
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Washiriki wakisikiliza kwa umakini hoja mbalimbali katika kikao hicho
Washiriki wakiendelea na kikao hicho
Mgeni rasmi, Dk. Yudas Ndungile (katikati waliokaa) na maafisa wa TMDA wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Mgeni rasmi, Dk. Yudas Ndungile (katikati waliokaa) na maafisa wa TMDA wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Mgeni rasmi, Dk. Yudas Ndungile (katikati waliokaa) na maafisa wa TMDA wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao hicho