Wafanyakazi wakiwa katika maadhimisho ya Mei Mosi kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, leo. (Picha na BMG)
Na Shinyanga Press Club Blog
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewasilisha kilio cha wafanyakazi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan na kupendekeza kuwa kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kiwe Sh. 970,000 ili kumuwezesha mfanyakazi kumudu gharama za maisha kwani kwa sasa hali ya maisha iko juu, huku mishahara ikiwa haijapanda kwa miaka sita sasa.
TUCTA imewasilisha kilio na mapendekezo hayo leo Mei Mosi, 2021 kwenye maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi kitaifa katika Uwan ja wa CCM Kirumba, Mwanza yakiwa yamebeba kauli mbiu ya 'Maslahi Bora, Mishahara Juu, Kazi iendelee'.
Akiwasilisha taarifa ya TUCTA, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Said Wamba amesema kuwa mishahara katika sekta binafsi/isiyo rasmi mishahara haijapandishwa kwa miaka nane, huku sekta ya umma ikiwa ni miaka sita, hali ambayo imepelekea kupunguza ufanisi kwa wafanyakazi.
"Kima cha chini cha mishahara kimeendelea kuwa duni ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha....Kwa sasa Tucta tunapendekeza Sh. 970,000 na wakati umefika kuwa na kiwango halisi cha kitaifa kitakachomwezesha mfanyakazi kuishi na kumudu maisha kutokana na hali halisi ya maisha kupanda," amesema.
TUCTA pia imeiomba Serikali kupandisha mishahara kwa mwaka huu, huku ikidai kuwa wafanyakazi wamekuwa wakikamuliwa kodi kubwa tofauti na kada nyingine.
Wamba pia amedai kuwa kuna uchelewashaji wa mafao ya wastaafu, kwani hadi sasa ni miaka mitatu wastaafu hawajalipwa stahiki zao, hivyo akaiomba Serikali kulifanyia kazi na mifuko ya hifadhi iwalipe mafao wastaafu.
Katibu Mkuu huyo ameiomba Serikali kulipa madai sugu ya wafanyakazi, kwani watumishi wengi wanaidai serikali yaliyotokana na malimbikizo ya mishahara, uhamisho, upandishwaji vyeo watumishi wanaostahili kwa mujibu wa sheria za ajira.
"Watumishi wa kiwango cha elimu ya darasa la saba ambao walisitishiwa mishahara na Julai mwaka 2017 waliondolewa kwenye utumishi wa umma, pamoja na maelekezo ya serikali ya kuwalipa stahiki zao kwa ambao hawakufanya udanganyifu lakini wapo waajiri ambao hadi leo hawajatekeleza maagizo ya serikali pamoja na yale ya Rais.
"Tunaomba serikali izingatie watumishi ambao hawakufanya udanganyifu ama kughushi vyeti, pia serikali itoe maelekezo kwa waajiri hawa waweze kulipa stahiki hizo," amesisitiza Wamba.