WAUGUZI SHINYANGA WAADHIMISHA SIKU YAO KWA KUTOA BURE HUDUMA ZA VIPIMO, AFYA YA UZAZI NA KUCHANGIA DAMU

Wauguzi hao wakielekea katika kituo cha afya Kambarage kwa ajili ya kutoa msaada na huduma za bure za matibabu kwa wagonjwa

Na Shinyanga Press Club Blog
WAUGUZI katika halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani hapa wameungana na wauguzi duniani kote kuadhimisha siku ya wauguzi duniani, ambayo wameiadhimisha kwa kutoaa huduma za afya bure na kutembea mtaa kwa mtaa kwa maandamano yenye lengo la kuwahamasisha wananchi kupima afya na kutoa damu kwa lengo la kuokoa maisha ya wanawake na watoto wachanga wakati wa kujifungua na wagonjwa wenye uhitaji.

Siku ya wauguzi duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 12 ikiwa ni kumuenzi muasisi wa taaluma ya uuguzi Frolence Nightingale, ambapo maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya ‘Wauguzi ni sauti inayoongoa dira katika huduma za afya’.

Akizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa niaba ya muuguzi mkuu wa manispaa ya Shinyanga baada ya kuchangia damu na kupima afya, Afisa Muuguzi Msaidizi Kituo cha afya Kambarage, Pudensiana Rwebangira amesema wameyaanza maadhimisho hayo tangu Mei 8, mwaka huu kwa kuandaa huduma mbalimbali kwenye jamii hususan zinazolenga afya ya uzazi ikiwemo upimaji virusi vya ukimwi (VVU) kwa vijana, akina mama na wanaume.

Pia walitoa huduma ya uchunguzi saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama, huduma ya afya ya uzazi kwa vijana na uzazi wa mpango pamoja na huduma ya damu salama kwa kukusanya zaidi ya chupa 15 ambazo zitakuwa msaada kwa akina mama wajawazito wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua, huku wananchi hasa vijana wakiitikia kwa wingi kupata huduma ya saratani mlango wa kizazi, uzazi wa mpango na upimaji wa VVU.

“Katika siku ya leo ya kilele cha maadhimisho haya, wauguzi wa manispaa tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu ajira upande wa kada ya uuguzi kwani wauguzi wanaelemewa na kazi kubwa, hivyo ajira hizo zitasaidia kupunguza mzigo huo na kusogeza mbele huduma kwa jamii,” amesisitiza.

Naye Daktari Muuguzi wodi ya wanawake kituo cha afya Kambarage, Dk. Daniel Nsaningu ameishukuru serikali kwa hatua ya kutangaza ajira mpya katika kada ya afya kwani zitasaidia kupunguza changamoto zilizopo na kupelekea huduma bora za afya kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi akiwemo Peter Gembe na Veronica Nyorobi waliojitokeza kupata huduma na walionufaika na huduma hiyo baada ya hamasa iliyotokana na wauguzi hao, wameshukuru na kupongeza namna wauguzi hao walivyoonyesha upendo kwa kujali afya ya jamii na kuonyesha namna wanavyojali na kuipenda kazi yao.
Afisa Muuguzi Msaidizi Manispaa ya Shinyanga, Pudensiana Rwebangira akizungumzia shughuli zilizofanywa na wauguzi katika halmashauri hiyo ili kuadhimisha siku ya wauguzi duniani
Mganga Mkuu Manispaa ya Shinyanga, Dk. Elisha Ndaki akizungumza na wauguzi katika kilele cha maadhimisho ya siku yao ambayo yemefanyika katika kituo cha afya Kambarage
Daktari Muuguzi wodi ya wanawake kituo cha afya Kambarage, Dk. Daniel Nsaningu akizungumzia umuhimu wa wauguzi katika kuboresha huduma za afya kwa jamii
Wauguzi wakiwa kwenye maandamano katika kilele cha siku ya wauguzi duniani
Wauguzi wakiadhimisha siku yao
Maadhimisho ya siku ya wauguzi yakiendelea mjini Shinyanga
Maadhimisho yakiendelea
Wauguzi wakiwasha mishumaa kuashiria upendo kwa wagonjwa na kumkumbuka muasisi wa taaluma ya uuguzi, Frolence Nightingale
Baadhi ya wauguzi katika manispaa ya Shinyanga wakitoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa katika wodi ya wazazi kituo cha afya Kambarage wakati wa kuadhimisha siku ya wauguzi duniani
Wauguzi wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa katika kituo cha afya Kambarage
Huduma za vipimo zikiendelea kwa wananchi
Wauguzi wakiendelea na huduma ya vipimo vya VVU kwa vijana
huduma za vipimo zikiendelea
Wauguzi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wao



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464