Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu akisalimiana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga leo baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuzungumza na sekretarieti ya mkoa huo na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo
Na Damian Masyenene, SHINYANGA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amezitaka halmashauri zilizopo mkoa wa Shinyanga kuhakikisha zinaongeza kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani ili kufikia malengo zilizowekewa, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, kusimamia vyema miradi ya maendeleo, kuzifanyia kazi hoja zilizoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhakikisha kila shule ya msingi inalo darasa la awali na kuwataka waweka hazina wa halmashauri hizo kujitathmini.
Ummy ametoa maelekezo hayo leo alipokutana na kuzungumza na sekretarieti ya mkoa huo pamoja na wakurugenzi wa halmashauri sita zilizopo mkoani hapo na watendaji wengine katika serikali mitaa, ambapo amewatahadharisha waweka hazina na maafisa mipango wa halmashauri kuwa siku si nyingi atapitia orodha yao kutathmini utendaji wao kwani wamekuwa kikwazo kwenye halmashauri.
Waziri huyo amebainisha kuwa ndani ya mwezi mmoja aliokaa katika wizara hiyo amegundua kuwa halmashauri zinapata mapato mengi lakini yanafujwa na yanatafunwa kabla ya kufikishwa sehemu husika, huku akizitaka pia kuifanyia kazi na kusimamia vyema mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato.
Pia amewaelekeza Mkuu wa Mkoa na Katibu tawala kuhakikisha wanakuwa macho muda wote katika halmashauri za Kishapu na Shinyanga DC kwani fedha za maendeleo zimetengwa kiduchu tofauti na maelekezo ya wizara ambayo yanazitaka halmashauri kutenga asilimia 40.
“Kishapu wametenga asilimia 30 tu ambazo ni Sh Milioni 407 lakini walipeleka Sh Milioni 130, Shinyanga DC wao wana asilimia 25 walitenga Sh milioni 700 zimepelekwa tu Sh Milioni 300, kwahiyo hii inadidimiza maendeleo ya wananchi na hiki kitatumika kama kipimo cha kupima utendaji kazi wa wakurugenzi wetu kwa sababu fedha kwenye halmashauri zipo lakini hazitumiki vizuri zinapigwa,” amesema.
Akizungumzia ripoti ya CAG ambayo mkoa wa Shinyanga haukufanya vizuri halmashauri mbili pekee (Kahama na Manispaa ya Shinyanga) kati ya sita ndizo zilizopata hati zinazoridhisha, Waziri Ummy ameeleza kuwa asilimia 83 ya hoja za mkaguzi ni za kiuhasibu na inaonyesha kuwa wakaguzi wa ndani hawakupitia ama kuziona hesabu za mwisho za halmashauri zao.
Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Shinyanga, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Albert Msovela amebainisha kuwa mkoa huo unao upungufu wa watumishi 3,216, waliopo ni 11,723 na mahitaji ni 12,935, huku akieleza kuwa hadi kufikia Aprili 31, mwaka huu mkoa huo umekusanya mapato asilimia 73.
Katika upande wa elimu, RAS Msovela ameeleza kuwa walipanga kuandikisha wanafunzi 40,517 wa awali lakini hadi kufikia Machi mwaka huu wameandikisha wanafunzi 38,510, darasa la kwanza wakiandikishwa 65,100 kati ya 61,265 waliopanga kuandikishwa, huku upungufu wa walimu ukiwa ni 476.
“Wanafunzi 26,255 walipangwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021, hadi kufikia Machi 31, mwaka huu jumla ya wanafunzi 24,226 sawa na asilimia 92 wameripoti, wavulana wakiwa ni 11,394 na wasichana ni 12,832,” amesema.
Akitoa maoni kwenye hoja zilizowasilishwa na Waziri Ummy, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amesema kuwa bajeti yao ilikwamishwa na kutofanya vizuri kwa mgodi wa Mwadui na zao la Pamba, huku akiomba mnada wa Muunze ubadilishwe na kuwa mnada wa awali, fedha za kuhamisha mizigo kwa watumishi hususan walimu ziletwe kwa wakati na maofisa utumishi waongezwe.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu wa mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julius Chambo akishauri fedha za miundombinu na ujenzi ziletwe kwa wakati kuliko hali ilivyo sasa ambapo zinaletwa zimechelewa na kwa muda mfupi zinatakiwa kurejeshwa tena hazina, huku akiomba vitendea kazi na fedha za ufuatiliaji ziletwe kusaidia ukaguzi.
Meneja wa TARURA Manispaa ya Shinyanga, Mhandisi Salvatory Yambi ameomba wawezeshwe magari kwani kwa sasa kwa zaidi ya miaka miwili hawana gari la usimamizi wa miradi, pia kuongezewa mafundi sanifu na waandisi.
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu (kulia) akisalimiana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga baada ya kuwasili leo kwa ziara ya kukagua miradi na kuzungumza na sekretarieti ya mkoa huo
Waziri Ummy Mwalimu akisalimiana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga leo baada ya kuwasili mkoani humo
Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu (wa tatu kutoka kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (kulia) wakati wa kikao na sekretarieti ya mkoa huo leo
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mkoa huo mbele ya Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu (hayupo pichani)
Viongozi mbalimbali wa serikali mkoani Shinyanga wakiwa katika kikao na Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwlaimu (hayupo pichani)
Kikao kikiendelea
Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri za mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye kikao hicho
Kikao kikiendelea
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu akitoa maelekezo kwa Meneja wa TARURA Manispaa ya Shinyanga, Mhandisi Salvatorty Yambi kuitaka Tarura kuanzia bajeti ijayo itekeleze miradi ya barabara kulingana na mapendekezo ya barabara la madiwani
Picha zote na Marco Maduhu