BASI LAANGUKA SHINYANGA, WATATU WAHOFIWA KUFA, MAJERUHI 34

Basi la Kampuni ya Classic likiwa limeanguka katika eneo la Buyubi

Na Shinyanga Press Club Blog
Watu watatu wanahofiwa kufa katika ajali ya basi la Kampuni ya Clasic eneo la Buyubi Kata ya Didia Mkoani Shinyanga, huku wengine 34 wakijeruhiwa baada ya basi hilo kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo imetokea usiku wa leo Saa 10 alfajiri ambapo basi hilo lilikuwa likitokea Jijini Kampala nchini Uganda kuelekea Jijini Dar es salaam, ambapo baadhi ya abiria wameeleza kuwa dereva wa basi hilo alikimbia baada ya ajali.

Baadhi ya majeruhi wamesema kuwa ajali hiyo imetokea baada ya dereva kushindwa kukata kona katika barabara ya Kahama-Shinyanga katika njia panda ya Didia.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa baadhi ya abiria waliokuwemo kwenye basi hilo ni wanafunzi wanasoma nchini Uganda ambao walikuwa wakisafiri kuja likizo Tanzania.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na hospitali ya misheni Bugisi kwa matibabu zaidi.

Mkuu wa jeshi la Polisi wilayani Shinyanga John Kafumu amefika eneo la tukio na kueleza kuwa taarifa zaidi zitatolewa na kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga Debora Magiligimba.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464