Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
Na Shinyanga Press Club Blog
CHANGAMOTO ya kukatika umeme mara kwa mara katika mji wa Shinyanga mkoani humo imeonyesha kuwakwaza wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wanaotegemea nishati hiyo katika uzalishaji mali.
Hali hiyo ya kukatika umeme pasipokuwepo sababu za kuridhisha huku Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoa wa Shinyanga likieleza kuwa tatizo hilo husababishwa na dharura mbalimbali, limedumu kwa muda mrefu sasa hali iliyofanya uvumilivu wa wadau hao kuwa mdogo.
Mjadala mkubwa uliibuka katika jukwaa la wadau wa maendeleo mkoani hapo linaloratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp liitwalo ‘Shy Press na Wadau’ baada ya Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Maji (EWURA CCC) mkoa wa Shinyanga, Joseph Ndatala kuchapisha andiko lenye ujumbe wenye kichwa cha habari ‘Tanesco Shinyanga Ijitathmini’ lililoibua maoni mengi ya wananchi na kulazimika Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na idara ya mahusiano Tanesco mkoa wa Shinyanga kutoa majibu.
Katika andiko lake Ndatala alihoji na kushauri kwa kusema “Umeme kila siku marekebisho kwa nini msitangaze rasmi kuwa kuna shida wafahamu wananchi!! kama kuna mgao wa umeme wananchi waambiwe maana kila siku masaa kadhaa hakuna umeme.
Ni maoni yangu Meneja Tanesco Mkoa wa Shinyanga atoke hadharani atuambie umma wa Shinyanga tatizo mahali lilipo, hii ni kwa sababu kitengo chake cha uhusiano kwa umma hakitupatii majibu mahali lilipo tatizo,”.
Katika maoni hayo, Wadau wengi waliitaka Tanesco kueleza na kuweka wazi sababu za kukatika umeme mjini hapo tofauti na maelekezo ya Serikali, huku kukatika huko kwa umeme kusiko na ratiba maalum wala sababu za msingi kukielezwa kusababisha hasara mbalimbali na kukwamisha baadhi ya shughuli za uzalishaji mali.
Mmoja wa wadau hao, alihoji kwa kusema ‘Umeme una faida Sana kwa wananchi na hata TANESCO wenyewe. Niliwahi kujiuliza hii ni manispaa gani ndani ya Km7 hakuna umeme,”
Mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo aliyetambulika kwa jina moja la Neema, alipeleka kilio chake kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati kwa kumuomba ashughulikie tatizo hilo kwani limekuwa sugu.
”Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunakuomba uanze na shida kubwa ya umeme usio wa uhakika katika mkoa wetu, tumekuwa na tatizo la kukatika umeme kila siku tena mara kwa mara, hii imetufanya kushuka kwa maendeleo yetu, tunahitaji umeme wakutosha na wa uhakika katika kazi na biashara zetu, tunahitaji umeme wa kutosha kwa familia na ndoa zetu, tunakuomba baba tuondolee kero hii kwani imekuwa ni janga na tatizo kubwa, tunakuamini na tuko tayari kushirikiana na wewe katika kuijenga Shinyanga yetu,” amesema.
Baada ya hoja hizo za wadau, Ofisi ya Idara ya Mahusiano kwa umma Tanesco Mkoa wa Shinyanga ilijibu hoja hizo kwa kuwapa pole wateja wake na kueleza kuwa changamoto iliyopo inatafutiwa ufumbuzi na hivi karibuni tatizo hilo litakwisha kabisa.
“Poleni sana Wakuu, tunaomba radhi kwa usumbufu unaojitokeza. Tunajitahidi kumaliza hili tatizo, linafika mwisho,” imesema taarifa hiyo.
Jambo hilo lilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko kujibu baadhi ya hoja na kutoa ufafanuzi wa hatua zilizofikiwa upande wa serikali kuhakikisha changamoto iliyopo katika manispaa hiyo inakwisha na kuondoa usumbufu unaojitokeza kwa wananchi wake, huku Mkuu huyo wa wilaya akipongezwa na wananchi kwa hatua hizo.
“Nimeongea na Mhe Waziri wa Nishati asubuhi na amewaelekeza TANESCO kufanya interchange wanapokuwa na matengenezo ili wananchi wasikose umeme. Ikitokea umeme utakatika kila siku maeneo hayo wadau wa umeme maeneo husika wanijulishe,” amesema.
"Hongera DC (mkuu wa wilaya) kwa juhudi zako, ninapenda sana kiongozi anayetumikia umma, bila hiyana nitumie nafasi hii kukupongeza kwa ziara yako ya kutembelea Kata kwa Kataambayo ilileta matunda katika maeneo tofauti. Kazi iendelee kiongozi,” amepongeza mjumbe wa EWURA CCC mkoa wa Shinyanga.