Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa ajali ya basi la Kampuni ya Classic katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani)
Na Marco Maduhu, Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kumkamata dereva wa basi la Kampuni ya Classic aliyejulikana kwa jina la Maxison Mkuru baada ya kutoroka jana muda mfupi baada ya gari hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 20 katika eneo la Buyubi Kata ya Didia wilayani Shinyanga.
Akitoa taarifa hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Debora Magiligimba ameeleza kuwa dereva huyo alifanikiwa kutoroka mara baada ya ajali kutokea, ambapo kwa sasa jeshi hilo linaendelea kumhoji na atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo, amesikitishwa na ajali ya basi la Classic iliyotokea jana mkoani Shinyanga na kuonya madereva wa vyombo vya moto kuacha kuendesha mwendo kasi ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, alipotembelea majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga.
Amesema madereva wa vyombo vya moto wanapaswa muda wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa pale wanapokuwa na abiria, ili kutosababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu.
“Katika ajali hii ya basi hapa mkoani Shinyanga, nimeambiwa chanzo chake ni mwendokasi hivyo nawaomba madereva wazitii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kugharimu maisha ya watu,”amesema Chilo
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga, Dkt. Agustine Maufi, amesema katika majeruhi 26 waliowapokea jana, Sita wamepewa Rufaa ya kwenda kutibiwa Bugando Jijini Mwanza, na 20 waliobaki wanaendelea na matibabu na hali zao ni nzuri.
Naibu Waziri akiwajulia hali majeruhi hao
Naibu Waziri akiwajulia hali majeruhi wa ajali ya basi katika hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga
Naibu Waziri akiwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea kuona majeruhi wa ajali ya basi katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga