Mzee wa Kanisa la Wasabato Mjini Shinyanga, Dkt. Ellyson Maeja (kushoto) akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Kaimu Katibu wa Afya (SRRH), Iveta Mtesigwa vilivyotolewa na kanisa la Sabato mjini Shinyanga kwa ajili ya kutibiwa watu waliojeruhiwa kwenye ajari ya basi la Classic.
Na Suzy Luhende, Shinyanga
KANISA la Waadventista wa Sabato (S.D.A) mjini Shinyanga limetoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watu waliojeruhiwa kwenye ajali ya basi la kampuni ya Classic lililokuwa likitokea nchini Uganda kwenda jijini Dare es Salaam nchini Tanzania, ambalo lilianguka Alfajiri ya Juni 2, 2021 na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 20.
Wakikabidhi msaada huo wenye thamani ya Sh. 300,000, baadhi ya viongozi wa kanisa hilo akiwemo mzee wa kanisa, Dk. Ellyson Maeja na Mwinjilisti Amani Tibore wamesema kuwa wameguswa na tukio hilo lililogharimu maisha ya Watanzania na kwamba sehemu ya abiria wa basi hilo walikuwa wanafunzi waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu cha Bugema nchini Uganda kinachomilikiwa na kanisa la Wasabato.
Muonekano wa basi hilo baada ya kupata ajali leo alfajiri
Dk. Maeja amesema kanisa limeona litoe msaada wa vifaa tiba na dawa ili viwasaidie majeruhi waliolazwa hospitalini hapo, ambapo wanaoendelea vizuri wameruhusiwa na kwamba wamewakodia hoteli kwa ajili ya kupumzika na sasa wanafanya taratibu za kusafirisha miili ya marehemu watatu kwenda Zanzibar.
Amevitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni monitol 12 Bottle, Surgical Gloves 100, Examination Glove 100,Canula 24g,Canula 20, Canula 16g, Cotton Woul 5 na Bandeji dozi 10.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa Afya (SRRH) mkoa wa Shinyanga, Iveta Mtesigwa amesema kuwa miongoni mwa majeruhi 20 waliopokelewa, wanne wameumia kichwani na wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi.
Mtesigwa amesema amelishukuru kanisa hilo kwa kutoa vifaa hivyo kwani baadhi ya vifaa hivyo vilikuwa vimeisha kwahiyo msaada huo utaongeza ufanisi katika matibabu ya wagonjwa hao, huku akizibisha taasisi na wadau wengine watakaoguswa kusaidia.
Mzee wa Kanisa la Wasabato mjini Shinyanga, Dkt. Ellyson Maeja (wa pili kushoto) na Mwinjilisti wa kanisa hilo, Amani Tibore (kushoto) wakikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa wawakilishi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga vilivyotolewa na kanisa la Sabato mjini Shinyanga.