KATIBU WA UVCCM SHINYANGA AWATAKA VIONGOZI WA UMOJA HUO KWENYE MATAWI, KATA NA WILAYA KUACHA MAKUNDI

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini akizungumza na makatibu tawi na kuwataka kuzingatia ilani ya chama na fursa zilizopo.

Na Suzy Luhenda, Shinyanga
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)  mkoa wa Shinyanga, Muksini Zikatim amewataka makatibu wa matawi, kata na wilaya kuachana na makundi ambayo hayakijengi chama badala yake wawe na makundi yenye kuleta maendeleo ndani ya umoja huo.

Zikatim ametoa rai hiyo leo katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga wakati akitoa mafunzo kwa makatibu tawi kata wa jumuia ya vijana na makatibu kata wa CCM kutoka wilaya ya Shinyanga mjini, kwa lengo la maandalizi ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na jumuia zake.

Amewataka vijana kuachana na makundi yasiyo na faida kwenye chama badala yake wakijenge chama na jumuia zake na kujipanga vizuri katika kikiimarisha ili kuwa na uchaguzi wa amani ifikapo mwaka 2022.

"Nawaomba sana viongozi wote wa jumuia yetu ya UVCCM msijiingize kwenye migogoro isiyowahusu, mnatakiwa muwe na vikundi vya kuleta mafanikio ndani ya chama cha mapinduzi CCM, huku mkifuata kanuni na taratibu za kazi zenu mlizopangiwa kufanya," amesema Zikatim.

Pia amewataka makatibu wote wa matawi na kata wa umoja huo washirikiane na kufanya mikutano ya ndani ili kuwaweka vijana wote vizuri, huku wakihakikisha matawi yote yanakuwa na wanachama 100 ama zaidi, hivyo kila matawi kama wanachama wake hawajatimia wakahamasishe waweze kujiunga kwenye jumuia ya vijana.

Aidha Zikatim aliwataka viongozi na wanachama wote kuacha kumuita Mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu badala yake wampe heshima yake wamuite Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani jina la mama anaitwa akiwa nyumbani kwake.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Agnes Bashem amewataka makatibu hao kwenda kuelimisha vijana na kufuata ilani ya chama na fursa za chama, kwani wakifanya hivyo vijana wataongezeka na chama kitaendelea kuimalika zaidi.

"Vijana acheni kujiingiza kwenye makundi ya watu wanaojiita ni wazoefu ambao wanaendekeza makundi na migogoro ya zaidi ya miaka 20 hivyo msiipandilie magari katikati maana hamjui waliianzishaje nyie hamasisheni vijana wenzenu chapeni kazi na mshirikiane, wale wanaojifanya wazoefu hawana chochote wasiwaharibu nyinyi vijana," amesisitiza Bashem.

"Na sasa tumeazimia tuwe tunatoa zawadi kwa makatibu ambao wanafanya vizuri kwenye matawi yao kwenye kata zao, ili kuwafanya waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi," amesema Bashem.

Naye Katibu Tawi la Mwamagunguli Kata ya Kolandoto, Frank Joseph amesema wamefurahishwa na viongozi kwa kuanza kuwapa mafunzo kwani walikuwa hawapati mafunzo makatibu wengi wa matawi walikuwa hawajui kazi yao hivyo sasa wameelewa na wataendelea kuelewa kutokana na ziara zinazoendelea za viongozi wa chama na vijana.
Katibu wa UVCCM mkoa wa Shinyanga, Muksini Zikatim (Katikati) akiwaelimisha makatibu tawi na kata ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.
Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga, Rafael Nyandi (kushoto) akizungumza baada ya mafunzo ya makatibu tawi na kata



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464