KUELEKEA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA, WADAU HAKI ZA WATOTO SHINYANGA WASHAURI MALEZI NA MAKUZI BORA KUPEWA KIPAUMBELE

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yatakayofanyika Juni 16, mwaka huu

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
Juni 16 ya kila mwaka,Tanzania huungana na nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho haya ni tukio la mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na askari wa utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini Juni 16, 1976.

Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Tutekeleze Ajenda 2040: Kwa Afrika Inayolinda Haki za Mtoto’, ambapo kupitia taarifa ya wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Juni 9, mwaka huu, Serikali imetoa rai kwa jamii na familia kuwa jukumu la kuwalea na kuwalinda watoto ni la familia na jamii kwa ujumla na kwamba makao ni mahali ambapo mtoto hupelekwa kupata huduma kwa muda maalum na uamuzi wa kumpeleka mtoto kwenye makao iwe ni hatua ya mwisho baada ya njia nyingine zote za kumsaidia kushindikana.

Kuelekea maadhimisho hayo, Wadau mbalimbali wa masuala ya Watoto mkoani Shinyanga zikiwemo asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na kutetea haki za Watoto, wakizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa nyakati toafuti wameeleza kuwa bado suala la malezi na makuzi ya watoto mkoani humo lina changamoto kutokana na wazazi kujisahau na kutofanya ufuatiliaji, hali inayopelekea baadhi ya madhira kuwakumba watoto na kupoteza haki zao.
Meneja Miradi wa shirika la ICS, Sabrina Majikata

Mmoja wa wadau hao ni Shirika la Investing in Children and their Societies (ICS) linalotekeleza miradi ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na Watoto mkoani Shinyanga na Simiyu kwa kufanya majadiliano na wazazi juu ya stadi za malezi, kuendesha mafunzo kwa wawezeshaji jamii, kuwafikia wanaume (wababa) ili washiriki kikamilifu kwenye malezi ya watoto na familia, ambapo Meneja Miradi wa shirika hilo, Sabrina Majikata, amesema kuwa wanafanya hayo kwa lengo la kujenga na kuimarisha mazingira salama ya mtoto shuleni na nyumbani.

Sabrina ameeleza kuwa changamoto ya malezi inasababishwa na ufuatiliaji hafifu kwa wazazi ama walezi kutokana na wazazi kujisahau na kutotoa usaidizi kwa watoto, huku akisema kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja.

Meneja huyo amebainisha kuwa kupitia programu ya malezi na makuzi bora ya mtoto wamewafikia wawezeshaji 100 ngazi ya jamii katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga tangu mwaka 2015, wazazi zaidi ya 10,000 na watoto zaidi ya 5,000 wamefikiwa moja kwa moja shuleni na mabaraza ya watoto ngazi ya jamii.

“Mila na desturi katika jamii zimekuwa kikwazo katika malezi na makuzi na ustawi wa mtoto kwani sehemu kubwa ya wazazi na walezi hawana stadi za malezi. Jamii ibadilike hasa mila na desturi, kuna mambo tunapaswa kuachana nayo kwa sababu hayana afya na maslahi kwa Watoto.

“ICS tunajivunia kuwekeza kwa watoto na kuwajengea uwezo wa kuelewa namna ya kujilinda na kuwaelewesha wazazi kupitia mabaraza ya ulinzi wa mtoto na pia tumeshiriki katika uandaaji wa mipango ya serikali katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto,” amesema.
Afisa Mradi wa Ukatili wa Kijinsia kutoka Asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Jane Kashumba

Mbali na kushauri Serikali kuweka kwenye mitaala ya elimu ajenda na somo la ukatili wa kijinsia ili kuwafundisha watoto na jamii kwa ujumla kujua habari za kijinsia, jinsi ya kujikinga na wapi pa kwenda kupata huduma, Afisa Mradi wa Ukatili wa Kijinsia kutoka Asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Jane Kashumba amesema kuwa wazazi ni kama wametelekeza watoto bila kutambua kama wamewatelekeza, hii inatokana na wazazi kutofanya ufuatiliaji hadi pale linapotokea tatizo na limeshaleta athari kwa mtoto ndipo wanagutuka.

Dk. Kashumba ameshauri jamii kurudi kwenye tamaduni zao za malezi na makuzi na kujenga mahusiano mazuri na watoto, kwani kwa sasa wazazi na walezi wengi wanafikiri mtoto akishafika sekondari basi anajitegemea.

“Tuache usasa usio na maana ambao unawaharibu na kuwapotosha ubongo watoto, watoto wanaachwa huru zaidi na kulelewa na wafanyakazi wa nyumbani ambao huwafundisha mambo yasiyo sahihi, kwahiyo tusiache Watoto wajilee wenyewe tutawaweka kwenye hatari za maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo Virusi Vya Ukimwi (VVU),” ameshauri.
Afisa Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI), Paskalia Mbugani

Kwa upande wao Shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI) linalofanya shughuli zake katika halmashauri tatu za Manispaa ya Shinyanga, wilaya ya Kishapu na Shinyanga kupitia miradi iliyojikita kwenye elimu, afya, kijamii (ukatili wa kijinsia na watoto), linafanya miradi inayolenga kubadilisha tabia kwa wanawake na watoto watambue haki zao na namna ya kuzidai.

Akizungumzia suala la malezi kwa Watoto, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Thubutu Africa Iniatives (TAI), Rehema Katabi, ameshauri wazazi kuwa na utayari wa kuwa wazazi na walezi kwani mahusiano na mtoto yanaanza tangu mtoto anapotafutwa, huku akisisitiza watu kutokimbilia kuzaa bila kujipanga kuwa walezi na kushauri jamii kuwekeza zaidi kwa watoto ili kujenga jamii ijayo na kuwashirikisha kwenye vitu chanya na siyo hasi.

“Pia tukubali kujifunza dunia iko wazi, tuachane na tamaduni kandamizi zinazofifisha ustawi wa mtoto. Na tofauti (migogoro) za wazazi zisifanye mtoto kukosa haki zake,” ameshauri.
Afisa Miradi wa GCI, Lucy Mosha

Shirika la Green Community Initiatives (GCI) linalofanya shughuli zake katika manispaa ya Shinyanga kupitia mradi wake wa ‘Sauti ya Mwanamke na Mtoto’ ambao umewafikia watu 259 wakiwemo wanaume 128, wanawake 73 na Watoto 58 kwa kuwajengea uwezo juu ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, limeshauri na Serikali kuboresha huduma ama kuwatengea huduma watoto wenye usonji ili nao wapate ustawi bora na haki katika jamii.

Afisa Miradi wa Shirika hilo, Lucy Mosha, amesema kuwa katika jamii za kiafrika hususan Shinyanga baadhi ya watoto ndiyo wanaojitafutia kipato na kujilea, hivyo kujiingiza katika tabia hatarishi, ambapo GCI hufanya uhamasishaji, kutoa elimu ya suala la uzazi na utayari wake, malezi na makuzi bora ili kuepusha wimbi la watoto wa mitaani.
Mkurugenzi wa WAYDS, Charles Deogratias (kushoto) akizungumza na mwandishi wetu

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Women and Youth Development Solution (WAYDS), Charles Deogratias amesema kuwa mtoto wa Afrika hususan Shinyanga bado yuko nyuma kutokana na kuendelea kukabiliwa na changamoto za ukatili, unyanyasaji na ndoa za utotoni, hivyo akatoa wito wa kuitumia siku ya mtoto wa Afrika kupata suluhisho la kuzitatua changamoto zinazowakumba.

“Ili tuweze kupata maendeleo tunahitaji kushirikiana bila kuminya haki za watoto, vijana, wanawake ama watu wenye ulemavu. Tupige hatua kwa pamoja kama jamii bila kuacha kundi lolote nyuma na kubeba lingine,” ametoa wito.

Deogratias amesema shirika lake linalenga katika malezi na ustawi wa mtoto, haki za wanawake na changamoto za vijana ili kuangalia fursa zitakazowasaidia kuinuka, ambapo hutumia mbinu ya ushirikishwaji jamii kwa kushirikiana na vikundi na mabalozi mbalimbali kwa kuiwezesha jamii.

Kwa upande wa Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amesema katika Katika kuimarisha malezi ya familia, Serikali imeendelea kushughulikia mashauri na matunzo ya watoto ambapo jumla mashauri 27,806 katika kipindi cha mwaka 2019/2020, huku idadi ya watoto wanaopata malezi ya kambo ikiongezeka kutoka watoto 85 mwaka 2015 hadi watoto 342 mwaka 2020.

Serikali pia imeendelea kuratibu vituo vya kulelea watoto wadogo mchana ambapo vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo 744 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 1,543 mwaka 2020. Vilevile, Serikali imeendelea kuratibu makao ya watoto walio katika mazingira hatarishi na hadi Disemba, 2020 jumla ya makao ya watoto 178 yamesajiliwa na watoto 351 wanalelewa katika makao hayo.

Pamoja na juhudi hizo Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu malezi chanya kwa Jamii kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii ambapo hadi kufikia Disemba, 2020 jumla ya Maafisa Maendeleo ya Jamii 7,445 walipata mafunzo na wazazi 110,805, ambapo maafisa hao wamefanikiwa kuanzisha jumla ya vikundi 3,963 vya kuhamasisha na uelimisha malezi chanya katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza elimu ya malezi na kukuza uwajibikaji kwa wazazi na walezi katika familia.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464