Mabinti wanaounda kikundi cha Upendo Klabu katika kijiji cha Malito Kata ya Shilela halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, ambao walipata mimba wakiwa chini ya umri wa miaka 18 kisha wakawezesha maarifa na stadi za maisha wakionyesha baadhi ya nguo walizoshona.
Na Damian Masyenene, Kahama
Zaidi ya wasichana 89 ambao walikatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni katika kata za Bugarama na Shilela halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, wamewezeshwa kiuchumi kwa kupatiwa mafunzo ya stadi za maisha na ujasiriamali ili kuwasaidia kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyokutana navyo katika jamii wanazotoka.
Hayo yameelezwa jana Juni 2, 2021 wakati wa ziara ya kupitia maendeleo ya utoaji wa usawa kwa wanawake na wasichana katika halmashauri ya Msalala unaotekelezwa kupitia Programu ya pamoja ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNFPA na UN Women, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA).
Ziara hiyo ikiongozwa na Naibu Mkuu wa Shirika la UNFPA Tanzania, Dk. Wilfred Ochan na wawakilishi kutoka UN Women, UNFPA, KOICA, mkoa na serikali za mitaa walitembelea maeneo yaliyochaguliwa ya mradi katika halmashauri hiyo na kukutana na vikundi vya wasichana walionufaika, kamati za kupinga ukatili kwa wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Vituo vya taarifa na maarifa na wasaidizi wa kisheria kwenye kata za Bugarama, Lunguya na Shilela katika halmashauri hiyo.
Mmoja wa mabinti katika kikundi cha Upendo Group chenye wasichana 11 kilichonufaika na mafunzo ya stadi za kazi katika Kijiji cha Malito kata ya Shilela, Veronica Mhalule (19) ameeleza kuwa akiwa kidato cha pili mwaka 2019 alilazimika kukatiza masomo yake baada ya baba yake kumkataza kwenda shule bila sababu yoyote, hatimaye akashawishika na kubeba mimba ya mwanaume ambaye hamfahamu wala kujua mahali aliko hadi sasa na amemtelekeza.
Ameongeza kwa kusema kuwa alijifungua mwaka jana na mtoto alipofikisha miezi mitano ndipo likaja Shirika la KIWOHEDE likitafuta mabinti kwa ajili ya kuwapeleka katika chou cha Maendeleo ya watu kuhudhuria mafunzo ya ufundi na elimu ya stadi za maisha, lakini kutokana na kuwa na mtoto ilibidi yeye na wenzake walio na Watoto watafutiwe mwalimu awafundishe hapo hapo kijijini kwao mafunzo ya ushonaji nguo ambayo wamehitimu sasa.
“Tumejifunza ujasiriamali tunashona nguo na kikundi chetu kina wasichana 11 waliozalishwa katika umri mdogo, kwa sasa tunajiamini na mafunzo haya yamenisaidia katika maisha yang una ni namlea mwanangu. Wito wangu kwa wazazi wahamasishwe kutowakatisha tamaa Watoto wao na kuwachisha masomo, lakini pia wanaowarubuni Watoto wa kike na kuwapa mimba wachukuliwe hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine,” alisisitiza.
Naye Halima Ramadhani ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Mabingwa Klabu kilichopo katika kata ya Bugarama ambacho kina wasichana 78 waliohitimu mafunzo ya ushonaji, umeme, huduma za steshenari na udereva, amesema kuwa alijifungua akiwa na miaka 17 na kwamba alilazimika kumuacha nyumbani mtoto wake akiwa na miezi sit ana kuhudhuria mafunzo hayo katika chou cha Mwakata kupitia ufadhili wa KIWOHEDE.
“Tumetoka chuoni tumepata vitu tofauti na sasa kila msichana amejiwezesha kiuchumi na wengine wameajiriwa. Kikubwa hapa tunaomba kuwezeshwa kupata fursa kwenda kwenye taasisi kubwa kujifunza Zaidi kwa sababu mazingira yetu huku vijijini hayana nyenzo za kutupatia fursa kubwa,” amesema.
Naye Veronica Charles kutoka Kikundi cha Mabingwa Klabu amesema kuwa baada ya kuhitimu mafundo hayo alipambana akakodi cherehani na sasa ameweka malengo ya kununua yak wake na kuweka mfano katika eneo lake kwa kufanya vizuri na kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya Watoto wa kike, huku Levina Paul akieleza kuwa baada ya mafunzo hayo hawadharauliki tena katika familia zao na sasa wanaheshimika na wanatoa msaada na kusaidia uchumi kwenye familia zao.
Katika kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa rasmi na kunufaika na mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jinsia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Erasto Ching’oro aliuelekeza uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na halmashauri ya Msalala na idara ya maendeleo ya jamii kuweka utaratibu mzuri utakaovisaidia vikundi hivyo na kuvirasimisha.
“Bahati nzuri haw ani wanawake na ni vijana kwahiyo wanaweza kunufaika na asilimia nne za vijana nan ne za wasichan/wanawake, kwahiyo maofisa maendeleo ya jamii walichukue kama zoezi kuweka utaratibu mzuri utakaowasaidia,” alielekeza.
Akipokea maelekezo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale ambaye pia ni Mratibu wa mkoa huo wa kamati ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na Watoto (MTAKUWWA), aliwaagiza maofisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa vikundi hivyo vinasajiliwa ifikapo Juni 30, mwaka huu na Mkurugenzi wa halmashauri afanye jitihada ili waingizwe kwenye utaratibu wa kupata mikopo.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Wanawake na Watoto la KIWOHEDE, Justa Mwaituka ambalo lilisimamia vikundi hivyo kupata mafunzo ya stadi za Maisha, alisema walifanya mchakato wa utambuzi kwa wasichana hao na wengine walikuwa na wameolewa na wanaume wao waliwapa ruhusa wapate mafunzo hayo, ambapo ameeleza kuwa katika kata ya Shilela walihitaji wasichana 75 kwa ajili ya kuwapa maarifa na stadi za kazi na wanahudhuria kwenye kipindi cha redio kuwapa uzoefu wenzao ikiwemo madhira waliyoyapitia.
“Wamepata mafunzo ambayo tayari tumeanza kuona kazi zao na tunahitaji kuendelea kuwatia moyo ili wazidi kujiamini Zaidi na kazi zao, kwenye mradi tulihitaji wasichana 75 kwa ajili ya kuwapa maarifa na stadi za kazi na walijitokeza wengi Zaidi ya uwezio wetu,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto UN Women -Tanzania, Lucy Tesha amesema ni muhimu kuendelea kuelimisha ili jamii ielimike zaidi na kuzikabili changamoto zinazowanyanyasa wasichana kwani kutoshirikishwa kwenye fursa za kiuchumi hurudisha nyuma pato la taifa, hivyo akahimiza jamii kuzingatia elimu kwa Watoto wote kwa sababu ndiyo msingi ambao utawapa mabinti kuona fursa zilizopo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la UNFPA Kanda ya Ziwa, Amir Batenga amesema kuwa moja ya kazi wanazofanya ni kuelimisha wazazi kutambua haki ya mtoto kwenda shule na moja ya malengo katika mradi huo ni kuhakikisha kila mtoto anayepaswa kwenda shule basi anakwenda.
Ambapo, amewataka zwzazi kuhakikisha wanawapeleka shule Watoto wao na wawe wajumbe kwa wenzao ili watambue haki hiyo kwa Watoto, pia kamati za MTAKUWWA, idara ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kutembelea mara kwa mara maeneo yenye mradi na kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kuchukua hatua pale ambapo kuna uzembe.
Mwenyekiti Kamati ya MTAKUWWA ya Kijiji cha Bunango Kata ya Bugarama, Masanja Jeremia amesema baadhi ya wazazi huwaachisha watoto shule ili wafanye kazi za nyumbani ikiwemo kuchunga ng’ombe, watoto wenye ulemavu kutopelekwa shule na Watoto wa kike wanaomaliza darasa la saba hawaendelezwi , ambapo kamati hiyo inaewaelimisha na kuwahamasisha wanajamii kuheshimu haki za Watoto na kutoa ushauri kwa familia kuwapa kipaumbele ili wapelekwe shule.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameshauri kupewa vitambulisho ili kutambulika kwenye jamii na kuondoa kero na usumbufu wanapofika kwenye jamii kutoa elimu na ushauri, ili kufanya kazi yao kwa uhuru na ufanisi Zaidi, kwani wakati mwingine wanapokwenda kuelimisha wanaonekana kama maadui ama watengenezaji wa uadui katika familia baina ya wazazi na Watoto ama wana ndoa.
Mmoja wa wajumbe hao, Steven Elias amesema kuwa Watoto 10 hadi 20 wanaosoma hawajaenda shule lakini mzazi hafanyi ufuatiliaji wala kujisumbua kwa sababu anakuwa anafurahi kwa sababu anajua atapata mahari, pia wanapata kuanzia tano za ndoa akina baba kutelekeza familia ama kuoa mwanamke mwingine, zipo pia kesi za umiliki wa mali hasa wakati wa mavuno baba anafanya maamuzi ya matumizi ya fedha tofauti na matakwa ya familia na kuzua migogoro kwenye familia.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya MAKUWWA kata ya Lunguya, Nyakwesi Gunya wamekuwa wakitumia mikutano ya kuelimisha jamii kila Kijiji na kupokea taarifa za matukio ya ukatili na kuzifanyia kazi na kuzipa rufaa, ambapo jumla ya kesi nne zikiwemo za ubakaji na kupigwa Watoto zimefanyiwa kazi katika miezi mitatu iliyopita.
Naye Katibu Msaidizi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kijiji cha Malito Kata ya Shilela, Joseph Mbunge amesema kuwa wamekuwa wakiwahamaisha wazazi kuwapeleka Watoto shule na kupunguza tatizo la utoro ambapo wanafunzi 127 walifuatiliwa na kurejeshwa shuleni, kuibua matukio ya mimba za utotoni na kuyaripoti kwenye mamlaka zikiwemo kesi mbili za mimba kwa mwanafunzi wa darasa la tano na kidato cha tatu.
“Ukosefu wa hosteli ya wasichana katika shule ya sekondari unachangia mimba za utotoni, wazazi kutengana husababisha Watoto wa kike kubebeshwa majukumu mazito, wazazi kutojua umuhimu wa elimu. Kwa sasa mipango yetu ni vyumba vya siri vya kuzungumza na Watoto kuhusu ukatili katika shule tano za msingi na moja ya sekondari katika kata yet una kuhamasisha jamii kuwa na vituo vingi vya taarifa na maarifa,” amesema.
Programu ya Pamoja ya miaka mitatu ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNFPA na UNWomen, iliyotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida na Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga, inalenga kuendeleza usawa wa kijinsia na kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wa vijijini katika wilaya hizo hawaachwi nyuma, ambapo kupitia makubaliano ya KOICA, UNFPA na UNWomen zinajumuisha nguvu zao za kipekee kusaidia uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi wa wanawake na wasichana ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa wanawake kumiliki hati miliki za ardhi na kwa wakulima wadogo.
Naibu Mkuu wa Shirika la UNFPA Tanzania, Dk. Wilfred Ochan (wa pili kutoka Kulia) akishauri mambo mbalimbali katika kikao cha kamati ya MTAKUWWA na wasaidizi wa kisheria kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala
Wawakilishi wa mashirika ya UNFPA, UN Women, KOICA, Kiwohede, TAMWA, TGNP, C-SEMA wakibadilishana uzoefu na wasaidizi wa kisheria katika kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala kutoka shirika la DEMAO (Destiny Makers Organization)
Mwakilishi wa Shirika la UNFPA Kanda ya Ziwa, Amir Batenga (kushoto) akitoa tafsiri ya mawasilisho mbalimbali kutoka kamati za MTAKUWWA na wasaidizi wa kisheria kwa Naibu Mkuu wa shirika hilo, Dk. Wilfred Ochan (katikati)
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA katika kata ya Bugarama wakichangia mjadala kwenye kikao hicho
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya Mtakuwwa kata ya Bugarama wakifuatilia kikao hicho
Wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA kata ya Bugarama wakisikiliza uwasilishaji wa taarifa ya kamati yao mbele ya wawakilishi wa mashirika ya UNFPA na UN Women (hawapo pichani)
Mwenyekiti wa kamati ya MTAKUWWA kata ya Bugarama, Masanja Joseph akiwasilisha taarifa ya kamati yake
Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka shirika la msaada wa kisheria la DEMAO, Rahel Paul akiwasilisha taarifa ya shirika hilo
Baadhi ya wasichana wanaounda kikundi cha Mabingwa Klabu katika kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala ambao wamewezeshwa ujuzi na stadi za maisha ikiwemo ufundi nguo, umeme, udereva na huduma za steshenari ili kujikwamua kiuchumi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Baadhi ya wanakikundi wanaounda kikundi cha ujasiriamali katika kata ya Lunguya wakiwa katika shamba darasa ambalo wanalima nyanya, hoho na pasheni baada ya kuwezeshwa na Shirika la TAHA kwa ufadhili wa KOICA na UNFPA
Muonekano wa shamba darasa hilo
Mwakilishi kutoka TAHA, akiwaelezea wataalam kutoka KOICA, UNFPA, UN Women namna ambavyo shamba darasa hili litawanufaisha wanawake wajasiriamali katika kata ya Lunguya
Wataalam kutoka UNFPA, UN Women, KOICA, Kiwohede, TGNP, C-SEMA na TAMWA wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha wajasiriamali katika shamba darasa la nyanya, hoho na psheni katika kata ya Lunguya halmashauri ya Msalala
Mabinti wanaounda kikundi cha UPENDO CLUB katika kijiji cha Malito kata ya Shilela halmashauri ya Msalala ambao walikatiza masomo yao kutokana na mimba za utotoni, wakionyesha bidhaa walizozitengeneza baada ya kuwezeshwa maarifa na stadi za maisha
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Veronica Mhalule akiwaongoza wenzake kunadi bidhaa zao mbele ya viongozi wa mashirika ya UNFPA, UN Women na wawakilishi wa wizara
Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea haki za Wanawake na Watoto la KIWOHEDE, Justa Mwaituka akieleza namna walivyowawezesha kupata ujuzi wa stadi za maisha zaidi ya wasichana 70 katika kata ya Shilela, wakati wa mkutano na kituo cha taarifa na maarifa na kikundi cha Upendo Klabu katika kijiji cha Malito
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Malito kata ya Shilela halmashauri ya Msalala wakifuatilia kikao hicho