MAKALA: MABINTI WAELEZA WALIVYOBEBESHWA MIMBA UTOTONI, SASA UWEZESHAJI KIUCHUMI NA AFYA YA UZAZI VYAWAPA DIRA

Kikundi cha wasichana 75 wanaounda klabu ya Mabingwa katika kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ambao wamewezeshwa mafunzo ya stadi za maisha katika ushonaji, umeme, udereva na kazi za steshenari baada ya kukatishwa masomo kwa mimba za utotoni na kutoendelezwa kielimu.

Na Damian Masyenene, Shinyanga
BAADHI ya simulizi za Watoto wengi wa kike waliobeba mimba za utotoni mkoani Shinyanga zinataja chanzo kuwa ni kukatishwa masomo na wazazi kwa lengo la kuozeshwa ili kupata mali, wengine hata wakifaulu hawaendelezwi lakini pia mila na Imani potofu za jamii juu ya watoto wa kike na wanawake kwa ujumla.

Hali hii iliwakuta Halima Ramadhani, Veronica Mhalule, Veronica Charles, Levina Paul na Leticia Ally ambao ni miongoni mwa wasichana 89 kutoka Kata za Bugarama na Shilela katika Halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambao walikatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kubeba mimba chini ya umri wa miaka 18, lakini sasa wamewezeshwa kiuchumi kwa kupata maarifa na ujuzi wa stadi za Maisha pamoja na afya ya uzazi kwa ajili ya kupanga uzazi na kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Simulizi zao
Veronica Mhalule (19) ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Club chenye wasichana 11 kilichonufaika na mafunzo ya stadi za maisha katika Kijiji cha Malito kata ya Shilela, alibainisha kuwa akiwa kidato cha pili mwaka 2019 alilazimika kukatiza masomo yake baada ya baba yake kumkataza kwenda shule bila sababu yoyote, hatimaye akashawishika na kubeba mimba ya mwanaume ambaye hamfahamu wala kujua mahali aliko hadi sasa na amemtelekeza.

Ameongeza kwa kusema kuwa alijifungua mwaka jana na mtoto alipofikisha miezi mitano ndipo likaja Shirika la KIWOHEDE likitafuta mabinti kwa ajili ya kuwapeleka katika chou cha Maendeleo ya watu kuhudhuria mafunzo ya ufundi na elimu ya stadi za maisha, lakini kutokana na kuwa na mtoto ilibidi yeye na wenzake walio na Watoto watafutiwe mwalimu awafundishe hapo hapo kijijini kwao mafunzo ya ushonaji nguo ambayo wamehitimu sasa.

“Kikundi chetu tupo wasichana 11 tuliozaa katika umri mdogo, kwa sasa tunajiamini na mafunzo haya yamenisaidia katika maisha yangu na ninamlea mwanangu. Wito wangu kwa wazazi wahamasishwe kutowakatisha tamaa watoto wao na kuwaachisha masomo, lakini pia wanaowarubuni watoto wa kike na kuwapa mimba wachukuliwe hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine,” alisisitiza.

Naye Halima Ramadhani ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Mabingwa Klabu kilichopo kata ya Bugarama ambacho kina wasichana 78 waliohitimu mafunzo ya ushonaji, umeme, huduma za steshenari na udereva, amesema kuwa alijifungua akiwa na miaka 17 na kwamba alilazimika kumuacha nyumbani mtoto wake akiwa na miezi sita na kuhudhuria mafunzo hayo katika chuo cha Mwakata kupitia ufadhili wa KIWOHEDE.

“Tumetoka chuoni tumepata vitu tofauti na sasa kila msichana amejiwezesha kiuchumi na wengine wameajiriwa. Tulifundishwa namna ya kutumia uzazi wa mpango, hivyo nafikiria wakati ujao nijipange vizuri hata nikitaka kuzaa niwe nimejiandaa.

“Mafunzo haya ya kujiwezesha kiuchumi yanatujenga kuacha utegemezi unaotuweka kwenye vishawishi vya ngono na mimba zisizotarajiwa,” alisema.

Naye Veronica Charles (20) kutoka Kikundi cha Mabingwa Klabu amesema kuwa baada ya kuhitimu mafundo hayo alipambana akakodi cherehani na sasa ameweka malengo ya kununua ya kwake na kuweka mfano katika eneo lake kwa kufanya vizuri na kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya Watoto wa kike, ambapo ameeleza kuwa elimu ya afya ya uzazi imemjenga na kutambua namna ya kuzuia mimba za utotoni na kujikinga na mimba zisizo tarajiwa na za chini ya umri.

“Tulifunzwa njia nyingi za uzazi wa mpango, kwahiyo nitatumia elimu hiyo kuwa na mafanikio ndani ya mahusiano ili tusiwe na utegemezi tutakapopata Watoto,” alieleza.

Naye Leticia Ally (17) mwanakikundi wa Mabingwa Klabu ambaye aliishia darasa la saba na kunufaika na mafunzo hayo ya uwezeshaji kiuchumi katika fani ya ushonaji yanayotekelezwa kwa program ya Pamoja na mashirika ya UNFPA na Un Women kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), alisema kuwa Watoto wengi wa kike katika maeneo ya vijijini wanarubunika kwa fedha kutokana na mazingira magumu na hali duni ya Maisha katika familia zao, hivyo mafunzo hayo yamempa mwanga na dira ambayo itamsaidia kutorubunika tena.

Naye Levina Paul alieleza kuwa baada ya mafunzo hayo hawadharauliki tena katika familia zao na sasa wanaheshimika na wanatoa msaada na kusaidia uchumi kwenye familia zao.

Kikundi cha wasichana 11 cha Upendo Klabu katika kijiji cha Malito Kata ya Shilela halmashauri ya Msalala wilayani Kahama kilichowezeshwa stadi za maisha na elimu ya afya ya uzazi kikionyesha bidhaa walizozalisha baada ya mafunzo

Serikali yawapa matumaini
Vikundi hivyo viwili vinajumuisha jumla ya wasichana 89 ambao ni 75 wa Mabingwa Klabu katika kata ya Bugarama na 11 wa Upendo Klabu katika kata ya Shilela, ambapo Serikali imeonyesha matumaini kwa mabinti hao ili kuwapa fursa kubwa na kutanua ujuzi na mitaji kwenye shughuli zao.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jinsia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Erasto Ching’oro aliuelekeza uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na halmashauri ya Msalala na idara ya maendeleo ya jamii kuweka utaratibu mzuri utakaovisaidia vikundi hivyo na kuvirasimisha.

“Bahati nzuri hawa ni wanawake na ni vijana kwahiyo wanaweza kunufaika na asilimia nne za vijana nan ne za wasichan/wanawake, kwahiyo maofisa maendeleo ya jamii walichukue kama zoezi kuweka utaratibu mzuri utakaowasaidia,” alielekeza.

Akipokea maelekezo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale ambaye pia ni Mratibu wa mkoa huo wa kamati ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na Watoto (MTAKUWWA), aliwaagiza maofisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa vikundi hivyo vinasajiliwa ifikapo Juni 30, mwaka huu na Mkurugenzi wa halmashauri afanye jitihada ili waingizwe kwenye utaratibu wa kupata mikopo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Wanawake na Watoto la KIWOHEDE, Justa Mwaituka alisema kuwa mbali na mafunzo hayo ya stadi za Maisha, wasichana hao wamekuwa wakipata nafasi kwenye kipindi cha redio ya Divine FM mjini Kahama kuwapa uzoefu wenzao ikiwemo madhira waliyoyapitia na kuhamasisha ili kuwavutia mabinti wengine.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto UN Women -Tanzania, Lucy Tesha alisema elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa nguvu ndani ya jamii kwa ajili ya kuhamasisha elimu ya Watoto wa kike na kuzikabili changamoto zinazowanyanyasa wasichana kwani kutoshirikishwa kwenye fursa za kiuchumi hurudisha nyuma pato la taifa, hivyo akahimiza jamii kuzingatia elimu kwa Watoto wote kwa.

Naye Mwakilishi wa Shirika la UNFPA Kanda ya Ziwa, Amir Batenga alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanawapeleka shule Watoto wao na wawe wajumbe kwa wenzao ili watambue haki hiyo kwa Watoto, pia kamati za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), idara ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kutembelea mara kwa mara maeneo yenye mradi na kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kuchukua hatua pale ambapo kuna uzembe.

Programu ya Pamoja ya miaka mitatu ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNFPA na UNWomen, iliyotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida na Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga, inalenga kuendeleza usawa wa kijinsia na kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wa vijijini katika wilaya hizo hawaachwi nyuma, ambapo kupitia makubaliano ya KOICA, UNFPA na UNWomen zinajumuisha nguvu zao za kipekee kusaidia uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi wa wanawake na wasichana ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa wanawake kumiliki hati miliki za ardhi.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Wanawake na Watoto la KIWOHEDE, Justa Mwaituka akieleza namna walivyowapa wasichana hao ili kuwaunganisha na mafunzo ya stadi za maisha.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464