Baadhi ya wanafunzi walioshiriki michezo ya Umisseta Manispaa ya Shinyanga
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya mkoa wa Shinyanga yenye jumla ya wachezaji 100 wa michezo mbalimbali waliochaguliwa kuuwakilisha mkoa huo, inaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya michezo hiyo ngazi ya taifa, huku malalamiko yakiibuka juu ya mchakato wa upatikanaji wachezaji hao ukigubikwa na madai ya kuingizwa mamluki wasio wanafunzi.
Tayari timu mbalimbali zitakazowakilisha mkoa huo zipo kambini katika Chuo cha Ualimu SHY COM mjini Shinyanga zikiendelea na mazoezi ya kujinoa kuelekea mashindano ya Umiseta Kitaifa katika mchezo wa Mpira wa wavu, miguu, pete, riadha na mingineyo.
Baadhi ya wanafunzi na walimu walioshiriki michezo hiyo kupata timu zitakazouwakilisha mkoa huo wamedai kuwekwa kwa nguvu wanamichezo wasio wanafunzi (mamluki) huku wanafunzi wenye vipaji wakiachwa makusudi na pia wanafunzi wa kike wa michezo mbalimbali kukatwa majina yao kutoshiriki michezo hiyo kwa kile kinachoelezwa kuwa na ubaguzi na unyanyasaji.
Kwa mujibu wa taarifa na mahojiano yaliyofanywa na Radio Faraja FM imebaini kuwa baadhi ya wachezaji wanaodaiwa kuwa mamluki ni wa timu ya soka ya Mbezi City ambao waliazimwa na Shule ya Sekondari Buluba.
Kocha wa timu hiyo, Tola Mwangonela aliithibitishia Radio Faraja FM kuwa wachezaji wake watatu wameshiriki mashindano hayo ya UMISSETA kupitia shule ya sekondari Buluba na kusema kuwa nafasi hiyo kwao ni fursa.
Mwandishi wetu alizungumza na mmoja wa wachezaji wanaodaiwa kuwa mamluki ambaye aliichezea timu ya shule ya Sekondari Buluba, Emmanuel Peter ambaye alisema kuwa huu ni mwaka wa tatu anashiriki mashindano hayo akiiwakilisha shule hiyo, huku akikiri kuwa ni mchezaji wa timu ya Mbezi City ambayo kati ya wachezaji wake watatu walioombwa kushiriki kwenye michezo hiyo wawili wamechaguliwa kuwakilisha timu za mkoa wa Shinyanga kwenye michezo ya Umisseta ngazi ya taifa mkoani Mtwara.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa baada ya waandishi kufuatilia sakata hilo, mchezaji huyo ametimuliwa kambini baada ya wasimamizi wa michezo hiyo kufuatilia na kubaini kuwa hakuna mchezaji hata mmoja kutoka shule ya Sekondari Buluba aliyefuzu kuitwa timu za mkoa, mchezaji huyo alikiri kuingia kinyemela kwakuwa anaipenda michezo.
Akizungumzia ushindi wa jumla ilioupata halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwenye michezo hiyo na kufafanua baadhi ya madai ya uwepo wa wachezaji mamluki, Mratibu wa UMISSETA Manispaa ya Shinyanga, Edward Mashenene alisema kuwa manispaa hiyo ilifanya maandalizi ya kutosha yaliyoiwezesha kuibuka na ushindi na kwamba madai yanayoendelea ni hisia za wanafunzi ambao hawakuchaguliwa.
Mashenene alisema kuwa miongozo ya michezo hiyo inataka wanafunzi halali na ukibainika kuingiza mamluki unafukuzwa kazi, kwahiyo hakuna mwalimu aliye tayari kupoteza kazi kwa sababu ya mamluki.
Alisisitiza kwa kueleza kuwa wanamichezo wote walioshiriki mashindano ya mwaka huu (2021) wamecheza wanafunzi halali kwa sababu mashindano hayo ni ya wanafunzi, huku akieleza kuwa huenda watu wanahofia tu maumbile makubwa waliyo nayo wanamichezo hao.
"Majina yote yanayoletwa lazima tusibitishe kwa wakuu wa shule kupitia namba za mwanafunzi za shule kwahiyo hakuna ugumu wa kudhibitisha hilo," alisema.
Hata hivyo, taarifa za hivi punde alizozipata mwandishi wetu kutoka kwa waratibu wa mashindano hayo ni kuwa jana Juni 15, 2021 walimnasa mmoja ya washiriki wanaodaiwa kuwa mamluki baada ya kujiridhisha kuwa hawamfahamu na kwamba aliingia kinyemela kambini hapo bila wao kufahamu.
"Uwanjani alikuwa anaonekana wakajua anafanya mazoezi tu, hawakufahamu kama naye pia anakaa kwenye bweni la wanafunzi, lakini muda wa chakula alikuwa hashiriki na wenzake," kimethibitisha chanzo chetu.
Kijana huyo tayari ameomba msamaha kwa walimu wa Shule ya Sekondari Buluba pamoja na waratibu wa mashindano hayo kwa kuwachafulia mashindano yao kwa kujipenyeza kinyemela, huku pia akiomba msaada wa kukuza kipaji chake cha michezo kama itawezekana kwa kuwa anapenda michezo