RC SENGATI, BALOZI BURIANI WAITEMBELEA KAHAMA, WAONYA WATUMISHI WASIOSIKILIZA KERO ZA WANANCHI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (kushoto) akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama leo Juni 9, 2021 wakati wa ziara yake wilayani humo.

Na Shinyanga Press Club Blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo, Balozi Dk. Batilda Buriani leo wamefanya ziara wilayani Kahama na kuzu ngumza na watumishi wa halmashauri tatu za Msalala, Ushetu na manispaa ya Kahama kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Akizungumza mbele ya watumishi hao, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati amewataka watumishi wa Halmashauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama kuacha tabia ya kukaa ofisini wakila kiyoyozi na badala yake watoke na wakatatue kero za wananchi.

Amesema kuwa asilimia 90 ya watumishi wa Halmashauri wanashinda wamekaa ofisini wakila kiyoyozi bila kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi, na kwamba wakati wa ziara yake bango moja la kero ya wananchi litaondoka na mtumishi mmoja.

“Sipo tayari kutumbuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa uzembe wa baadhi ya watumishi wanaoshinda ofisini bila kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kusimamia vyema miradi ya maendeleo wajiandae kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesisitiza RC Sengati.

Hata hivyo alisema, Halmashauri nyingi zimekuwa zikikusanya mapato na kulipana posho na matumizi ya uendeshaji wa ofisi, badala ya kuelekeza fedha asilimia 40 au 60 kwenye miradi ya maendeleo na kwamba fedha za utengaji wa mikopo ya wajasilimali na fedha za lishe kwa watoto Sh.100 yatenge kwa asilimia 100.

Awali akitoa taarifa ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha alisema halmashauri tatu za wilaya hiyo zimefanikiwa kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa vikundi vya ujasiriamali 2017,kiasi cha Sh.Bilioni 1.9 fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya asilimia 10.

Pia Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imetenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje, hekari 500 kwa ajili ya viwanda vidogo, hekari 1650 ujenzi wa viwanda vikubwa na hekari 623 zimepimwa na kutolewa bure kwa vijana ambao wao waliingia gaharama za utengenezaji wa hati tu.

Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Balozi Dk. Batilda Buriani alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba kwa kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyagawa bure kwa wawekezaji wazawa na kuvutia wawekezaji wa nje.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la wazee la Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Wilfredy Bilago alisema kuwa Manispaa ya Kahama ina jumla ya wazee 6,692 na kila mwaka Halmashauri hiyo imekuwa ikitenga fedha kwaajili kuwakatia bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa.

Aliongeza kwa kueleza kuwa mpaka sasa Halmashauri imeshatoa kiasi cha Sh.27.7 Milioni na kuwakatia wazee bima za afya ili kuwaondolea gharama za matibabu wafikapo katika vituo vya afya na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri za Msalala na Ushetu kuinga mfano huo.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Balozi Dk. Batilda Buriani (kushoto) akizungumza katika kikao na watumishi wa halmashauri za manispaa ya Kahama, Msalala na Ushetu leo kwenye ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akizungumza katika kikao hicho
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake leo wilayani humo
Wadau wa maendeleo na mashirika binafsi wakiwa kwenye kikao hicho
Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa kwenye kikao hicho


Picha ya Patrick Mabula
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464