SHINYANGA YAFIKIRIA UTALII, KILIMO CHA ALIZETI KUONGEZA MAPATO, RC SENGATI, RAS BATILDA WAANIKA MIPANGO, WATETA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati na Katibu Tawala wa mkoa huo, Balozi Dk. Batilda Buriani leo wamekutana na waandishi wa habari na kueleza mikakati yao katika kukuza uchumi wa mkoa huo, kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo na mipango kadhaa yenye lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

Viongozi hao ambao ni wapya kwa mkoa huo baada ya kuteuliwa hivi karibuni, Dk. Sengati akichukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack na Balozi Dk. Buriani akichukua nafasi ya Albert Msovela, wameeleza kuwa mkoa wa Shinyanga ni Tajiri kutokana na rasilimali ilizonazo lakini utajiri huo unapaswa kutafsiriwa kwa Maisha bora kwa wananchi, miundombinu Rafiki, elimu bora, upatikanaji sahihi wa dawa na uwekezaji.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga, Balozi Dk. Batilda Buriani amesema kuwa wanafikria kubuni miradi mipya, kuanzisha kilimo cha mkataba cha Alizeti ili kuzalisha mafuta na kuondokana na changamoto ya uhaba wa mafuta nchini na kuboresha sekta ya mifugo na bidhaa zake ili iwe na tija.

Amesema mkoa huo unavyo vivutio vingi ikiwemo hifadhi ya Moyowosi-Kigosi na vingine ambavyo havijatangazwa ipasavyo, hivyo watatumia fursa hiyo kupanua wigo wa kupata mapato na uwekezaji nje ya vyanzo vilivyopo.

“Nimefarijika kuja hapa naona hali ya mazingira imebadilika siyo kame kama zamani na hali ya umaskini imepungua, tutapenda kuhakikisha utajiri na rasilimali vinahakisi hali ya maendeleo ya wananchi. Kwa pamoja tunataka kubadilisha sura na mwonekano wa Shinyanga, tunataka kutumia uzoefu wetu katika maeneo mbalimbali ili kuitangaza na kuipeleka nje Shinyanga na kuvutia uwekezaji.

“Tuna mengi lakini kubwa ni kuhakikisha tunaleta chuo Kikuu na kukaribisha taasisi za kimataifa ili tuifanye Kahama kuwa jiji. Kwenye afya tunataka kupunguza maambukizi ya Ukimwi, kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa na huduma kwa Wazee, upatikanaji wa mikopo ya silimia 10 kwa akina mama, vijana na Walemavu kwenye halmashauri tutasimamia na kutengeneza miradi endelevu,” ameeleza.

Naye Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Philemon Sengati amesema kuwa Watanzania wakiwemo waandishi wa habari ni watu waadilifu, waadilifu na wenye nidhamu wanaolitakia taifa lao maendeleo na kwamba rasilimali za mkoa huo kwenye Madini, Mifugo, Kilimo na mkao wa biashara na uwekezaji vinaridhisha kwa kiasi kikubwa lakini vinatakiwa kuakisi utajiri huo na ubora wa maisha ya watu wake hasa walioko pembeni, hivyo hilo litakuwa kipaumbele cha mkoa kutafsiri huo utajiri katika maisha ya wana Shinyanga.

“Tunataka kupunguza Vifo vya akina amama, kuongeza kiwango cha elimu, uchumi wa mtu mmoja mmoja upande, miundombinu ijengwe kila mahali. Niombe Wanahabari mtupatie ushirikiano kwa pamoja tuweke kumbukumbu kwa watu wetu kwa kuweka alama chanya katika mkoa wetu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru, amewashukuru viongozi hao kwa kuonyesha matumaini makubwa kwa waandishi wa habari, ambapo amewaomba kutengeneza mazingira Rafiki kwa Wanahabari katika kutangaza shughuli mbalimbali za mkoa huo.

Naye Mwakilishi wa Kituo cha Faraja FM, Simeo Makoba, ameuomba uongozi wa mkoa huo kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati sahihi katika idara mbalimbali kwa kuwashirikisha waandishi wa habari ili kuzifikia azma na malengo hayorifa kufikia malengo, huku akishauri vyombo vyote vya habari kushiriki kwenye ujenzi wa mkoa huo bila kubaguliwa kwa ukubwa ama udogo wake.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akizungumza katika kikao chake na waandishi wa habari ofisini kwake leo
Waandishi wa habari wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati wakati wa kikao chao leo ofisini kwake
Waandishi wa habari wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (hayupo pichani) wakati wa kikao chao leo ofisini kwake
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Balozi Dk. Batilda Buriani (kushoto) akizungumza wakati wa kikao na waandishi wa habari ofisini kwa mkuu wa mkoa huo, Dk. Philemon Sengati (kulia) leo.
RAS Balozi Dk. Batilda Buriani akieleza mipango na mikakati mbalimbali wanayotarajia kuifanya kusukuma mbele maendeleo ya mkoa huo
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru akizungumza kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Philemon Sengati na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Balozi Dk. Batilda Salha Buriani na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Juni 7,2021
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (aliyevaa suti na miwani) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao kilichowakutanisha leo ofisini kwake

Picha na Kadama Malunde

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464