Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua sehemu inayotumika kupakuwa mbolea wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es Salaam
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ipo kwenye mikakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kituo cha kuingiza mbolea na kusambaza kwa nchi zenye uhitaji.
Ameyasema hayo jana Juni 14, 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia shughuli ya upakuaji na uingizaji wa mbolea ndani ya nchi.
Amesema njia mojawapo ya kuhakikisha mbolea inashuka ni kuhakikisha mbolea nyingi inaingia nchini, na ili kufanikisha hilo lazima Tanzania iwe ni 'HUB’ ya kuagiza na kuingiza mbolea.
“Kwa bahati mbaya hivi karibuni Zambia walikuwa wanaleta mbolea kupitia bandari yetu lakini sasa hivi wanaleta kupitia bandari nyingine, tunataka warudi waingize mbolea kupitia bandari ya Dar es Salaam.
“Tunapenda wafanyabiashara walete mbolea kwa wingi hapa nchini, sisi tutaweka mfumo mzuri wa kuwarahisishia kuiondoa mapema ili kuipeleka Congo na Zambia au nchi nyingine yoyote wanapotaka kwenda kuuza,” Amesema
Waziri amesema kuwa hiyo ni hatua ya awali, nyingine wanatarajia kuimarisha uzalishaji wa mbolea ili kufanikisha kupatakana kwa wingi nchini.
“Kuna kiwanda kinajengwa Dodoma, yule wa Minjingu tumemwambia tutamlinda na aongeze ufanisi wa mbolea yake ili kazi iende mbele, hii itatusaidia sisi wakulima kupata mbolea kwa bei rahisi hivyo mazao yatauzwa pia kwa bei rahisi,” Amekaririwa Profesa Mkenda.
Amesema hatua hiyo inalenga katika kuongeza ushindani wa kuingiza mbolea na hiyo ndiyo sababu ya kuongeza muda wa zabuni ili kuwe na kampuni nyingi ambazo zitakuja kushindana kuleta mbolea.
Akizungumzia kuhusu bei ya mbolea Waziri Mkenda amesema kuwa, Kwa sasa inaongezeka duniani na hata nchini imeshapanda ambapo kati ya Juni mwaka jana na Juni mwaka huu bei imeongezeka kwa asilimia 50.
“Mahitaji ya mbolea nchini ni takribani Tani laki saba, wakati uzalishaji wetu ni chini ya laki moja, tayari wameanza mazungumzo na leo muwakilishi wa balozi wa Saudi Arabia na Qutar.
“Ni mojawapo ya nchi ambazo zinazalisha mbolea kwa wingi, na nitaendelea kufanya mazungumzo na mabalozi wengi kuwashawishi kampuni zao kule zije kuwekeza nchini hiyo itachangia bei zipungue,” Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt Stephan Ngailo amesema kuwa suala la vibali wameshaanza kuhakikisha wafanyabiashara wanaoomba vibali wanapatiwa kwa wakati.
“Tunataraji kuanza kuruhusu wafanyabiashara kuomba vibali kwenye kuingiza mbolea, wanapata hati ya kulipia kwa njia ya mtandao na kibali pia.
Amesema kuwa hiyo itarahisisha vibali kutolewa kwa wakati, hivyo itaongozeka ufanisi lengo kuhakikisha mkulima anapata mbolea bora bei rahisi na kwa wakati uliokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema amemueleza Waziri Mkenda kuwa TFRA imeboresha mfumo wa upakiaji wa mbolea unaofanywa kwa njia ya kisasa unaowezesha upakiaj kufanyika haraka.
Lema amesema kuwa mashine ya awali ilikuwa na uwezo wa kuakia mifuko 1500 kwa saa 24 lakini hiyo ya kisasa ina uwezo wa kujaza mifuko 3000.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akikagua ufanisi wa Bandari ya Dar es salaam katika upakuaji wa mbolea inayowasili nchini alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.