MSIMU ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara haitaitwa tena Vodacom Primier Ligue (VPL) baada ya Vodacom kuvunja mkataba wa kuendelea kuwa mdhamini wa Ligi Kuu kwa sababu mbalimbali zilizoelezwa na uongozi.
Vodacom imebisha haikusudii kuendelea na udhamini wa Ligi Kuu ya mpira wa Miguu Tanzania Bara sababu kuu ikitajwa kuwa mwenendo wake wa biashara usioridhisha. Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya awali ya kampuni hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi, 2021 Vodacom imepata hasara ya Sh30 bilioni tofauti na mwaka uliopita (Machi 2020) ambapo walipata faida ya Sh45.76 bilioni.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kampuni hiyo ambayo imekuwa ikidhamini Ligi Kuu kwa miaka 10 ilipata hasara kutokana na wateja wake zaidi ya milioni 2.9 kufungiwa laini zao kwa kushindwa kukamilisha usajili wa alama za vidole pamoja na sababu nyingine za kikodi.
Jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Hisham Hendi alisema imekuwa ni fahari kubwa kwa kudhamini ligi ya Tanzania ikiitwa jina lao kwa zaidi ya miaka 10 na itaendelea kuwa hivyo lakini kutokana mwenendo wa ufanisi wa kampuni hawataendelea.
“Tunafurahia ubia na tunaupenda, ligi imekuwa ikiitwa jina letu, lakini kwa kampuni ambayo inatengeneza hasara, leo usipoweza kuinuka juu lazima uangalie gharama zako na katika mazingira magumu lazima uchukue maamuzi magumu,” alisema.
Alisema udhamini wa ligi hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo yanawagharimu fedha nyingi kwani wamekuwa wakilipa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya udhamini lakini sasa hawana budi kuachia.
“Kila msimu tunatumia zaidi ya Sh3 bilioni, lakini pengine tunaweza kuwa na majadiliano na TFF kwa baadaye lakini kwa sasa tunapaswa kuchukua maamuzi magumu na sio kwa udhamini wa ligi pekee bali na mambo mengine ya kupunguza gharama,” alisema Hendi.
Alisema kama kampuni iliyoorodhesha katika soko la hisa na wanahisa wengi wanawatazama, hivyo ni muhimu kufanya maamuzi ambayo ni sahihi kwao. Hendi aliongeza wanamalizia msimu huu wa mwisho lakini kuanzia msimu ujao hawatakuwepo.
Mkataba wa Vodacom ulikuwa unamalizika msimu ujao na ameelezatayari wameiandikia barua TFF kuwafahamisha kuhusu suala hilo lakini TFF hawajaijibu.
Alipotafutwa rais wa TFF, Wallace Karia alieleza atafutwe Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo ambaye naye alisema hawana taarifa hizo na wakizipata watatoa taarifa rasmi.
CHANZO: Mwanaspoti