WANAHARAKATI HAKI ZA WATOTO SHINYANGA WASHAURI SERIKALI, WADAU KUUTUPIA MACHO MSAADA WA KISAIKOLOJIA KWA WAHANGA WA UKATILI

Afisa Mradi wa Kutokomeza ukatili wa Kijinsia kutoka Asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Jane Kashumba akizungumzia hali ya ukatili wa kisaikolojia kwa watoto wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) shuleni na kwenye familia

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
KATIKA kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, mwaka huu iliyobeba kauli mbiu ya ‘Tutekeleze Ajenda 2040: Kwa Afrika Inayolinda Haki za Mtoto’, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa imeendelea kuratibu mifumo ya msaada ya kutolea taarifa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kupitia simu ya bure Na 116 ambapo idadi ya taarifa zilizopokelewa kupitia simu imeongezeka kutoka simu 1,010,186 mwaka 2013 hadi simu 14,624 zilizopigwa mwaka 2020.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima Juni 9, mwaka huu jijini Dodoma, ilieleza kuwa jumla wa watoto 6,877 walipatiwa huduma mbalimbali baada ya taarifa zao kupitia simu ya 116 kufikishwa kwa mamlaka husika ukilinganisha na watoto 493 waliosaidiwa mwaka 2013. Vilevile Serikali imeendelea kuimarisha mifumo mingine ikiwemo uanzishaji wa kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto ambapo hadi Disemba, 2020 jumla ya Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 16,343 zimeanzishwa katika Halmashauri 184 kwenye Mikoa yote 26.

“Aidha, Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo 420 vya polisi nchini na vituo vya huduma ya mkono kwa mkono 13 katika mikoa 10 na nyumba salama 9 zimeanzishwa katika mikoa 7 ya Tanzania bara.  Serikali imetunga Sheria ya Msaada wa kisheria ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa haki kwa watoto kwa kupata uwakilishi wa msaada kisheria anapokuwa katika ukinzani na sheria. Vilevile, Serikali imeongezeka idadi ya mahakama zinashughulikia mashauri ya watoto kutoka 3 mwaka 2015 hadi mahakama 141 mwaka 2020 kwa ajili ya kufikisha huduma za mahakama ya mtoto jirani na walengwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Licha ya juhudi hizo za serikali katika kutoa msaada kwa wahanga wa vitendo vya ukatili, kupanua wigo wa kutoa taarifa na kushughulikia changamoto za Watoto wanaokumbana na vitendo vya ukatili, Wanaharakati na wadau wa masuala ya Watoto mkoani Shinyanga wameeleza kuwa ipo haja ya kutupia jicho suala la msaada wa kisaikolojia kwa Watoto wanaokutana na changamoto mbalimbali na wadau wote kuhakikisha kuwa ushahidi unalindwa na haki inapatikana kuliko hali ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya kesi huishia njiani.

Baadhi ya wadau hao yakiwemo mashirika ya AGPAHI, Green Community Initiatives (GCI), Women and Youth Development Solution (WAYDS), Thubutu Africa Initiatives (TAI) na Investing in Children and their Societies (ICS) wakizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa nyakati tofauti mjini Shinyanga kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, wameeleza kuwa ukatili wa kisaikolojia haupewi umakini hivyo kuendelea kuwaumiza watoto shuleni, kwenye familia, vituo na maeneo mengine.

Afisa Mradi wa Kutokomeza ukatili wa Kijinsia kutoka Asasi isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Jane Kashumba amesema kuwa Serikali inapaswa kuweka kwenye mitaala ya elimu ajenda na somo la ukatili wa kijinsia ili kuwafundisha watoto na jamii kwa ujumla juu ya jambo hilo ili kuzuia, wajue habari za kijinsia, jinsi ya kujikinga na wapi pa kwenda kupata huduma.

Amesisitiza kuwa kwa sasa ukatili wa kisaikolojia dhidi ya Watoto wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) umepungua kutokana na wahanga kutokuwa na magonjwa nyemelezi na matumizi sahihi ya dawa yamesaidia, huku akisema hali hiyo ya ukatili imebaki mashuleni kutokana na walimu kutokuwa na elimu ambapo kwenye shule za sekondari hufanya kaguzi za vifaa hadharani hali ambayo imefanya wanafunzi wenye VVU kutokwenda na makopo ya dawa.

Pia ukatili huo umebaki kwenye ngazi ya familia kutokana na kuwa mtoto anayeishi na VVU anatambulika na wanafamilia.
Meneja Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI), Paskalia Mbugani (kushoto) akizungumza na mwandishi wetu katika ofisi za shirika hilo

Meneja Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI), Paskalia Mbugani ameshauri wadau kushirikiana ili kesi za ukatili wa kijinsia na watoto zisipoteze ushahidi na hatimaye watoto wapate haki zao, pia msaada wa kisaikolojia kwa wahanga ni muhimu kwani ukatili wa kisaikolojia kwa mtoto hauzingatiwi, kwahiyo wadau na serikali wanapaswa kulifanyia kazi na kuhakikisha sheria zinatekelezwa ili kuleta matumaini katika vita hii na kuifanya jamii ihamasike kuona haki zinatendeka.

Katika kuifikia ajenda 2040, Paskalia ameshauri jamii na wapigania haki za watoto kuifahamu vyema ili kuwa na uelewa mpana wa yaliyomo kwenye ajenda hiyo na kufahamu mwelekeo sahihi na kile kinachokipiganiwa na serikali katika mipango na mikakati yake ilizingatie.

“Tunapenda kuona mabaraza ya watoto yanaunganishwa na kushirikishwa katika maamuzi yanayowaangalia Watoto. Tuna uhitaji mkubwa sana wa nyumba salama kwa watoto waathirika wa ukatili kwa sababu baada ya kutendewa wanarudi kwenye jamii ile iliyowafanyia ukatili, tunahitaji pia msaada wa kisaikolojia na bado watendaji wa idara ya ustawi wa jamii hawatoshi,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Women and Youth Development Solution (WAYDS), Charles Deogratias, amesema kuwa ili kupata maendeleo jamii inapaswa kushirikiana bila kuminya haki za watoto, vijana, wanawake ama watu wenye ulemavu na kupiga hatua kwa pamoja kama jamii bila kuacha kundi lolote nyuma na kubeba lingine.

“Mtoto wa Afrika hususan Shinyanga bado yuko nyuma kutokana na kuendelea kukabiliwa na changamoto za ukatili, unyanyasaji na ndoa za utotoni, hivyo tuitumie siku ya mtoto wa Afrika kupata suluhisho la kuzitatua changamoto zinazowakumba,” amesema.
Afisa Miradi wa GCI, Lucy Mosha

Kwa upande wa Asasi ya Kiraia ya Green Community Initiatives (GCI) ambayo inayojihusisha na kutetea haki za watoto na wanawake na kusimamia elimu jumuishi pamoja na masuala ya wazee na makundi ambayo hayapewi kipaumbele katika jamii wakiwemo watoto wenye usonji, wameshauri elimu ya kupamba na na aina zozote za ukatili itolewe na hamasa kwenye familia kutoa taarifa za vitendo hivyo bila kujali mahusiano yaliyopo ili kuvikomesha na kutokwamisha harakati za kumlinda mtoto.

Afisa Miradi wa GCI, Lucy Mosha amesema kuwa katika jamii yetu hususan Shinyanga baadhi ya watoto ndiyo wanaojitafutia kipato na kujilea hatimaye kujiingiza katika tabia hatarishi, ambapo ameshauri kuwa kunapaswa kuwa na uwajibikaji kwa wazazi na walezi ili kila mtu kwa nafasi yake awajibike kulinda ama kuona haki za mtoto zinalindwa.

Shirika la Investing in Children and Societies (ICS) ambalo limekuwa likitekeleza kazi zake katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu kwa kuwajengea uwezo Watoto waweze kuelewa namna ya kujilinda na kuwaelewesha wazazi kupitia mabaraza ya ulinzi wa mtoto, wameshauri kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja na wazazi waache kujisahau na kutotoa usaidizi kwa Watoto wao.

Meneja Miradi wa ICS, Sabrina Majikata, ameeleza kuwa ili mpango mkakati wa mkoa wa Shinyanga wa miaka mitano wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ufanikiwe, ni lazima usimamizi wa rasilimali uwe mzuri kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa, uwajibikaji wa wadau na serikali kwa watendaji kuwajibika ipasavyo kuhakikisha wanasimamia maslahi bora ya watoto.

“Jamii ibadilike hasa mila na desturi, kuna mambo tunapaswa kuachana nayo kwa sababu hayana afya na maslahi kwa watoto,” ameshauri.
Meneja Miradi wa ICS, Sabrina Majikata




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464